Tafuta

Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu Severine Niwemugizi awekwe wakfu ni kipindi cha: furaha, shukrani, toba, msamaha na kuomba tena neema ya kusonga mbele. Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu Severine Niwemugizi awekwe wakfu ni kipindi cha: furaha, shukrani, toba, msamaha na kuomba tena neema ya kusonga mbele. 

Askofu Severine Niwemugizi: Jubilei ya Miaka 25 na Mchango Wake Kwa Watanzania

Askofu Msaidizi Methodius Kilaini katika mahubiri ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara awekwe wakfu ni kipindi cha furaha na shangwe; toba na wongofu wa ndani tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini. Anapembua miaka 25 ya Askofu Niwe, katika ustawi, maendeleo na mafao kwa watanzania.

Na Padre Agapito Mhando, -Vatican.

Kwa kuwa ni Jubilei utakuwa ni Mwaka Mtakatifu kwenu, hayo ni maneno kutoka katika kitabu cha Mambo ya Walawi yakiongelea Mwaka Mtakatifu, Mwaka wa Jubilei. Jubilei kwa Wayahudi ilikua ikiadhimishwa kila baada ya miaka Saba, na walifanya saba mara Saba jumlisha Mwaka mmoja miaka Hamsini na inakua Jubilei Kuu. Na kutoka Mwaka 1300 B.k, Mama Kanisa akaona miaka Hamsini ni mingi mno hasa kwetu Sisi basi ikawekwa kuwa kila baada ya miaka Ishirini na mitano Kanisa linafanya Jubilei. Mwaka wa Jubilei ni Mwaka wa kufanya toba, ni Mwaka wa kusamehe, ni Mwaka wa kupatanishwa na wale ambao tumefarakana nao, ni Mwaka wa kuongoka, ni Mwaka wa kutenda mema na kusamehe madeni yote yaliyokuwa nyuma. Wakati wa Jubilei ni wakati wa kuwa na furaha kwa watu wote. Jubilei ni neno la Kilatini «Iubilaeum» linalomaanisha furaha na shangwe kuu. Jubilei ni wakati wa Furaha, ni wakati wa kumshukuru Mungu na kuwashukuru wale wote ambao wametuwezesha kufikia hatua ya maadhimisho haya. Nasi sote leo tumekuja hapa Ngara kutoka sehemu mbalimbali, kufurahi, kusherehekea na kuserebuka tukiwa tunaadhimisha miaka 25 tangu Askofu Severine Niwemuzi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, ili kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba, tarehe 22 Februari 2022 katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu Askofu Niwemugizi alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Sote tupo hapa kusema asante kwa Mungu ambaye amekuwezesha na kukufikisha hapa na ambaye amekupa nguvu kwa kutekeleza kazi zote zile ambazo umeshazifanya. Tumekuja hapa kusema asante kwenu ninyi nyote kwa namna ya pekee Wana Rulenge-Ngara, kwa waamini wote na watu wote wenye mapenzi mema, Mababa Askofu, Mapadre kwa kumsaidia Askofu na kuweza kutembea pamoja naye kwa miaka hii 25 Niwemugizi ni jina linalojenga kweli. Niwemugizi maana yake Ni Mwenyezi Mungu anawezesha, anatenda, anatoa na kuokoa. Mungu amekuwezesha kwa muda huu wa miaka 25 nasi hatuna budi kusema Mungu asante na asante kwako ambaye umeitikia kutekeleza huu wito kwa nguvu na uwezo wako wote. Watu wote hawa wamekuja kutoka mpakani mwa Zambia, Nyasa, Msumbiji, Rwanda na Burundi na DRC ili kuja kuadhimisha Sikukuu yako, kwa sababu tunapenda na kuthamini kazi za kitume na kichungaji ulizozitenda kwa miaka 25 na tunamwomba Mungu aendelee kukulinda, kukubariki na kukuongoza katika maisha na utume wako.

