Tafuta

Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mwaka 2022 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 Tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mwaka 2022 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 Tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. 

Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu Jimbo Zanzibar

Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika salam na matashi mema kwa Askofu Augustine Ndeliakyama wa Jimbo Katoliki la Zanzibar anayeadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu, anazungumzia: historia ya maisha yake, changamoto za kitume, suluhu na umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Na Askofu Flavian Matindi Kassala, Dar es Salaam, Tanzania.

Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. wa Jimbo Katoliki Zanzibar alizaliwa tarehe 25 Septemba 1951 huko Mengwe, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi na Kitawa, tarehe 4 Juni 1983 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Novemba 1996 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar na kuwekwa wakfu kuwa Askofu, tayari: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Zanzibar tarehe 27 Aprili 1997. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam akishirikisha na Askofu Mstaafu Bernard Martin Ngaviliau, C.S.Sp. wa Jimbo Katoliki Zanzibar pamoja na Askofu Mstaafu Dennis Vincent Durning wa Jimbo Katoliki la Arusha. Katika Nembo yake ya Kiaskofu akachagua maneno: “Pax et Unitas” yaani “Amani na Umoja” iwe ni dira na mwongozo katika utume wake wa Kiaskofu. Imegota miaka 25 ya Uaaskofu. Kumbe, maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na chombo cha amani, umoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu Shao ni mtoto wa pekee aliyebatizwa miaka mitatu baada ya kuzaliwa.
Askofu Shao ni mtoto wa pekee aliyebatizwa miaka mitatu baada ya kuzaliwa.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. alibatizwa miaka mitatu baada ya kuzaliwa, akiwa ni mtoto pekee ambaye alibahatika kupata Sakramenti ya ubatizo kama mtoto mchanga katika familia yake. Baadaye aliingia katika safari yake ya masomo ya awali ambapo alihitimu na kuingia masomo ya shule ya sekondari. Alipenda kwenda shule za seminari, lakini alikataliwa kujiunga na seminari kwani baba yake mzazi alikuwa hajaingia imani ya kikristo. Aliamua kukaa nyumbani na kujiandalia mahali pa kuishi kutokana na urithi alioupata toka kwa baba yake. Alikwenda nchini Kenya na kujiunga na seminari ambapo Padre aliyempokea alimpangia kuingia seminari ya Jimbo. Hata hivyo nia yake ilibaki kuwa ni Padre Mtawa wa Shirika la Roho Mtakatifu. Baada ya kumaliza masomo ya awali aliendelea na majiundo ya malezi ya Kipadre katika Seminari kuu ya Mama wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki la Moshi. Kisha aliendelea na malezi ya kitawa kwa kuingia Unovisi.  Baadaye aliingia Seminari Kuu ya Taalimungu na hatimaye kupewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 4 Juni 1983 Aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Zanzibar mwaka 1997: ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Zanzibar.

Katika utume wake Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. aliingia Zanzibar ambayo bado haikuwa rahisi kuinjilisha, ikiwemo kufungua Makanisa katika baadhi ya maeneo. Alijikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pamoja na hali hiyo, bado alitiwa moyo kuona kuwa mtangulizi wake ambaye alifanyakazi katika marufuku kabisa ya kueneza Ukristo, bado alifungua baadhi ya vigango. Askofu Shao alikumbana na pingamizi karibu sawa kuhusu uhuru wa dini, hata kama mbinyo wa awali ulikuwa umepungua kiasi. Alitumia mali iliyonunuliwa na mtangulizi wake, hasa ardhi, kulisimika Kanisa Katoliki Visiwani Zanzibar. Walilazimika kununua nyumba za watu na kuzibomoa ili kupata eneo la kujenga Makanisa. Pamoja na juhudi zote hizo, bado idadi ya Wakatoliki katika baadhi ya maeneo bado ni changamoto pia katika ukuaji wa Kanisa hata nyakati hizi. Makanisa kama majengo yanaendelea kuongezeka, lakini kama idadi ya waamini Wakatoliki katika baadhi ya maeneo inategemea watumishi wa umma na wawekezaji wa utalii tu. Wakati huo huo, baadhi ya maeneo yana matumaini makubwa katika ukuaji wa Kanisa, hasa pale ambapo wakazi wakatoliki wanamiliki ardhi yao. Katika kuhakikisha kuwa mbegu ya Injili inawagusa watu wote wa Mungu Visiwani Zanzibar, Kanisa Katoliki limebaki kujikita zaidi katika huduma za afya, elimu, maendeleo na ustawi wa jamii. Hali hii imeliwezesha Jimbo Katoliki la Zanzibar kufikisha Parokia 12, hali katika huduma za kijamii likiendelea kuwagusa watu wengi zaidi kwa ushuhuda wa Injili ya huruma na mapendo.

