Tafuta

Kardinali  Berhaneyesus D. Souraphiel CM,Askofu Mkuu wa  Ethiopia Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel CM,Askofu Mkuu wa Ethiopia 

Ethiopia:Yanahitajika mazungumzo ya amani ya kudumu kusitisha vita

Kardinali Berhaneyesus Souraphiel,anatumaini kwamba mazungumzo yanayoendelea yaweze kuleta ufanishi wa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe katika Mkoa wa Ethiopia.Kardinali huyo ameelezea wasiwasi wake mkubwa juu ya janga kubwa la kibinadamu ambalo limeikumba nchi ya Pembe ya Afrika na hasa kwa sasa ukosefu wa msaada na balaa la njaa kali kwa wati walioathirika na vita hivyo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Papa Francisko anaendelea kuwaalika ulimwengu mzima kutazama kile kinachoitwa vita vilivyosahaulika, kama vile vilivyoikumba Ethiopia kwa miezi kadhaa. Katika mahojiano na Radio Vatican, Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Addis Ababa, na mkuu wa Kanisa Katoliki la Ethiopia, kwa kutumia maneno ya Baba Mtakatifu, amezungumzia juu ya janga la kibinadamu linaloikumba taifa la Ethiopia kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na njaa. Kardinali amesema kuwa mazungumzo yanayoendelea yalete amani ya kudumu. Na kiukweli, vita na njaa vinawakilisha mkanganyiko wa kushangaza ambao unaipeleka Ethiopia kwenye mzozo ambao unahatarisha maisha ya wengi. Yote yalianza tarehe 4 Novemba 2020, siku ambayo mzozo kati ya Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray (TPLF) na jeshi la Ethiopia ulizuka. Kardinali Souraphiel amezungumzia hali mbaya, hata kama kumekuwa na uboreshaji na kuanza kwa mazungumzo. Kwa hakika, zaidi ya watu milioni 2 wameyakimbia makazi yao na maelfu wamekufa kutokana na vita, na mamilioni zaidi ya Waethiopia wanahitaji sana msaada wa kibinadamu.

Usaidizi wa nchi ili kuwa na upatanisho wa kudumu

Kiongozi wa Kanisa Katoliki la Ethiopia la mapokeo ya Aleksandria, ambapo waamini wake kwa sasa wanaishi kipindi cha Kwaresima kwa mtazamo wa Pasaka, mnamo tarehe 24 Aprili 2022 ameelezea jinsi wanavyo jitayarisha kwa Juma Kuu Takatifu na Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana.  Amesema kwa kawaida Watu hushiriki katika Njia ya Msalaba, kusali na kufunga kwa kuzingatia Pasaka Takatifu ili kuishi pamoja kama familia, kwa sababu, anakumbusha kuwa Pasaka ni sikukuu ya familia. Kardinali huyo anakumbuka maombi ya hivi karibuni ya amani na dhidi ya vita, ambapo Papa Francisko pia aliitaja Ethiopia. Katika hotuba yake ya Urbi et Orbi ya Siku Kuu ya Kuzaliwa kwa Bwana  2021, Baba Mtakatifu aliomba Bwana asaidie nchi kupata njia ya upatanisho na amani kwa njia ya mazungumzo ya wazi, ambayo yanaweka mahitaji ya watu mbele. Zaidi ya hayo, mnamo tarehe 27 Februari iliyopita, mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Papa Francisko alihimiza ulimwengu mzima kukumbuka vita vilivyosahaulika. Mbali na Ukraine, Papa Francisko aliomba kutosahau vita katika sehemu nyingine za dunia, kama vile Yemen, Siria na Ethiopia, na akasema “fungeni silaha zote! Mungu yu pamoja na wapatanishi, si pamoja na watendao vurugu”.

Vita vinahusu masuala ya kisiasa na kiuchumi

Kardinali Berhaneyesus Souraphiel, akijibu swali juu ya Papa Francisko kuzindua miito mingi dhidi ya vita na kuiombea chi yake na thamani gani kuhusu miito hiyo, amesema ina thamani kubwa! Kwa hakika, amesema walimshukuru Baba Mtakatifu kwa kuikumbuka Ethiopia pamoja na migogoro na vita vyake vya ndani. Wanashukuru sana kuwa na wasiwasi huo na maombi kwa ajili ya hali ya nchi yao. Kwa kirefu ameeleza kwamba hivi sasa, angalau, hakuna vita au mapigano kama ilivyokuwa miezi michache iliyopita. Kwa sasa ni afadhali kwa sababu wanaambiwa kwamba mazungumzo yanaendelea kati ya serikali ya shirikisho na serikali ya mkoa au mamlaka ya kisiasa, kwa sababu migogoro mingi inahusu masuala ya kisiasa na kiuchumi. Ni matumaini kuwa mazungumzo haya yanayoendelea yataleta amani ya kudumu. Hata hivyo, wakati wowote kunapotokea vita na migogoro, ni raia wanaoteseka zaidi. Watu wa kawaida wameteseka sana, hasa katika eneo la Tigray, lakini janga hilo pia limeenea nje ya Tigray, hadi mikoa mingine jirani kama eneo la Amhara na eneo la Afar. Watu bado wanateseka katika maeneo haya ya kuhama, njaa na uharibifu.

