Tafuta

Safari za kimisionari za Paulo na Barnaba, ni vielelezo wazi vya upendo kwa Kristo. Walikuwa tayari kuacha starehe binafsi na kujisadaka kwa ajili ya  ya kutangaza na kushuhudia Injili. Safari za kimisionari za Paulo na Barnaba, ni vielelezo wazi vya upendo kwa Kristo. Walikuwa tayari kuacha starehe binafsi na kujisadaka kwa ajili ya ya kutangaza na kushuhudia Injili.   (Vatican Media)

Dominika V ya Kipindi Cha Pasaka: Changamoto Za Uinjilishaji Mpya! Ushuhuda Wa Upendo

Silaha za mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ibada ya Rozari isaidie kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani na familia inayo sali pamoja, hiyo itadumu.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na Msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tano ya Kipindi cha Pasaka ya Mwaka C wa Kanisa. Tunaendelea na Mwezi wa tano Mwezi wa Bikira Maria, Mwezi wa Rozari. Ikumbukwe kwamba, Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Mwezi Mei ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, silaha za mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni: Tafakari ya Neno la Mungu, Sala, Sakramenti ya Upatanisho pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ibada ya Rozari Takatifu isaidie kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani na familia inayo sali pamoja, hiyo itadumu. Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 14:21b-27). Inatia moyo sana jinsi Mitume walivyojaribu kadri wawezavyo kufuata upendo wa Yesu. Safari za kimisionari za Paulo akifuatana na Barnaba, ni vielelezo wazi vya upendo kwa Kristo. Walikuwa tayari kuacha starehe binafsi na kujisadaka kwa ajili ya  ya kutangaza na kushuhudia Injili. Hilo ndilo jambo kuu  kwetu leo. “Inatupasa sisi kupata taabu nyingi ili kuingia katika ufalme wa Mungu.” (Mdo 14:22) ...)

Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa maneno na matendo
Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa maneno na matendo

Upendo wao kwa Bwana Yesu Kristo hufuta kabisa tamaa zote za ubinafsi na za kilimwengu. Pamoja na hayo tumesikia wakaweka baadhi ya wazee waendelee kuwaimarisha badala yao kwani wao walienda sehemu nyingine. Kabla ya kuwasimika walifunga na kusali. Paulo na Barnaba waliendelea kufundisha sehemu mbalimbali. Mwishowe, hata walitoa maisha yao kwa ajili ya Kristo. Somo la pili ni kutoka katika Kitabu cha Ufunuo sura 21:1-5a). Mtume Yohane alieleza maono yake ya mbingu mpya na dunia mpya. Ni jambo ambalo linapaswa kutia hamasa kwa kila mmoja wetu na kubaki waaminifu kwake nyakati zote. Bila kujali majaribu na mateso mengi tunayokumbana nayo katika ulimwengu huu. Kila kitu kinapita. Kuna mbingu mpya na nchi mpya. Mungu atakaa nasi - hiyo ndiyo sababu kuu Mtakatifu Yohane alieleza jambo hilo kwa kusema: “Mungu atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na hakutakuwa na kifo tena wala maombolezo, kilio wala maumivu.” Hayo yote utimilifu wake ni mbinguni! Na kwa sababu hiyo, Mtakatifu Paulo alihitimisha kwamba mateso ya maisha ya sasa si kitu ikilinganishwa na utukufu unaowangoja watoto waaminifu wa Mungu.

Injili ya Dominika ya tano ya Kipindi cha Pasaka ya mwaka C wa kanisa (Yoh:13:31-33a,34-35) inatupa sehemu ya tukio la Karamu ya mwisho. Hii ilikuwa ni baada ya Yuda Iskariote kuondoka katika chumba cha juu ili kukamilisha kitendo chake cha usaliti. Kisha Yesu anatoa fundisho na amri yake muhimu zaidi kwa wanafunzi wake, kii cha fundisho lake ni upendo. Injili inasema: “amri mpya nawapa mpendane kama nilivyowapenda ninyi”. Kuifuata amri hii ndiyo njia pekee ambayo kwayo tutajulikana kuwa wakristo, wafuasi. Maana anasema “watu watatambua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu mkipendana ninyi kwa ninyi” lakini pia licha ya kuwapa amri ya upendo yeye mwenyewe anawaaga na anapowaga anasistiza kupendana wao kwa wao. Anasistiza amri ya upendo kumpenda jirani. Upendo ni neno la kawaida sana. Kwa kweli, tunaitumia kwa urahisi sana na tuna tabia ya kuipunguza makali yake. Ni mara chache tunatambua ukuu na undani wa maana yake na uzito wa changamoto yake. Katika injili, Yesu alitoa sifa muhimu sana kwa upendo: Yesu anasema “mpendane kama vile nilivyowapenda ninyi” kwa maneno mengine, Yesu anatuhimiza tufuate aina yake ya upendo, yaani, upendo wa kujisadaka, hata kufikia hatua ya kijitoa kwa ajili ya wengine.

