CELAM:kujenga amani ndiyo wito wa siku ya sala na kufunga
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Maaskofu wa Amerika Kusini (Celam), katika ujumbe wao kwa mwanzo wa Kwaresima 2022, uliosomwa kwa njia ya video na Rais wake, Askofu Mkuu Miguel Cabrejos, wa Jimbo Kuu katoliki la Trujillo (Peru), amezindua kwa upya wito wa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, yanayoongoza Ujumbe wake wa Karesima yaliyotolewa katika Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia kuwa: “Tusichoke kutenda mema na tutende mema kwa wote”. Kwa maana hiyo, amesema: “katika kipindi cha Kwaresima kinawaalika kutenda mema na kujenga amani, tukifuata mfano wa Mtakatifu Fransisko wa Asisi ambaye kwa salamu ya ‘Amani na salama” alitanguliza kuonesha ulimwengu wote wito wa mwanadamu kuwa kaka na dada”. Askofu mkuu Cabrejos na ambaye ni mransiskani alieleza kwamba, “Kwaresima inatualika katika wongofu, kubadili fikra zetu, ili ukweli na uzuri wa maisha yetu usikae sana katika kumiliki bali katika kutoa, na si katika kujilimbikiza, bali katika kupanda mema na kushirikishana”.
Kwa upande mwingine, maaskofu wa Amerika Kusini (Celam) wamesisitiza na kurudia kutoa mwaliko kwa watu wote wa Mungu katika bara la Amerika ya Kusini na visiwa vya Caribbean kushiriki katika siku ya kufunga na kuomba kwa ajili ya amani, iliyoitishwa na Papa kwa siku ya Jumatano hii ya Majivu, na tangu uvamizi wa Ukraine na Urusi ambao bado unaendelea ni ujumbe ulio hai. Kwa maana hiyo, wito ni kuunganisha nia ya Baba Mtakatifu na ya wanadamu katika kilio chao cha amani na kukomesha vurugu nchini Ukraine. Rais wa Celam amehitimisha: akisema kwamba kwa siku 40 zinzotarisha kufikia siku kuu tatu kabla ya Pasaka yaani Mateso, kufa na kufufuka kwa Bwana, waendelee kujiimarisha dhamira zao wote kwa watu maskini na walio hatarini zaidi katika jamii yao, kwa kutoa nafasi kwa ustaarabu wa upendo zaidi.