Askofu Niwe katika miaka 25 amechangia ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.
Askofu Niwe katika miaka 25 amechangia ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.

Baba Niwemugizi umekuwa kuhani wa Jimbo la Rulenge na na baadae Jimbo la Rulenge-Ngara kwa miaka 25, Mtakatifu Petro anatuasa kama ilivyosomwa katika Somo la Pili: (1Pet. 5:1-4) nawasihi wazee walio kwenu Mimi niliye Mzee mwenzenu na Shahidi wa Kristo na mshirika wa utukufu...lichungeni kundi... sio kwa kulazimishwa... Mtaipokea ile taji. Hii ndiyo kauli ya Somo ulilo lichagua kwa sababu ndiyo kauli ambayo umeishika na kuitekeleza kikamilifu katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tunajiuliza kwani Kuhani mkuu ni nani? Tunasoma katika Waraka kwa Waebrania kuwa, Kuhani ni mtu aliyeitwa na Mungu kutoka miongoni mwa watu ili awatumikie watu katika mambo yamhusuyo Mungu hasa kwa kutolea sadaka na dhabihu kwa ajili ya kuwaondolea watu dhambi zao. Hivyo Baba Niwemugizi, Mungu amekuita na amekuteua kutoka kwa watu ili uweze kuwatumikia watu hawa kwa mambo yamhusuyo Mungu na kutolea sadaka kwa Mungu. Hivyo kwako Baba Niwemugizi mzaburi anasema, Bwana ameapa wala hata ghairi kwamba wewe ni Kuhani milele kwa mfano wa Melkisedeki.

Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, anasema amekutana na Baba Niwemugizi katika vipindi vinne tofauti tofauti katika maisha. Mara ya kwanza nimekutana naye alipokuwa amemaliza shule ya Sekondari Nyakato wakati huo akiwa kijana kabisa, nikakaa naye pale Bunena kidogo nikawa Bosi wake. Alikua kijana mwema, mnyoofu na msikivu na alikua akitenda kazi bila kuchoka, alinishangaza kwani alikua na vijana wenzake wawili walikua wanatoka na kufanya matembezi na mara nyingine walikua wakipata na kupiga “ile kitu”, lakini yeye alikua akibaki ndani akisoma na kusali. Likanijia swali huyu kijana ni wa namna gani? Hivyo nilikuja kufurahi kwa neema ya Mwenyezi Mungu amekua Padre. Alikua na uamuzi huo toka zamani lakini akaukamilisha na akaamua kuwa Padre. Na Mie nikawa mwalimu wake. Nilikua mwalimu wake pale Seminari kuu ya Falsafa ya Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba msimamo wake ukawa ni huo huo kwamba ni kijana mwenye akili mwenye msimamo na mwenye utashi katika maamuzi yake.

Lakini dunia hii mviringo, nikakutana naye mara ya tatu tukiwa sote Wanafunzi Roma, tukawa “ngoma droo” tukijifunza na kuhenya pamoja. Yeye akifanya shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa na Mimi nikifanya shahada ya Uzamivu ya historia ya Kanisa. Tulikaa vizuri Roma nikawa Mwenyekiti wake lakini baadae naye akawa Mwenyekiti wangu nakumbuka alikua anafanya mipango ya kuweza kukutana na Baba Mtakatifu lakini yapo mambo mengi mazuri na makubwa aliyoyafanya. Nilikutana naye mara ya Nne mara hii alikua bosi wangu kipindi alipokua Askofu nami nikiwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC naye akiwa Rais wa Baraza. Lakini mara zote hizi amekuwa ni Severini yule yule mpenda watu, mpenda Mungu na Mchamungu. Haya ndiyo tunayokuja kuyaadhimishia leo, mchungaji asiyekuwa na woga, ambaye hajali athari zinazoweza kumpata, anayesimamia haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hata kama wengine wanasita anabaki kila mara na kuwa na sauti ile ile ya kufanya kazi yake Mungu akifuata kauli mbiu yake ya kiaskofu "Hekima ya Mungu iniongoze".

