Shule: wanafunzi wakiwa katika Uwanja wa Napoli wakiandamana kusema kuwa huwezi kufa ukiwa masomoni. Shule: wanafunzi wakiwa katika Uwanja wa Napoli wakiandamana kusema kuwa huwezi kufa ukiwa masomoni. 

Siku ya Wafanyakazi Duniani 2022:kuna vifo vingi kazini&ukosefu wa ajira

Katika ujumbe wa Baraza la Maaskofu nchini Italia katika fursa ya Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi 2022 ,wanakumbusha jinsi ambavyo kuna vifo vingi kazini na hivyo sio rahisi kusahau wasio kuwa na ajira,na wengine ambao wamefikia hatua ya kujiua kwa sababu ya kukosa kazi.Janga la uviko na kuongezea sasa vita nchini Ukraine ni mambo yanayoleta wasi wasi mkubwa wa familia na jamii kwa ujumla.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika kuelekea kilele cha Siku Kuu ya Wafanyakazi duniani  Mesi Mosi, 2022, Baraza la Maaskofu Italia (CEI) wamechapisha ujume wao unaotoa nuru ya mantiki nyingi kuhusiana na hali halisi ya wafanyakazi katika jamii na kubainisha wasi wasi wao mkubwa. Katika ujumbe huo, Baraza la Maaskofu wanandika kuwa: “Tunapitia msimu mgumu, ambao bado una alama ya athari mbaya za janga na vita nchini Ukraine, ambayo kazi inaendelea kusumbua jamii ya  kiraia na familia na inajitoa katika kufanya mang’amuzi ambayo yanatafsiri mapendekezo ya mshikamano na ulinzi wa hali hatari zaidi. Matokeo ya mtikisiko wa kiuchumi yana uzito juu ya mabega ya vijana, wanawake, wasio na ajira, hatari, katika hali ambayo matatizo ya kimuundo yanaongezwa kwa kuzorota ubora wa kazi. Kanisa nchini Italia haliwezi kuondoa mtazamo wake katika mazingira ya hatari kubwa kwa afya na maisha yenyewe ambayo wafanyakazi wengi wanakumbana nayo. Vifo na vingi sana, kazini vinatukumbusha hili kila siku. Thamani ya mwanadamu inatiliwa shaka, mtaji pekee ambao ni utajiri wa kweli”. Maaskofu wanabainisha kwamba, “utajiri halisi ni watu: bila wao hakuna jumuiya ya kazi, hakuna biashara, hakuna uchumi. Kuwa na usalama mahali pa kazi maana yake ni utunzaji wa rasilimali watu, ambao ni wa thamani sana machoni pa Mungu na pia machoni pa mfanyabiashara wa kweli,” Papa Francisko alikumbuka alipokutana na Chama cha Kitaifa cha Wajenzi wa majengo (20 Januari, 2022). Mawazo ya Maaskofu yanawaendea hasa wale ambao wamepoteza maisha katika utimilifu wa taaluma ambayo ilikuwa dhamira yao ya kila siku, maonesho ya hadhi na ubunifu wao na pia kwa familia ambazo hazijawaona wakirudi nyumbani, kwa kazi yao, waliwasaidia kwa upendo. Kama jinsi ambavyo hawawezi kusahaulika wale wote ambao hawakuwa na kazi, na  ghafla wamekandamizwa na uzito usioweza kuvumilika, wamefikia hatua ya kujiua wenyewe, kwa maana hiyo maaskofu wanawahakikishia Sala zao, na tumaini lao kwa Bwana anayependa maisha na mshikamano wao ili uwe ishara ya jumuiya inayojua kulia na wale wanaolia (rej. Rum 8:15) na ya jamii inayojua kutunza, wale ambao, ghafla walinyimwa mapendo na usalama wa kiuchumi.

