Kardinali Zuppi ni Rais Mpya wa Maaskofu wa Italia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa amechagua. Huyo ni Kardinali Matteo Maria Zuppi, mwenye umri wa miaka 66, ambaye ni askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Bologna, ambaye ndiye rais mpya wa Baraza la Maaskofu wa Italia (CEI). Uteuzi huo umekuja asubuhi tarehe 24 Mei 2022, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kwanza cha Mkutano Mkuu wa 76 wa CEI unaofanyika Hilton karibu na Uwanja wa Ndege kimataifa wa Fiumicino, Roma. Hata hivyo uchaguzi huo umetokea mara baada ya maaskofu kutoka pande zote za Italia kufanya uchaguzi wa watu watatu kwa ajili ya uteuzi wa mwisho wa rais ambaye angechukua nafasi ya Kardinali Gualtiero Bassetti, mwenye umri wa 80, na ambaye ni askofu mkuu wa Perugia-Città della Pieve.
Na alikuwa ni Kardinali Bassetti aliyemaliza muhula wake wa w Urais kwa miaka mitano na kutoa ufunguzi wake wa mwisho Jumanne asubuhi, 24 Mei 2022 kwa kusoma taarifa ya Baba Mtakatifu kuhusiana na chaguo la Kardinali Zuppi, kuwa wa kwanza kati ya watatu waliowasilishwa kwake. Kwa maana hiyo mara baada ya tamko hilo, maaskofu waliokuwapo walilipokea kwa kishindo cha makofi ambacho kimerudia tayari historia iliyofanyika katika muongo wa 1969-1979, wakati Baraza la Maaskofu Italia (CEI) waliongozwa na askofu mkuu Antonio Poma wa Bologna.
Kabla ya kuwasili Bologna, ambako Papa Francisko alimteua kuwa Askofu mkuu mnamo tarehe 27 Oktoba 2015,akimrithi Kadinali Carlo Caffarra, Kardinali Zuppi, anayejulikana na wote kama ‘Don Matteo’ na bado anaitwa hivyo, alianza historia yake ya kibinafsi na ya kikuhani jijini Roma. Kiukweli, alizaliwa katika mji mkuu, katika familia ya watoto sita: yeye ni wa tano. Hatua ya kwanza muhimu ni mnmo 1973, miaka ambayo alisoma katika shule ya sekondari ya Virgilio, mahali ambapo aliweza hata kukutana na David Sassoli, aliyekuwa rais wa baadaye wa Bunge la Ulaya (na ambaye hivi karibuni Kardinali Zuppi aliadhimisha misa ya mazishi yake mnamo Januari 14 mwaka huu) na kuunda uhusiano wa kina na wa kudumu na Andrea Riccardi, mwanzilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio.
Kwa maana hiyo Zuppi alinza kushiriki Jumuiya na kushirikiana katika shughuli za huduma kwa wale ambao wanahitaji msaada kwa mfano kutoka katika shule maarufu kwenda kwa watoto waliotengwa wa makazi duni ya Roma, hadi kufikia mipango ya wazee ambao wako peke yao na wasiojitegemea, wahamiaji na wakimbizi, wasio na makazi, wagonjwa mahututi , walemavu na wanaokula dawa za kulevya, wafungwa na waathirika wa migogoro. Vile vile hata katika hatua za kiekumene kwa ajili ya umoja kati ya Wakristo hadi kwa ajili ya mazungumzo ya kidini, ambapo hayatasaulika yaliyota mkutano huko Assisi.
Akiwa na umri wa miaka 22, baada ya kuhitimu masomo ya Fasihi na Falsafa katika Chuo Kikuu cha La Sapienza, kwa tasnifu katika Historia ya Ukristo, Kadinali wa baadaye alijiunga katika seminari ya jimbo la Roma huko Palestrina, akifuatilia kozi za maandalizi ya upadre katika Chuo Kikuu cha Kipapa Laterano na kupata digrii ya taalimungu. Tarehe 9 Mei 1981 alipewa daraja la Upadre kwa ajili ya mapadre wa Palestrina na mara baada ya hapo akawa Padre wa Parokia ya Kanisa Kuu la Kiroma la Mtakatifu Maria huko Trastevere, kwa kuchukua nafasi ya Askofu Paglia.