Tanzania: Siasa Safi ni Huduma ya Ujenzi wa Amani ya Kudumu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu inayoadhimishwa tarehe Mosi Januari anasema: “Siasa safi ni huduma ya amani”. Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza”. Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Matumizi ya nguvu ni kinyume cha kanuni maadili inayopania suluhu ya amani na utulivu. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni mbinu mkakati wa kujijenga kisiasa kwa kuwashutumu wakimbizi na wahamiaji kuwa ni sababu ya umaskini na majanga yanayowaandama watu wao. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni ushuhuda wa urithi wa utajiri wa kimaadili kizazi baada ya kizazi!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Ijumaa tarehe 4 Machi 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe, muda mfupi tu baada ya kuachiwa huru. Rais Samia amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kushirikiana ili kuijenga Tanzania kwa kuaminiana na kuheshimiana kwa misingi ya haki. Mhe. Mbowe amemshukuru Rais Samia kwa kuonesha kwake kujali huku akikubali kuwa msingi mkubwa wa kujenga taifa la Tanzania ni kusimama katika haki. Vile vile, amesema wamekubaliana kufanya siasa za kistaarabu na za kiungwana na kuwa yuko tayari kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ili nao pia waweze kutekeleza majukumu yao ipaswavyo. Watanzania na wapenda amani sehemu mbalimbali za dunia, wamelipokea tukio hili kwa imani na matumaini ya ujenzi na uimarishaji wa demokrasia shirikishi nchini Tanzania kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.