Na kila mara ana ongozwa na hekima ya Mungu akisema “Nina yaweza yote katika yeye anitiaye nguvu”. Hilo amekuwa nalo na ndilo jambo ambalo amekua akilifanyia kazi kila wakati hadi mwisho aliamini kama alivyosema Kristo Yesu “Mimi nitaendelea kusema na kama sisemi hata na mawe yatapiga kelele.” Hivyo yeye ameendelea kuwa mstari wa mbele na kuamini kama Mtakatifu Paulo kuwa kama Mungu akiwa upande wetu nani awezaye kuwa kinyume chetu, kama Mungu yupo pamoja nami nani anaweza kuwa kinyume na Mimi? Je, ni kitu gani kinaweza kunikatisha tamaa, iwe njaa, iwe mateso iwe kitu chochote kile anasema tutashinda. Hata ikiwa Msalabani. Hiyo ndiyo imekuwa kauli yake ambayo amekuwa nayo na mimi nimekutana nayo katika vipindi vyote nilivyokutana naye katika safari ya maisha na wito wa Kipadre.

Askofu msaidizi Kilaini amepembua mchango wa Askofu Severine hatua kwa hatua.
Askofu msaidizi Kilaini amepembua mchango wa Askofu Severine hatua kwa hatua.

Mtume Yakobo anatuasa akisema imani isipokuwa na matendo imekufa. Kama Nabii wa Mungu hapa jimboni Rulenge-Ngara ameimarisha vyombo vya unabii. Amewasaidia Mapadre wengi kwenda kusoma ndani na nje ya nchi ili waongeze: elimu, ujuzi na maarifa. Hivyo hapa Rulenge-Ngara tuna mapadre waliobobea katika elimu dini, iwe katika Maandiko Matakatifu, Maadili au iwe mambo mengine. Tunawakuta madaktari wa watu hospitalini, wapo walio mawakili, wahasibu, wataalam wa misitu, kilimo, wataalamu wa elimu na wa nyanja nyingine zote kwa sababu Baba Niwemugizi anataka kumwinjilisha mwanadamu mzima: kimwili na kiroho. Asante saana kwa kuwaelimisha Mapadre ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Amewaimarisha watawa Kwa mfano Shirika la Mt. Bernadeta ambalo amehakikisha linapata usajili mzuri na wa kudumu kutoka Roma. Masista wa Upendo Upeo, amehakikisha yeye kama Mwanasheria wa Sheria za Kanisa anawaweka katika msimamo thabiti ili waweze kuelekea katika utawa ulio sahihi na utawa ulio wa kweli katika Kanisa. Na Matokeo yake sasa wanaendelea vizuri na kushamiri vizuri, matendo makuu ya Mungu.

