Tanzania:Jubilei ya fedha ya utume wa watawa wa Mtakatifu Karoli Borromeo
Na Angella Rwezaula–Vatican;&Thompson Mpanji Jimbo kuu Mbeya-Tanzania.
Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya pamoja na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwawa Jimbo katoliki la Iringa Tanzania, kwa pamoja wameungana kuwapongeza na kuwashukuru watawa wa kike wa Shirika la Mtakatifu Karoli Borromeo katika kutimiza miaka 25 ya utume wao tangu kuingia nchini Tanzania wakijikita katika nyanja ya Elimu, Afya na Jamii kwa ujumla. Katika maadhimisho ya misa Takatifu, iliyoongozwa na Askofu Mkuu Nyaisonga, akisaidiana na Askofu wa Iringa, ambayo ilifanyika katika makuu ya Shirika hilo, tarehe 11 Aprili 2022 huko Frelimo, jimboni Iringa, maaskofu hao kwa nyakati tofauti waliweza kushukuru umisionari wao barani Aftika hasa nchini Tanzania na Uganda. Katika pongezi hizo, za maaskofu wamekumbuka jitihada mbalimbali hasa za kukuza na kuendeleza shule zao wanazoziendesha kitaaluma, kwa kuleta manufaa makubwa kwa watu wa Mungu na Taifa lake pia. Katika maadhimisho hayo, mahubiri yalitolewa na Askofu Ngalalekumtwa ambaye kwa hakia aliwaomba wakristo wote kuwapongeza wamisionari ha ona kuwaombea kwa sababu alisema wanalo deni kubwa na zito la shukrani kwao kwa utume huo katika uwanja mpana wa elimu, afya kwa wote na jamii kwa ujumla.
Walifika jimboni mnamo 21 Mei 1997
Akisoma historia fupi ya Shirika, Sr. Litty George, amesema, kwamba wakati wa siku ya Pentekoste mnamo tarehe 26 Mei 1996, Mama Mkuu wa Shirika Sr. Andrea na Makamu wake Sr. Victoria Braganza, walianza safari yao ya umisionari hadi Iringa nchini Tanzania. Hao waliguswa, na wakaamua kutuma watenda kazi katika shamba la Bwana ambapo watawa wa kwanza walikuwa ni: Sr. Punithavathy Fernando, sr Mangala Maria na Sr. Jansi Joy kwa kusindikizwa na Sr. Victoria Braganza aliyekuwa Makamu wa Shirika. Kwa kujazwa na Roho ya Bwana, walifika kwa ujasiri na kwa utii manmo tarehe 19 Mei 1997 na kupokelewa na Mwakilishi wa Askofu wa Iringa ambaye kwa sasa ni Marehemu, Padre Libaratus na Mwakilishi wa Wasalesiani wa wakati huo aliyekuwa ni Padre Sajan katika uwanja wa ndege Dar es Salaam. Kwa maana hiyo walifika jimboni Iringa mnamo tarehe 21 Mei na kupokelewa kwa shangwe kuu na Wakristo na Familia ya Mungu jimboni Iringa na kupewa nyumba ya kuishi na mapadre wa Salesiani ili kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja wakati wakiandaliwa makao rasmi ya kwao.
Uhitaji wa watu uliwateka mioyo ya watawa
Akiendelea kuelezea historia hiyo ya shirika alibainisha kwamba walikuja, walishuhudia kwa usahihi wa uhitaji mkubwa wa watu wa hapo ambao uliwateka mioyo yao. Jubilei ni muda au wakati wa kutazama nyuma kwa shukrani na kutazama mbele kwa matumaini. Kitabu cha Mambo ya Walawi kinaonesha mazingira ya Jubilei, kama tukio la ukumbusho wa shukrani kwa matukio yaliyopita kwa kufurahi kwa sababu ya neema zilizopokelewa pia kwa kutambua uaminifu wa Mungu. Ka maana hiyo katika taarifa yao walisema kwamba kwa kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 ya uwepo wao ni ushuhuda ambapo maisha ya watu wengi yameguswa, wameponywa na kuletwa katika ukamilifu. Mbegu hiyo ndogo ya ushuhuda iliota na kueneza mizizi na machipukizi yake nchini Tanzania na Uganda.
Utume Tanzania na Uganda
Kwa sasa shirika hilo lina jumla ya Jumuiya 7 nchini Tanzania na jumuiya 2 nchini Uganda. Kwa ujumla ni watawa 47 miongoni mwao 21 ni wazalendo na bado idadi inaongezeka kila siku. Wanamshukuru Mungu azidi kutenda miujiza yake katika maisha yao na utume wao. Kwa namna ya pekee wamependa kuwakumbuka wote waliowasadia kwa kipindi chote na walipokaa katika jumuiya zao za Iringa, Kibaha, Dar es salaam, Morogoro, Mbeya, Mbinga na Dodoma na huko Uganda eneo la Nebbi na Koch. Kikweli walisisitiza kwamba utume wao una mafanikio kwa sababu ya misaada na michango ya watu mahalia na wengine wengi waliowasaidia na kuwasindikiza bila kuchoka. Kwa njia hiyo wamewashukuru sana na wanazidi kuwaombea. Kwa kuhihitisha walipenda kutumia fursa hiyo kuwashukuru tena watu wote wa Mungu kwa kutenga muda wao maalum kushiriki pamoja nao katika kuadhimisha Jubilei hiyo ya fedha kwa ajili ya utume wao mtukuka kwa Watu wa Mungu. Wameinua sala zao kwa Mungu kwa ajili yao katika misa hiyo na kumwomba Mungu zaidi kuwabariki sana.
Moyo wa shukurani kwa Mungu kwa makuu waliyotendewa
Naye Mkuu wa Shirika wa kanda ya Afrika, Sr. Sagaya Marry Raju katika mahojiano maalum amesema wamejazwa na Moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, wakiwakumbuka manabii walioitwa na kuchaguliwa kwa ajili ya huduma yake, hasa masista wa Mtakatifu Karoli Borromeo. Akiendelea alisema kwamba cheche za moto ziliwaka na Halmashauri Kuu ikishirikiana na Mkuu wa Shirika ilisukumwa na wito wa Roho Mtakatifu hadi kufika Afrika Mashariki na kwa namna ya pekee jimboni Iringa. Na wakati wa kutafuta kwao, Mkuu wa shirika Mama Andrea, alikutana na Padre Stephen Chemmalakuzhy (SDB), aliyekuwa Mkuu wa Shirika la Wasalesian wa Don Bosco, kanda ya Afrika Mashariki, ambaye baada ya kushauriana na Padre Tony Fernandes aliyekuwa Gombera wa Jumuiya ya Wasalesian jimbo la Iringa kupitia kwa Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo la Iringa, aliwazawadia eneo la kukaa na kuendeleza utume wao.