Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Mambo msingi: Toba, Wongofu wa ndani na uaminifu kwa Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Mambo msingi: Toba, Wongofu wa ndani na uaminifu kwa Mungu. 

Dominika ya III ya Kwaresima Mwaka C: Toba, Wongofu Na Uaminifu

Leo tunatafakari Bwana Mungu ambaye anatuweka huru kutoka utumwa wetu wa dhambi, ikiwa tu tutasikiliza na kuzingatia onyo lake la kutubu. Kwa hivyo, wazo letu kuu leo ni toba, wongofu wa ndani kama ushuhuda wa kuthamini huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mungu anatoa nafasi kwa waja wake kuboresha maisha na mahusiano yao kila kukicha! Anza sasa!

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Katika Dominika hii ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Kanisa linatupatia wakati mwingine wa neema ya kutunyoosha katika safari yetu. Leo tunatafakari Bwana Mungu  ambaye anatuweka huru kutoka utumwa wetu wa dhambi, ikiwa tu tutasikiliza na kuzingatia onyo lake la kutubu. Kwa hivyo, wazo letu kuu leo ​​ni toba. Mpendwa msikilizaji, Kitabu cha Kutoka ambako tunapata somo la kwanza leo, kinatusimulia kukutana kwa Musa na Mungu aliye hai. Kama sehemu ya mpango Wake wa wokovu, Mungu alimwita kiongozi na mpatanishi wa watu wake—Musa—ambaye alipeleka ujumbe wa Mungu kwa Waisraeli na kuwaongoza watu wake kutoka katika utumwa wao huko Misri. Kukutana kwa Musa na Mungu kwenye kichaka kilichowaka moto ulikuwa wakati muhimu katika historia ya wokovu. Ingawa Musa mwanzoni alikataa akitoa sababu zake, baadaye alikubali mapenzi ya Mungu na jukumu la kuwaongoza watu wake kutoka Misri. Huyu ni Mungu anayetutafuta, Mungu anayejidhihirisha, Mungu anayetaka tuishi kwa ajili yake na Mungu ambaye ni mwaminifu daima katika uhusiano wake nasi, hata pale tunapokutana na mambo magumu. Wakati fulani hatutaki kubadilisha maisha yetu, kutubu, na daima tunahitaji kukumbushwa. Basi kipindi hiki tunakumbushwa tena kufanya toba.

Toba ni chemchemi ya huruma, msamaha na wokovu
Toba ni chemchemi ya huruma, msamaha na wokovu

Mpendwa msikilizaji, somo la pili toka Barua ya Kwanza kwa Wakorintho inafunua masimulizi yaliyofupishwa, ya tahadhari kutoka katika kitabu cha  Kutoka. Baada ya kukombolewa kutoka utumwani Misri, Waisraeli walikaa miaka arobaini jangwani kabla ya kuingia katika Nchi ya Ahadi. Wakati huo, walikiuka Agano la Mungu kupitia ibada ya sanamu na mashaka dhidi ya usimamizi wa Mungu. Hata hivyo, Mungu aliendelea kuwa mwaminifu kwao walipokosa uaminifu kwake. Mtakatifu Paulo anatutaka tubaki waaminifu, tusiwe wazembe na wakaidi kwa Mungu. Wakati wowote hatupaswi kuchukulia upendo wa Mungu na fadhila kuwa kirahisi, kana kwamba tumeshinda wokovu na thawabu zake zote na hatuna tena kazi yoyote ya kufanya. La! Badala yake, ni lazima tujitahidi kila siku kuishi kwa uaminifu Sheria ya Mungu huku tukitumaini kwamba Mungu anatupenda. Haijalishi ni hali gani, ni lazima tuwe na hakika ya upendo na utunzaji wake kwetu. Injili tuliyoisikia kadri ilivyoandikwa na Mtakatifu Luka inarekodi maneno yenye nguvu kutoka kwa Yesu; ni maneno yanayoakisi mapokeo ya Agano la Kale. Mungu anatupenda sana na anataka nasi tumpende. Anataka tuache dhambi na kumgeukia. Licha ya maelezo mengine yaliyotangulia juu ya toba, Yesu anatoa juu ya Mfano wa Mtini ambao ulikuwa hauzai kabisa, unahusu toba na rehema. Mungu, kwa huruma yake, anatupa nafasi ya kutosha ya kutubu na kuzaa matunda. Hata hivyo, tukidumu katika kukataa upendo wake, hakika tutaangamia kwa chaguo letu wenyewe. Mungu hafurahii roho zilizopotea. Mungu anataka kurudisha mioyo yetu wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima.

Mpendwa msikilizaji, masomo yetu yanalenga juu ya toba, watu kutubu, kumrudia Mungu. Kuachana na dhambi na hivyo wanapokosa kurudi kujipatanisha na Mungu kwa kupokea sakramenti ya Kitubio. Katika injili ya leo, Yesu alisema moja kwa moja katika maneno yake aliposema: “Nanyi msipotubu mtaangamia.” Mtu anaweza kusema kwamba hii ni kali sana kutoka kwa Kristo ambaye ni mwenye huruma. Ukweli ni kwamba Yesu anaposema hivi, haipunguzi huruma na rehema yake. Badala yake, anafanya hivyo kwa sababu anatujali sana na huona tusichoweza kuona. Anatuonya ili kuondokana na matokeo mabaya ya kuishi maisha ya dhambi na anataka tutubu na kuishi maisha ya neema. Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Habari Njema ni kwamba, tunapewa fursa ya kujifunza kutokana na kushindwa kwa Mababu zetu na matokeo ya matendo yao. Tunapewa nafasi nyingine ya kumwita Bwana ambaye ni “mwenye rehema, huruma na upendo.” Yesu anataka tuchukue hatua ya ujasiri na chanya kurekebisha njia yetu ya maisha.

Toba ni kielelezo cha msamaha na uponyaji.
Toba ni kielelezo cha msamaha na uponyaji.

Huu ni mwito wa kutubu kwa nyakati tulizopuuza na kushindwa kumpenda Mungu na jirani zetu; kwa nyakati tulizochagua uovu badala ya wema; na kwa nyakati hizo tulikata tamaa na kuonyesha ukosefu wa ajabu wa imani katika Mungu. Baba mvumilivu, mwenye huruma na upendo yuko tayari kutukaribisha tena. Kwa hiyo, kipindi hiki cha Kwaresima, anatuambia: “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitawasamehe dhambi zao, na kuiponya nchi yao.” (2 Nya 7, 14). Toba huleta rehema, huruma, msamaha na wokovu. Inaleta uponyaji na urejesho wa tumaini la maisha bora ya sasa na kwa siku za baadaye. Kwa hiyo, tukitubu dhambi zetu kwa dhati, Mungu hatatusamehe tu, bali atatuponya. Tuombe Mungu msamaha kwa dhambi zetu, tuombee pia amani Ukraine na sehemu nyingine ambako watu wanateseka sababu ya vita.

Padre Msigala E D3
18 March 2022, 14:49