Upendo wa kweli ni kielelezo na utambulisho wa Wakristo
Upendo wa kweli ni kielelezo na utambulisho wa Wakristo

Mama Theresa wa Calcuta anasema: “Upendo wa kweli husababisha maumivu. Yesu, ili kutupa uthibitisho wa upendo wake, alikufa msalabani. Kwa sababu alitupenda upeo. Upendo wa kujitoa sadaka inayouma. Upendo hufanya imani kuwa kweli na kuunganisha., inaondoa ubinafsi. Mama Theresa wa Calcutta anasema: “Ikiwa imani ni haba, ni kwa sababu kuna ubinafsi mwingi duniani. Imani, ili kuwa ya kweli, lazima iwe na ukarimu na kutoa. Upendo na imani huenda pamoja.” Lakini haijawa hivyo kwa watu wengi. Tuna mwelekeo wa kutenganisha imani na upendo. Tunaomba na kumwabudu Mungu, lakini mioyo yetu ni ya ubinafsi. Upendo wa kweli hauhitaji kuwa wa pekee na wa ajabu. Hatuhitaji kuwa mashujaa katika matendo yetu ya upendo. Hatuhitaji kufanya matendo ya ajabu ya utume. Kinachohitajika tu ni kufanya mambo kwa upendo wa dhati, bila msukumo wowote wa ubinafsi. Mama Theresa ana maneno kamili kwa hili: "Mungu ametuumba hivyo tunafanya mambo madogo kwa upendo mkubwa." Upendo ndio alama pekee ya kweli ya Mkristo. Sisi sote ni wafuasi wa Kristo. Lakini si wote ni wafuasi wa kweli.

Wengi ni Wakristo kwa majina, wengine ni kwa urahisi, na wengine wengi ni Wakristo wa msimu. Kwenda Kanisani wengine ile Siku ya Jumatano ya Majivu tu hadi mwaka mwingine jumatano ya majivu, wengine ijumaa kuu au pasaka tu, wengine kukiwa na tukio fulani la familia nk. Tukirejea Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho, sura ya 13 anasema: kama mtu ana karama zote za Roho Mtakatifu  lakini kama hana upendo ni bure. Kwa maneno mengine, thamani ya chochote tunachofanya itakuja tu tunapofanya kwa upendo. Hapo ndipo tunaweza kuchukuliwa kuwa wafuasi wa kweli wa Kristo. Katika somo la pili tumesikia maono mazuri ya Mtakatifu Yohane: mbingu mpya na dunia mpya na kisha Mji Mtakatifu ukishuka kutoka kwa Mungu. Kila kitu ni kipya, kimebadilishwa kuwa kizuri, uzuri, ukweli; hakuna tena maombolezo,... Hili ndilo tendo la Roho Mtakatifu: anatuletea mambo mapya ya Mungu; anakuja kwetu na kufanya vitu vyote kuwa vipya, Roho anatubadilisha! Na maono ya Mtakatifu Yohane katika Kitabu cha Ufunuo yanatukumbusha kwamba sisi sote tuko njiani kuelekea Yerusalemu ya mbinguni, jambo jipya kabisa kwetu, na kwa ukweli wote, siku ya furaha ambayo tutaweza kuuona Uso wa Bwana, wa ajabu. uso, mzuri sana wa Bwana Yesu.

Tunaweza kuwa pamoja naye milele, katika upendo wake. Tukiendelea pia na Mwezi wa Bikira Maria, Mwezi wa kusali na kutafakari Rozari Takatifu, tukumbuke kwamba,  jina "Rozari" linatokana na neno la Kiingereza "rose", aina ua la waridi. Na "Rosarium" kwa lugha ya Kilatini ina maana halisi "bustani ya mawaridi". Ndiyo maana tunaposali rozari kwa majitoleo kamili na uchaji wa Mungu, tunamtolea Bikira Maria bustani ya waridi, ya nyoyo zetu ambayo hainyauki wala kufa. Na hii ndiyo njia yetu ya kuonesha upendo wetu na majitoleo yetu kwa Mungu na jirani. Tuombe kwa maombezi ya Bikira Maria Malkia wa Amani, Ulimwengu ujaliwe: haki, amani, ustawi na maendeleo ya kweli.

Dominika 5 Pasaka
10 May 2022, 14:44