Askofu anawekwa wakfu ili kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu
Askofu anawekwa wakfu ili kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu

Miito ya Upadre bado imeendelea kuwa ni changamoto. Vijana wengi wanaojitoa kwa wito wa upadre wanatoka nje ya Zanzibar. Hali hii imeleta minong’ono kutoka kwa wenyeji wakazi wa visiwa hivi. Wachache wazawa waliojitokeza kwa wito wa Upadre ilikuwa ni ngumu hata kufuata masomo ya seminari. Bahati mbaya kiwango cha elimu cha Zanzibar kilikuwa chini kidogo ukilinganisha na cha Bara, na hivyo hawakuweza kuendana na sifa zilizohitajika katika seminari waliyopelekwa ya Mtakatifu Petro huko Morogoro. Jimbo halikukata tamaa, liliona bado kuna haja kubwa kwa Zanzibar kuwa na Mapadre wazawa, Wazanzibari. Hivyo waliwekeza katika kuinua kiwango chao cha elimu hapa hapa Zanzibar ili vijana wao watakapotoka kwenda katika Seminari na shule za sekondari za Bara waweze kuendana na kasi ya huko. Kupitia mpango huo walifanikiwa kupata vijana 6 walioingia katika seminari ya Mtakatifu Petro, Morogoro, huku wengi wa wavulana na wasichana wakiingia katika shule za sekondari huko huko Bara. Mafanikio ya kuwekeza katika sekta ya elimu yaliwaleta vijana wengi wa kike na wa kiume katika ulimwengu wa wasomi. Pamoja na ukweli kwamba, Jimbo Katoliki la Zanzibar halijafanikiwa kupata mapadre wazawa kutokana na mfumo huu, lakini vijana wengi Wazanzibari wamefanikiwa kuingia katika ulimwengu wa wasomi, wakiwemo madaktari, wanasiasa mahiri pamoja na wataalam wa nyanja mbalimbali.

Kutokana na mafanikio haya, Jimbo liliamua kuwekaza katika kutafuta jinsi ya kuinua kiwango cha elimu ya juu humu humu Visiwani Zanzibar. Hata hivyo, vurugu za kidini na misimamo mikali ya kiitikadi zimerudisha nyuma sana juhudi hizo za kuwekeza katika elimu ya juu. Hata mpango wa kupata kituo kilichoanzishwa kwa mpango huo zilikwama kutokana na vurugu za kisiasa. Kwa sasa Jimbo Katoliki la Zanzibar limefungua shule ya Seminari ya awali, yaani darasa la kwanza hadi la saba, katika kituo hicho hicho, hali wanafunzi hao wakipatiwa malezi endelevu pia. Huduma za kijamii zimepanuka kupitia juhudi na ushiriki wa Kanisa. Kwa sasa Jimbo Katoliki Zanzibar linashiriki katika kutoa ushauri nasaha hasa kwa waathirika wa Ugonjwa wa Ukimwi. Pia kuna kituo maalum cha kushughulikia usimamizi wa haki za binadamu visiwani. Haki za kijinsia ni tatizo kubwa visiwani. Kupitia kituo hiki, Kanisa limefanikiwa kupambana na tatizo hilo hadi kufikia kwamba sasa linafanyakazi kwa kushirikiana na serikali na vyombo vyake katika kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na usawa wa kijinsia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Linampongeza Askofu Shao kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Linampongeza Askofu Shao kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu

Uzoefu wa Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. umekuwa na mchango mkubwa sana katika ustawi, maendeeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania katika ujujmla wake.  Kwa upande wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika kutumia uzoefu wake wa Visiwani, Askofu Shao amesimamia kitengo cha fedha na ajira kwa miaka mingi. Ameleta mafanikio makubwa katika Kanisa, na hasa katika nyanja za uwekezaji na kujitegemea. Kanisa limechukua daima njia ya kujitegemea na kupanua wajibu wake wa uinjilishaji pia katika kupitia shughuli za uzalishaji. Ni katika sera na mikakati ya shughuli za kiuchumi, kielimu na kiafya, Kanisa Katoliki Tanzania limekuwa na mahusiano makubwa na Serikali kama mdau muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mazingira magumu na changamoto za hali ya kidini na kisiasa Zanzibar vimekuwa na mchango mkubwa kwa Askofu Shao, ambao ameutumia kuwatia moyo ndugu zake wa Kanisa la Tanzania. Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” unakazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu ambao unapaswa kunafsishwa katika ujasiri na ukarimu, ili kutafuta suluhu ya changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu. Udugu ni chombo madhubuti kinachopaswa kuwatetea maskini na wanyonge, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; haki na amani kama chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, C.S.Sp. ni shuhuda wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu Shao Jubilei
09 May 2022, 15:23