Uwanja wa Mtakatifu Petro umeona maskauti Italia wakiombea nchi ya Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwitikio wa maskauti kwa mwaliko wa Papa Francisko wa kufunga na kusali siku ya Jumatano ya Majivu tarehe 2 Machi 2022 kwa ajili ya amani nchini Ukraine haukuchelewa kufika kwani usiku wa Jumatano vijana elfu moja waliovalia kaptura na kofia yaani mavazi yao rasimi, walikusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro saa 3.00 usiku kwa ajili ya mkesha ambao waliimba, walitafakari na kuomba kwa lugha ya Kiitaliano na Kiukreni. Sala ya jumuiya ambayo inakuwa kilio kikuu kuelekea mbinguni, kuomba kwa Mungu amani ambayo wanadamu peke yao hawawezi kuijenga, na kama Papa Francisko alivyoandika katika mahubiri yake kwa ajili ya Misa ya majivu, ambayo iliyosomwa na katibu wake Kardinali Petro Parolin katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu ndiyo ulikuwa wito na mada kuu kutoka katika Mahubiri ya ya Yesu kwenye Injili ya Mathayo, na ulioongoza moyo wa mkesha wa maskauti hao, wakati wa kutafakari ambapo wahisi hisia kali wakati maneno hayo yaliposikika katika lugha ya Kiukreni katika uwanja wa barafu. Lakini katika mawazo yaliyopendekezwa na waandaaji, pia ilikuwapo historia ya Kaini na Abeli kutoka katika kitabu cha Mwanzo, historia hiyo yenye mizizi ya uovu na ambayo mtu, aliyewekwa kuwa mlinzi wa ndugu yake, badala yake anakawa muuaji wake, akigundua vurugu na dhambi. Maneno ambayo yanafafanuliwa kwa maneno mengine, yale yaliyochukuliwa kutoka katika Waraka wa Papa Francisko wa Laudato si': katika kifungu kisemacho:“wakati mahusiano haya yote yanapopuuzwa, wakati haki haiishi tena duniani, Biblia inatuambia kwamba maisha yote yamo hatarini”.
Mwendelezo wa mkesha huo uliendelea taratibu kwa kusali Zaburi ya 31, kusoma kwa pamoja maombi ya Misa wakati wa vita, maneno ya nabii Isaya na sala ya ulimwengu kwa nia mbali mbali kuanzia kwa Makanisa yote ulimwenguni, kwa ajili ya wakimbizi, kwa ajili ya wahanga, walio dhaifu zaidi na walio hatarini ambao wanakimbia hofu, hadi wale ambao hawajaweza au walitaka kukimbia na hawawezi.
Na ilikuwa sasa jioni wakati mishumaa ilizimwa kwenye baridi na kwa faraja katika moyo wa kufanya maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II tena ili yasikike: “Kuombea amani kunamaanisha kuufungua moyo wa mwanadamu uliharibiwa na kwa nguvu ya kuufanya uwe mpya kwa uwezo wa Mungu”. Ulikuwa ni mpango rahisi, rahisi sana kama mtindo wa kiskauti ulivyo, lakini wakati huo huo kua jibu zito na la wazi, lenye nguvu kuliko mabomu, kwa sababu, kama Papa anavyo kumbusha mara nyingi, kuwa Bwana husikiliza maombi ya viumbe wake wote, hata walio na manyoya shingoni na kofia za kijani kibichi vichwani mwao, macho mekundu kwa sababu ya usingizi maana kesho wanatakiwa kwenda shule.