Tafuta

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania, anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali ili kuombea amani duniani. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania, anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali ili kuombea amani duniani. 

Askofu Mkuu Ruzoka Anawaalika Waamini Kusali Ili Kuombea Amani Duniani

Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania, anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Papa Francisko za kutafuta amani na utulivu nchini Ukraine, ili jitihada za kidiplomasia ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani haki, amani, ustawi na mafao ya wengi.

Na Ndahani Lugunya, Dodoma na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kulinda na kuthamini: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 55 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2022 yananogeshwa na kauli mbiu “Elimu, Kazi Na Majadiliano Kati ya Vizazi: Chombo cha Ujenzi wa Amani ya Kudumu.” Mtakatifu Paulo VI anasema kwamba, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni wakati wa kusikilikiza na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ujenzi wa amani ya kudumu unajikita katika: Majadiliano kati ya vizazi, Elimu pamoja na Ajira. Amani ni muhtasari wa ustawi, maendeleo na mafao ya binadamu wote katika ujumla wao na inapata chimbuko lake katika toba na wongofu wa ndani.

Vita kati ya Urussi na Ukraine vinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Vita hii ina madhara si tu kwa Urussi ambayo imewekewa vikwazo vya kiuchumi na hivyo kusababisha kupanda kwa gharama ya maisha wakati hali ya maisha, ikiendelea kuporomoka sana na hivyo watu wengi kuanza kutumbukia polepole katika umaskini wa hali na kipato. Lakini madhara yake pia yamejionesha kwa kiasi kikubwa nchini Ukraine, kwa watu kupoteza maisha, kukimbia makazi yao pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Uvamizi wa Urussi kijeshi nchini Ukraine unaendelea kuhatarisha usalama, ustawi na mafungamano ya Kimataifa si tu kwa Bara la Ulaya, bali makali yake yameanza kusikika sehemu mbalimbali za dunia kutokana na kupanda kwa gharama ya nishati ya mafuta na gesi. Uhaba wa ngano pamoja na kuporomoka kwa biashara kati ya Urussi na nchi mbalimbali duniani na hivyo kupelekea mfumuko wa bei ya mazao ya chakula na nishati. Kwa ufupi kabisa, uvamizi wa Urussi nchini Ukraine unaendelea kuvuruga uchumi duniani, mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kukwamisha jitihada za maendeleo ya teknolojia rafiki kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Diplomasia katika ukweli itasaidia kuokoa maisha ya watu.
Diplomasia katika ukweli itasaidia kuokoa maisha ya watu.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora nchini Tanzania, anaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu Francisko za kutafuta amani na utulivu nchini Ukraine, ili jitihada za kidiplomasia ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Kipindi hiki cha Kwaresima, iwe ni fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu kwa kufunga, kusali, kutafakari na kujibidiisha zaidi katika maisha ya Kisakramenti. Vita kati ya Urussi na Ukraine vinahatarisha amani ndani na nje ya Bara la Ulaya kama ilivyokuwa wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kunako mwaka 1914 kwa kugombania makoloni, Bara la Afrika likajikuta linaathirika vibaya sana. Kwa bahati mbaya Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kujifunza kutoka katika historia kama ilivyojitokeza kunako mwaka 1963, dunia ilipojikuta katika hali tete ya kutaka kuzuka kwa vita vya nyuklia kwa Urussi kutaka kuitetea nchi ya Cuba.

Leo hii nchi za Marekani na Ulaya zinataka kuitetea Ukraine, historia inayojirudia hatari kwa usalama na amani duniani. Majadiliano ya kidiplomasia yasipofikiwa na vita kusitishwa kuna hatari ya kuzuka Vita Kuu ya Tatu ya Dunia ambayo itakuwa na madhara makubwa sana kuliko vita nyingine yoyote iliyokwisha kutokea duniani. Ni katika hali na mazingira haya Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani. Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, anawaalika waamini wasichoke kusali, ili dunia iweze kuwa salama na mwanadamu aendelee kumtukuza Mwenyezi Mungu Muumbaji na Mkombozi!

Vita Ukraine
09 March 2022, 15:03