Miundo mbinu imeharibiwa

Miundombinu mingi imeharibiwa, ikiwemo shule, vituo vya afya na madaraja na kwa maana hiyo hivi vyote vinahitaji  kujengwa upya. Yeye ameomba katika baadhi ya maeneo ambapo watoto wanaombwa kwenda shule ili kuwazuia wasibaki nyumbani kila mara. Ingawa waliweza kurudi darasani, hata hivyo walikuta majengo yameharibiwa. Na kutokana na uhukosefu wa benchi wanakaa juu ya mawe au magogo ya mbao ili kufuatilia masomo. Kuwa pamoja ni muhimu sana kwa wanafunzi. Lakini mateso ya watu yanaendelea. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na taasisi nyingine nyingi, likiwemo Kanisa Katoliki kupitia Caritas, Waorthodox, Waislamu na Waprotestanti, wanajaribu kuokoa kwa kusafirisha chakula na dawa ikiwezekana. Kwa maama hiyo wanatumaini kuwa misaada haitakosekana ili kuzuia njaa kuwa balaa la kutisha.

Hali ya Tigray inazidi kuwa mbaya

Hali ya kibinadamu huko Tigray inazidi kuwa mbaya na mbaya zaidi, kwa sababu mikondo ya kibinadamu ambapo Umoja wa Mataifa au serikali au mashirika mengine yanajaribu kuleta chakula nchini wakati mwingine huzuiwa na hawajuhi na nani. Kwa sababu hiyo, mateso ya watu yanaongezeka. Walichofanya kama Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia ni kuzindua wito kwa njia ya mtandao wa Kikatoliki duniani kote, hasa kupitia Caritas Internationalis. Wiki mbili tu zilizopita waliomba fedha kusaidia watu hawa, sio tu wa Tigray, lakini hata katika mikoa ya jirani. Ukame pia umeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kifupi, wanalo janga kubwa la kibinadamu ambalo watu wanahitaji msaada.

Nchini Ethiopia inakaribisha hata wakimbizi wa nchi nyingine

Akijibu ni jinsi gani anaona wito wa Papa Francisko alio utoa wakati wa Pasaka wa kusitisha vita  vinavyoendelea nchini Ukraine, amesema wanasikitika sana kwamba vita vimezuka kati ya Urussi na Ukraine. Karibu miaka 75 baada ya Vita vya Pili Kidunia. Yeye mwenyewe alifikiri kwamba haitawahi kutokea vita tena huko Ulaya. Inawaumiza sana kuona mzozo wa Ukraine na mateso ya watu. Wanashutushwa kutokana na kusikia habari kwamba zaidi ya watu milioni 4 wameikimbia nchi yao. Wao wanajua maana ya kuwa wakimbizi, kwa sababu Ethiopia ni mojawapo ya nchi chache za Kiafrika zinazojali wakimbizi na kuokea wakimbizi. Wana takriban nusu milioni ya wakimbizi wa Kisomali, takriban wakimbizi 300,000 wa Eritrea na takriban wakimbizi 430,000 kutoka Sudan Kusini. Pia wanao wakimbizi wa Siria ambao wamefika Addis Ababa. Na hajuhi walifikaje nchini humo, lakini watu wanazunguka kila mahali.

Sauti ya Baba Mtakatifu pamoja na wakristo wote inahitajika

Kwa maana hiyo ni matarajio ya vita vya Ukraine havitazidi kwa sababu vita vinaharibu. Katika televisheni wanaona picha, si tu za Ukraine, bali pia za Iraq na Siria, Lebanon na Yemen. Baba Mtakatifu amekuwa akionya mara kwa mara kuhusu Vita vya Tatu vya Dunia, vilivyogawanyika vipande vipande, hapa na pale. Hili lazima lichukuliwe kwa uzito na kusimamishwa haraka iwezekanavyo. Ombi la Papa la kusitishwa kwa vita wakati wa salamu za Pasaka ni la sasa sana. Haihitajiki sauti tu ya Baba Mtakatifu, bali pia Wakristo wote, kwa sababu Urussi na Ukraine ni mataifa ya Kikristo. Hata huko Yemen sasa, kutokana na mfungo wa Ramadhani, Waislamu wameacha kupigana kwa muda wa mwezi mmoja. Hivyo “Ninaunga mkono kikamilifu ombi la Papa Francisko la usitishaji wa Vita katika kipindi hiki cha Pasaka".

20 April 2022, 17:02