Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya V Ya Kipindi cha Pasaka: Amri Mpya ya Upendo iwe ni utambulisho kwa wafuasi wa Kristo Yesu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya V Ya Kipindi cha Pasaka: Amri Mpya ya Upendo iwe ni utambulisho kwa wafuasi wa Kristo Yesu. 

Dominika ya V ya Kipindi cha Pasaka: Amri Mpya Ya Upendo!

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Pasaka ni mwaliko kwa waamini kutafakari umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu hadi miisho ya dunia. Huko watakumbana na shida, matatizo na changamoto pamoja na furaha ya Injili. Amri mpya ya upendo unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu ni utambulisho muhimu sana wa Wakristo.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Pasaka. Katika dominika hii ya 5 ya Pasaka Mwaka C, somo la kwanza linatuelezea hali halisi ya Kanisa la wasafiri hapa dunia kuwa limepambwa kwa furaha na mateso, somo la pili linatufunulia uzuri wa Kanisa la washindi huku mbinguni linavyofurahia ushindi dhidi ya dhambi na mauti na Injili inaweka mbele yetu amri kuu mapendo kama kitambulisho cha wafuasi wa Kristo mbele za watu wa mataifa. Kuiishi vyema amri ya mpendo kunatustahilisha kuurithi ufalme wa mbingu. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 14:21b-27) ni hitimisho la safari ya kwanza ya kimisionari ya Paulo Mtume na Barnaba katika Asia ndogo. Katika Mdo 13 na 14 Luka anasimulia matukio ya furaha na huzuni yaliyotukia wakati wa safari ya kwanza ya kimisionari ya Paulo na Barnaba wakiongozwa na Roho Mtakatifu (Mdo 13:2-14:28). Safari hii ya kimisionari ilichukua takribani miaka 4. Somo hili linatueleza jinsi Paulo na Barnaba walivyohubiri kwa ujasiri na upendo mkuu kwa nguvu za Mungu, wakiwaimarisha waamini na kuwaonya wakae imara katika Imani, licha ya madhulumu na mateso; “Imewapasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi” (Mdo 14:22).Somo hili pia linatufundisha kuwa wazee wa Kanisa huchaguliwa na Roho Mtakatifu anayejidhihirisha kwa njia ya kusali, kuomba na kufunga, na kisha kuchaguliwa wanawekewa mikono ishara ya kumpokea roho huyo ili awaongoze. Kumbe mamlaka ya uongozi sio ya kujitwalia, kujichukulia, kujivika na kujitangaza.

Upendo kwa Mungu na jirani viwe ni utambulisho wa wakristo
Upendo kwa Mungu na jirani viwe ni utambulisho wa wakristo

Hili ni fundisho, onyo na angalisho kwa wanaowakimbilia “wachungaji feki” wanaoibuka katika nyakati zetu wakitangaza Injili ya mafanikio. Tutambue kuwa mbinguni tutaingia kwa njia ya dhiki nyingi na imani imara kwa Kristo na sio kwa mafanikio ya mambo ya ulimwengu huu. Katika mji wa Listra Paulo alimponya kiwete, hivyo wapagani wakafikiri kwamba Paulo na Barnaba ni miungu wakamwita Paulo “Hermes” na Barnaba “Zeus”, wakataka kuwatolea sadaka na kafara ya ng’ombe ili kuwaabudu. Paulo na Baranaba waliwakataza, wakararua nguo zao wakipiga kelele msifanye haya, sisi nasi tu wanadamu, hali moja na ninyi; twawahubiri Habari Njema ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na vitu vyote vilivyomo” (Mdo 14:8-18). Lakini Wayahudi waliomchukia Paulo walimfitinisha na umati ukamgeuka, ukamtoa nje ya mji na kumpiga kwa mawe. Naye Paulo alipoanguka chini, wakafikiri amekufa, wakakimbia wakamuacha. Baadae Paulo aliinuka na kuendelea na kazi ya kuhubiri katika mji wa Derbe na kuanzisha Jumuiya ya Kikristo (14:19-20).

Kutoka Derbe, Paulo na Barnaba walirudi Antiokia, kuiimarisha na kuitia moyo Jumuiya ya Kanisa la Antiokia ambayo ilikuwa bado changa kiimani (14:21-28), akiwaeleza kuwa chochote walichotenda ilikuwa ni kazi ya Mungu na si yao na kwamba wao walitumika tu kama vyombo vya utendaji vya Mungu. Na ya kuwa Mungu anawaita watu wote katika wokovu na siyo Wayahudi tu. Mungu anamwita kila mmoja katika wokovu kwa kuwa upendo wake ni kwa wanawake na wanaume wa Karne zote na mahali pote. Kumbe, tunaona kuwa katika safari zake za kitume Paulo alifanya mambo makuu matatu: Kuwafundisha watu dhamani ya zawadi ya imani aliyowapatia Mungu alipowaita kumfuata Kristo. Kuwateua wachungaji au wazee wa Kanisa kutoka ndani ya Jumuiya husika ambao walikuwa na jukumu la kuiongoza Jumuiya yeye anapoondoka. Kuwasaidia waumini wachanga kiimani – walioongokea Ukristo kutambua thamani ya mateso na taabu, katika maisha ya Kikristo.

Uinjilishaji mpya unasimikwa katika ushuhuda, kielelezo cha imani tendaji.
Uinjilishaji mpya unasimikwa katika ushuhuda, kielelezo cha imani tendaji.