Upinzani wa wakati wa sasa

Nchi ambayo inataka kupanda kwa uchanya wake kutoka katika  mteremko wa mgogoro, wanasema haiwezi kuweka ukuaji wake wa kiuchumi juu ya sadaka ya kila siku ya maisha ya binadamu. Hali iliyopo mbele ni ya kushangaza kwa sababu mnamo 2021 kulikuwa na vifo 1,221 (kulingana na takwimu za Inail), pamoja na wale wasiojulikana" kwa sababu walitokea kwenye majareaha ya kazi haramu, yaani katika mazingira ya kichini chini ambayo majanga yasiyokubalika yanazidi kuongezeka. Kuna kukabiliana mbele ya muungu wa kisasa ambaye anaendelea kudai tozo lisilovumilika la machozi. Miongoni mwa sekta zilizoathirika zaidi ni viwanda, huduma, ujenzi na kilimo. Kila tukio linalotokea ni kushindwa kwa jamii kwa ujumla, kila ajali mbaya huashiria majeraha makubwa kwa wale wanaopatwa na athari za moja kwa moja, kama vile familia na wafanyakazi wenza na kwa maoni ya umma. Hakuna vifo tu bali majeraha ya hali tofauti yanahitaji uangalifu wa kutosha, kama vile magonjwa kazini yanavyohitaji ulinzi wa afya na usalama. Kunahitajika dharura za haraka zinazopaswa kutekelezwa, kwa kuzingatia nyanja mbalimbali. Maaskofu wa Italia katika ujumbe huo wanabainisha jinsi ambavyo dhamiri nzima ya kijamii inaulizwa pia na wale ambao wanajishughulisha na kazi zisizo za kawaida au zinazofanywa katika hali zisizo na heshima, kwa sababu ya unyonyaji, ubaguzi, uajiri haramu, ukosefu wa haki, ukosefu wa usawa.

Kilio cha maskini wapya kinaongezeka

Kilio cha maskini hawa wapya kinaongezeka kutokana na hali pana ya ubinadamu ambapo kuna vurugu za kiuchumi, kisaikolojia na kimwili ambapo waathirika zaidi ya wahamiaji wote, ni wafanyakazi wasioonekana na wasio na ulinzi, na wanawake, mateka wa mfumo unaokatisha uzazi na huadhibu mimba na kutotungwa. Kuhamasisha wanawake katika nyanja ya kitaaluma bado haitoshi.  Kielelezo cha Armida Barelli, aliyetangazwa mwenyeheri mnamo tarehe 30 Aprili huko Milan, pia ni himizo la umakini wa kuzingatia, kwa maana alihamasisha mipango mingi ya kuimarisha wanawake. Katika hali hizi zote, si tu kwamba kazi si huru, wala si ubunifu, shirikishi na msaada (rej. Evangelii gaudium 192), bali mtu anaishi katika hatari ya mara kwa mara ya kuona afya yake ikidhoofishwa na uhai wake ukiwa hatarini. Soko la ajira pia lina mapungufu makubwa ambayo ni miongoni mwa sababu za kile kinachoitwa “vifo vyeupe”. Kuongezeka kwa hatari kunalazimisha wafanyakazi wengi kubadilisha kazi mara kwa mara, miktadha ya kazi na taratibu, na kuwaweka kwenye hatari kubwa zaidi. Zaidi ya hayo, kazi hatari zaidi mara nyingi hukabidhiwa kwa vyama vya ushirika vya huduma, vilivyo na malipo duni, wafanyakazi wenye mafunzo duni, walioajiriwa na mikataba ya muda mfupi, kulazimishwa kufanya kazi kwa mtindo mbaya na mizigo mizito isiyofaa, katika mchanganyiko wa uharibifu unaoongeza hatari ya makosa mabaya.

Majukumu ya pamoja kwa ajili ya huduma ya afya ya mfanyakazi

Baraza la Maaskofu wakiendelea na ujumbe huu, wanauliza swali “je ni mali gani ziko hatarini katika hali hizi?  Kwa kujibu  wanabainisha kwamba “awali ya yote thamani ya kibinafsi na binafsi kazini, ambayo hufafanuliwa kama mtaji wa kibinadamu, ambao ni kusema watu wenyewe, wenye uwezo wa kufanya kazi, wa ujuzi, wa ubunifu, wa utambuzi wa mahitaji ya wenzao, wa kuelewana kama washiriki wa shirika (Compendium of the Social Doctrine of the Church, 276). Lakini pia ukamilishano kati ya kazi na mtaji, ambayo inashinda mitindo ya zamani kupitia mifumo ya kiuchumi yenye uso wa mwanadamu, ili rasilimali kuu ibaki kuwa mtu mwenyewe. Wema wa amani pia uko hatarini, kwa sababu wakati masharti ya kazi salama na yenye heshima yanapowekwa, misingi inawekwa ili kuepuka aina yoyote ya migogoro ya kijamii (rej. Papa Francisko: Ujumbe wa Siku ya 55 wa Amani ya Dunia). “Kutokana na thamani hizi muhimu huchipua utamaduni wa kujali, unaostawishwa na Neno la Mungu, linalotualika kufungua mioyo yetu kwa wale wanaoona hadhi yao na maisha yao yakiwa hatarini katika kazi zao. Je, tunawezaje kushindwa kukumbuka mateso ya watu wa Israeli waliokuwa watumwa huko Misri, wakilazimishwa kutengeneza matofali kwa wingi zaidi na kwa muda mfupi zaidi (taz. Kut 1:13-14a)? Uchaguzi usio na huruma unaowaweka watu chini ya mantiki ya idadi pia upo katika barua ya Yakobo, ambayo inakumbusha jinsi maandamano ya wavunaji yalivyofikia masikio ya Bwana Mwenyezi (taz. Yak 5:4).”

