Maaskofu Sudan:tumaini la kujipyaisha kiroho wakati wa ziara ya Papa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Maaskofu katoliki wa Sudan Kusini na Sudan wamewataka waamini kutumia wakati huu wakiroho katika maadhimisho ya Pasaka kwa ajili ya kufanywa kwa upya na kusali huku wakitafakari kuhusu ziara ya Baba Mtakatifu Francisko mwezi Julai mwaka huu. Katika barua yao ya pamoja ya kichungaji ya Pasaka kwa majimbo yote ya Nchi mbili, maaskofu hawa wanaomba mwaka huu wa maadhimisho ya Pasaka kuiishi kwa imani na kupyaisha katika kuandaa kumpokea Baba Mtakatifu. Maskofu wamesema “Sherehe ya Pasaka ni ufufuo wetu kutoka katika upumbavu wetu, na kutokuwa na tumaini hadi kufikia tumaini jipya katika Kristo, na hadi kuwa na mwanzo mpya unaooneshwa na furaha ya Kristo mfufuka anayepyaisha maisha”.
Watu wengi bado wanakufa kutokana na vita
Maskofu hao wameeleza kuwa sherehe za Pasaka zimechanganyikana na hisia za baraka na mwaka mgumu, kwa kuwa nchi zote mbili bado zinakabiliwa na migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ukame na watu kuyahama makazi yao. “ Watu wengi bado wanakufa kutokana na vita, wanawake, watoto na wazee kuuawa, na hata wagonjwa kuuawa katika vitanda vyao vya wagonjwa. Kaka na dada zetu wengi bado wako kwenye vituo na makambi ya wakimbizi na wengine bado wako uhamishoni. Wanaishi bila uhakika iwapo wanaweza kweli kuungana tena na familia zao. Tunajua maeneo makubwa ya nchi yetu yanakabiliwa na mafuriko na msimu wa mvua unapoanza, hofu inatanda mioyoni mwao iwapo mafuriko hayo yatapungua hata kidogo”.
Papa anakwenda kuwathibitisha imani
Hata hivyo, maaskofu wa Sudan yote wanatumaini kwamba viongozi wa kisiasa na wanasema: “hawataturudisha vitani ili kuondoa msukosuko wa kibinadamu na kuandaa njia kwa ajili ya haki, amani na upatanisho.” Katika barua yao ya kichungaji, maaskofu wanafichua nia ya ziara ya Papa Francisko na kusema kwamba anakwenda kuwasilisha ujumbe huo wa Mtakatifu Petro kama ilivyoandikwa katika Matendo ya mitume (10:34). “Papa anafanya ziara Sudan Kusini, ili kututhibitisha kiimani, kama Mtakatifu Petro alivyofanya kwa wenzake Mitume. Ziara yake ni kuwasilisha amani ambayo ni zawadi ya kwanza ya Kristo mfufuka kwa wanafunzi wake kwamba “Amani iwe nanyi” (Yn 20; 21).
Ziara ya Papa inaweza kuwafanya kuwa wapya
Maaskofu wa Sudan na Sudan Kusini wanakumbuka ishara yake ya kugusa moyo, busu la miguu ya viongozi wao wa kisiasa, ombi la unyenyekevu lakini la huruma kwa amani ya nchi yao. Hii ni kuhusu mkutano wao wa kiroho uliofanyika mjini Vatican mnamo 2019. Maaskofu kwa maana hiyo wanatumaini kuwa ziara yake itawafanya upya, kwani bado wanatikiswa na nguvu za vurugu, vifo na uovu wa migawanyiko ya kikabila ndani ya Kanisa na jamii yao. Maaskofu katoliki wa Sudan Kusini na Sudan wametoa tamko hilo siku ya Jumatatu tarehe 11 Aprili 2022, mara baada aiku chache za Mkutano wa ziada wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan uliofanyika jijini Juba kuanzia tarehe 21 hadi 23 Machi 2022 wa matazamio na maandalizi ya ziara ya Papa nchini Sudan Kusini kuanzia tarehe 5 hadi 7 Julai 2022.