Katika somo la pili la Kitabu cha Ufunuo (Ufu. 21:1-5a); Yohane anatupa picha ya Kanisa lisilo na dhambi na huzuni Kanisa la washindi-mbinguni.   Katika Kanisa hili hakuna taabu wala mateso maana kila kitu ni kipya - “Mbingu mpya na Nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi za kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena” (Uf 21:1).  Yerusalemu mpya ni mfano wa ufalme huo mpya na Mungu. Yohane anatumia lugha ya Agano la Kale ambapo neno dhambi likiwakilisha dunia makao ya mtu mdhambi na bahari makao ya shetani - “Je mimi ni bahari, au je ni nyangumi? Hata ukaniwekea ulinzi juu yangu? (Ayub 7:12). “Kisha nikaona mnyama akitoka baharini, mwenye pembe 10 na vichwa 7 na juu ya pembe zake ana vilemba 10 na juu ya vichwa vyake ana majina ya makufuru” (Uf 13:1). Mbinguni hakuna dhambi wala madhara yake (Isa 8:8). Katika somo hili tunaona utabiri wa Nabii Isaya; “mimi nataumba mbingu mpya na dunia mpya, na ya kale yote hayatakumbukwa,” (Isa 65:17), huko watu watapata raha na furaha; huzuni na masikitiko vitapotea kabisa, wala hakutakuwa na kifo (Isa 35:10), ukitimia. Mungu atafanya maskani yake pamoja na watu wake, atafuta kila chozi katika macho yao; wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Tazama, yote yanafanyika kuwa mapya kwa nguvu ya upendo wa Kristo alipokufa msalabani.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 13:31, 33a, 34-35); ni wosia wa Yesu kwa wafuasi wake alioutoa wakati wa karamu ya mwisho, kabla ya kukamatwa, kuteswa na kufa msalabani. Mara tu baada ya Yuda kuondoka Yesu aliwaaga wafuasi wake, akawapa amri mpya ya kupendana wao kwa wao: “Enyi watoto wadogo, bado kitambo kidogo nipo pamoja nanyi. Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi”. Wosia huu unakuwa ndio mwongozo wa maisha yao na ishara ya kuwatambulisha kuwa wao kweli ni wanafunzi wa Yesu. Kumbe upendo ni kitambulisho cha ufuasi wetu kwa Kristo. Wanafunzi wa kweli wa Kristo hujulikana kwa kushika amri hii mpya ya mapendo. Wakristo wa kweli hujulikana kwa kushika amri hii mpya. Katika Agano la Kale Amri ya kwanza inasema; “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote. Na amri ya pili inasema; “Mpende jirani yako kama unavyojipenda?” (Kumb 6:5, Wal 19:18). Hapa tunaona kama vile hakuna upya katika amri ya mapendo kwenye wosia wa Yesu kwa wanafunzi wake. Lakini kiuhalisia upo.

Amri ya mapendo katika sheria ya Agano la Kale ilisema; “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” (Wal 19:18). Yesu katika Agano jipya anatuambia; “Pendaneni kama nilivyowapenda mimi.” Zaidi sana kwa wayahudi jirani ni yule myahudi mwenzao tu tena asiyekuwa na matatizo. Myahudi aliyekuwa na matatizo hasa magonjwa waliyosadiki yanatokana na laana ya dhambi hakuthaminika wala hakupendwa ndio maana wengine walitengwa na jamii hasa wakoma. Yesu anaposema hii ni amri mpya anasisitiza; “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi”. Yesu ni mfano na kipimo cha mapendo kamili upendo unadai kujisadaka na kutoa uhai kwa ajili ya wengine. “Hakuna upendo mkubwa zaidi ya huu, kuutoa uhai kwa ajili ya wengine”. Upendo huu hauna vipimo wala vigezo bali unampenda mtu kwa kuwa ni mtu au binadamu kwa kuwa ni binadamu bila kuangalia undugu, ukabila, mafanikio, utajiri, uwezo wa kiakili au wenye sifa zinazotuvutia. Paulo anasema upendo huu unaovumilia daima, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli (1Kor. 4-6).

Upendo kwa Mungu na jirani ujenge ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi.
Upendo kwa Mungu na jirani ujenge ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi.

Upya wa amri hii ni kutokuwa na mipaka na matabaka. Hakuna kinachoweza kuuzuia. Ndiyo maana mtume Paulo anauliza, “nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?” (Rum. 8:35). Paulo anajibu; hakuna kiwezacho kututenga na upendo wa Kristo: wala kifo, wala uhai, wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni, wala yanayotokea sasa, wala yatakayo tokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa, (Rum. 8:38-39). Hivyo mapendo halisi na ya kweli hayachagui wala hayana ubaguzi. Mtume Yohane anatuasa; “Yeye asiyependa akaa katika mauti, na kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji; nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukaao ndani yake” (1Yoh 3:14-15). Upendo huu ndio utakaotufikisha Mbinguni. Ujio wa Kristo haukuwa kwa ajili ya kufanya maisha yetu hapa duniani yawe rahisi. Ujumbe wa injili aliutoa Yesu sio injili ya utajiri wa mali na madaraka na ufahari. Bali ni kuubeba msabala na kumfuata. Inahitaji upendo kuwa na nguvu ya kuubeba msalaba. Taabu tuzipatazo katika kuuishi wosia wa Kristo wa kupendana, visitukatishe tamaa bali vituimarishe. Upendo ni neno rahisi kulitaja lakini ni vigumu kuliishi. Upendo si lelemama, unagharimu. Uligharimu uhai wa Yesu. Ndiyo maana alisema; “hakuna upendo ulio mkuu zaidi ya ule wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili rafiki zake. Basi, tujipe moyo hata kama tunaishi upendo kwa dhiki, dhiki yetu haitapotea bure. Utafika wakati Mungu atakapofuta kila chozi katika macho yetu na kutujalia uzima wa milele huko mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 5 Pasaka
09 May 2022, 07:23