Maaskofu nchini Canada waanzisha Mfuko wa Upatanisho kwa ajili ya watu Asilia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kufuatia ahadi yao ya kifedha ya dola milioni 30 ya kusaidia uponyaji na upatanisho kwa waathirika na familia zao, na jumuiya za watu Asilia, Maaskofu wa Canada wametangaza kuanzishwa kwa Mfuko wa Upatanisho kwa ajili ya watu Asilia ambao utapokea michango iliyotolewa kwa madhumuni hayo na majimbo yote 73 nchini kote. Mfuko huo utasimamiwa na shirika jipya la Upendo lililosajiliwa, na ambalo litakalojumuisha wanachama Wazawa, ili kuhakikisha uwazi na usimamizi bora. Inatarajiwa kuchapisha ripoti za kila mwaka na itafanyiwa ukaguzi na kampuni huru ya uhasibu kila mwaka.
Jitihada za uoneshaji wa maumivu ya kihistoria
Maaskofu wa Canada wamejitolea kikamilifu kushughulikia maumivu ya kihistoria na yanayoendelea yaliyosababishwa na mfumo wa shule za bweni alisema Askofu Raymond Poisson, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Canada (CCCB). Katika kusonga mbele na dhamira yao ya pamoja ya kifedha, wataendelea kuongozwa na uzoefu na hekima ya watu wa kiasilia nchini kote. Kulingana na taarifa ya Baraza la Maaskofu nchini Canada CCCB, fedha zinazokusanywa zimekusudiwa hasa kwa ajili ya uponyaji na upatanisho kwa jamii na familia; kuhuisha utamaduni na lugha; elimu na ujenzi wa jumuiya; na midahalo ya kuhamasisha hali ya kiroho na utamaduni asilia. Washirika wa kiasilia au Kamati za Ruzuku za Mikoa na/au Majimbo zitaanzishwa ili kutambua miradi inayoendeleza vipaumbele vya hazina, kupitia maombi, na kuomba fedha za kusaidia miradi hiyo. Kamati hizi zitajumuisha washiriki wa watu asilia na Wakatoliki na Maaskofu wanapendekeza ziongozwe na washirika watu mahalia.
Shule za bweni zilitatizo watoto wengi karne ya 19 na 20
Shule za bweni za lazima zilifadhiliwa na serikali ya Canada na ziliendeshwa na taasisi za Kanisa wakati wa karne ya 19 na 20 kwa lengo la kuingiza vijana wa kiasilia katika utamaduni wa Ulaya na Canada. Hata hivyo, shule zilitatiza maisha na jamii na watoto wengi waliteseka na kutelekezwa na kudhulumiwa na kusababisha matatizo ya muda mrefu miongoni mwa watu wa kiasilia. Kwa jumla, watoto wapatao 150,000 wa First Nation, Inuit, na Métis walilazimika kuhudhuria shule hizi kati ya miaka ya 1870 na 1997. Tangu shule ya mwisho kufungwa, wanafunzi wa zamani wamedai kutambuliwa na kulipwa fidia, na hivyo kusababisha Makubaliano ya Makazi ya Shule za India mwaka wa 2007 na msamaha rasmi wa umma na Waziri Mkuu Stephen Harper mwaka wa 2008.
Uchunguzi wa miaka saba wa Tume ya ukweli na Maridhiano ya Canada
Uchunguzi wa miaka saba wa Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Canada (TRC) ulihitimisha mwaka wa 2015 kwamba zaidi ya watoto 4,000 walikufa walipokuwa wakisoma shule hizo, wengi kutokana na dhuluma, uzembe, au magonjwa. Kugunduliwa kwa mamia ya mabaki na makaburi yasiyo na alama kwa misingi ya shule tatu za zamani za makazi zinazoendeshwa na Wakatoliki wakati wa kiangazi cha 2021 kulivuta hisia mpya za umma kwa janga hilo, na mnamo Septemba Maaskofu walitoa taarifa rasmi ya kuomba msamaha na kuahidi dola milioni 30 za kimarekani kusaidia mchakato wa uponyaji na upatanisho.
Mkutano na Papa uliahirishwa Desemba 2021
Baba Mtakatifu Francisko naye aliuungana na Maaskofu katika kueleza ukaribu wao kwa wahanga. Ujumbe wa watu wa asilia ulitarajiwa kukutana na Papa huko Vatican mnamo Desemba 2021, lakini ziara hiyo iliahirishwa kwa sababu ya UVIKO-19. Katika taarifa yao wiki iliyopita, Maaskofu wa Canada walitambua mapungufu ya kampeni ya awali ya uchangishaji fedha wa Kikatoliki iliyofungamana na Makazi ya Shule ya Makazi ya Wahindi ya mwaka 2007 na kuahidi kwamba Mfuko mpya wa Maridhiano ya Watu asilia utasimamiwa vyema, kwa usimamizi ufaao.