Serikali zitekeleza udhibiti makini zaidi unaokuwa kichocheo cha kuzuia ajali

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha kazi sahihi ya  kuelimisha na kulinda wanyonge katika ulimwengu wa kazi, ambayo inashirikisha jumuiya ya kiraia na jumuiya ya Kikristo: “Leo ni lazima tujiulize ni nini tunaweza kufanya ili kurejesha thamani ya kazi; na ni mchango gani, kama Kanisa, tunaweza kutoa ili kukombolewa kutoka mantiki ya faida tu na kuweza kuishi kama haki msingi na wajibu wa mtu, ambaye anaelezea na kuongeza hadhi yake (Katekesi tarehe 12 Januari 2022). Ugumu wa sababu na matukio unahitaji mbinu ufungamani kwa wale wote wanaohusika na uingiliaji wa mfumo lazima ufanyike katika ngazi ya serikali na katika ngazi ya kampuni". Ni muhimu kuwekeza katika utafiti na teknolojia mpya, katika mafunzo ya wafanyakazi na waajiri, lakini pia kujumuisha nidhamu inayohusiana na afya na usalama kazini katika programu za shule na mafunzo ya ufundi stadi. Ni muhimu kwa Serikali kutekeleza udhibiti makini zaidi, ambao unakuwa kichocheo cha kuzuia ajali. Jukumu madhubuti katika kulinda usalama wa mfanyakazi na hali yake ya kiafya inahakikishwa na njia za shirika la kampuni katika suala la kupitishwa kwa hatua za ulinzi na usimamizi ili ziheshimiwe. Kuhusiana na hilo ndipo wito wa Papa Francisko kwa wajasiriamali unasikika unafaa kuliko hapo zamanai kuwa:  "Mna wito adhimu unaolenga kuzalisha mali na kuboresha ulimwengu kwa ajili ya wote; kwa hiyo mnaitwa kuwa wajenzi wa manufaa ya wote na mafundi wa ubinadamu wa kazi mpya. Mmeitwa kulinda taaluma na wakati huo huo kuzingatia hali ambayo kazi hufanyika, ili ajali na hali za shida zisitokee" (Hotuba kwa wajasiriamali, 27 Februari 2016).

Ikiwa mhusika wa kuzuia ni kila mmoja inawezekana kurudisha hadhi na kazi

Vyama vya wafanyakazi, katika utafutaji wao endelevu wa haki ya kijamii, hufuatilia kila mara hali za usalama mahali pa kazi kwa maana hiyo Maaskofu nchini Italia wanawatia moyo wa  kuwa na jitihada ya kulinda hasa zile fani ambazo zimevaliwa zaidi kwa afya au hatari zaidi. Kufuatia kile ambacho Kanisa nchini Italia limefanya katika maadhimisho ya Juma la Kijamii huko Taranto (mwezi Oktoba 2021) ni muhimu kuhimiza ushirikishi wa matendo mema ambayo katika nyanja za biashara na utawala yanaonesha jinsi ya kuchanganya sio tu ulinzi wa mazingira na ulinzi wa kazi, lakini pia hadhi na usalama, hivyo kuepuka hali zinazo hatarisha afya au hata kusababisha kifo. Ikiwa tu kila mhusika wa kuzuia, kwa njia tofauti kuanzia taasisi na washirika wa kijamii, anachangia katika mapambano dhidi ya ajali, kutakuwa na mabadiliko ya kweli. Kwa hili ni muhimu kuamsha dhamiri. Shukrani kwa dhana ya uwajibikaji wa pamoja, inawezekana kweli kutekeleza mabadiliko hayo yenye uwezo wa kumrudisha mtu katikati ya kazi, katika kila muktadha wa uzalishaji, wamehimitimisha ujumbe wao maaskofu wa Italia

29 March 2022, 12:21