Amekua ni Askofu mwenye upeo mkubwa anayewasaidia watu kijamii mahali popote alipo. Mwaka 2014, aliitisha Sinodi ya Jimbo iliyoweka msimamo na maelekezo kwa Jimbo kichungaji na kijamii ambayo imekuwa ni dir ana mwongozo wa Jimbo mpaka Mwaka 2024, Sinodi ambayo ilinogeshwa na kauli mbiu: "Sinodi Rulenge-Ngara, Naamini na kuwajibika". Katika sinodi hii ameweza kuwahusisha watu wa kada zote mapadre, watawa, walei, wanawake, wanaume, vijana na watoto ili wote waanze kutembea pamoja ili waweze kutenda kazi inayoeleweka na kuaminika. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Askofu Niwemugizi umeweza kukutanisha watu mbalimbali ili waweze kuwa kitu kimoja na kuwa kitu kimoja kinachotembea pamoja. Hiyo ndiyo kazi ya kwanza ya Kasisi/kuhani mkuu akifuata kazi tatu zake Kristo: Unabii, Ukuhani na Uongozi na kwa namna hiyo ametangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kazi ya pili ni Ukuhani: Kwa ajili ya kutakatifuza watu. Ukuhani ni kubariki, ni kuleta neema. Na kwako Baba Niwemugizi kama tusomavyo kwenye Waraka kwa Waebrania maana kila Kuhani mkuu anatwaliwa kati ya watu na amewekwa ili kutolea dhabihu kwa ajili ya wanadamu wenye dhambi. Baba Niwemugizi wewe umechaguliwa na Kristo, ni mpakwa mafuta wa Bwana ambaye amekupa uwezo kufunga na kufungua, kuhuisha mapaji mbalimbali ya Roho Mtakatifu. Amekuchagua na Mungu anamchagua mtu akijua uwezo na nguvu zake akijua pia mapungufu na kasoro zake na anamtumia na kumtuma aende kufanya hiyo kazi. Kwa maana hakuna awezaye kujitwalia mwenyewe Heshima ya kuwa Kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa Kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni (Ebr.5:4). Naye Bwana Yesu anasema si ninyi mlionichagua Mimi bali ni Mimi niliyewachagua ninyi duniani nikawatuma mwende kutangaza Habari Njema. Kumbe, usiwe na hofu hata siku moja kwani wewe ni mpakwa mafuta wa Bwana, wewe ni mwekwa wakfu wa Bwana na wewe ni mteuliwa wa Bwana. Hivyo nenda mbele kaendelee na kazi ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Kazi ya tatu ya Askofu ni kuongoza akifuata mfano wa Kristo mfalme anapaswa kuongoza kila mahali anapokuwa. Akifuata mfano wa Kristo Yesu asemaye “Mimi ndimi mchungaji mwema mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.” Baba Askofu umeliongoza Jimbo kwa nguvu zako zote na uwezo wako kwa miaka hii 25. Lakini akiwa ni mchungaji aliyeguswa na uhitaji wa kondoo wake kadri muda ulivyoenda akaona mahitaji yanaongezeka akaona si vyema kuwa na eneo kubwa la Jimbo, akapanga na kuufuata taratibu ili Jimbo likatwe na kuzaliwa Jimbo la Kayanga. Hivyo Baba Askofu Niwemugizi ndiye mzazi wa Jimbo la Kayanga na ameliendeleza na kulisaidia Jimbo limeweza kwenda vizuri na ndipo akabakiwa na Jimbo la Rulenge - Ngara ambalo nalo ameliongoza na analiendeleza hili Jimbo. Tukiangalia maendeleo jamii kwa siku za hivi karibuni ameendeleza elimu kwa kuanzisha shule ya Mt. Severini ya Biharamulo ambayo matokeo yake ni mazuri pia shule ya wasichana ya Mtakatifu Clara na amefanya mambo mengine mengi ambayo yanasaidia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili.

Amejikita pia katika sekta ya kilimo na kupiga vita baa la njaa na utapiamlo popote alipokwenda, ikikumbukwa kuwa Kagera ni moja ya sehemu zenye utapiamlo wa kutisha. Mtakatifu Yakobo anasisitiza ndugu yako akija kwako akasema nina njaa na ukabaki kumpa pole ya maneno matupu anabaki na kwenda na njaa yake kama humpi chochote lakini wewe Baba Askofu Niwemugizi umejitahidi kusaidia watu katika mambo wanayo yafanya. Pia Askofu Niwemugizi imefahamika kuwa wakati wa Kwaresima ni kawaida yake kufunga na majitoleo yake huyakusanya na wakati muafaka ukifika wakati wa kipindi cha Pasaka huenda na kula chakula pamoja na wafungwa. Huu ni mfano mzuri na tena wa kuigwa katika huduma kwa wafungwa Magerezani ili kutambua kwamba, hali waliyo nayo ni ya kupita, hivyo wawe na matumaini ya kuwa huru tena na hatimaye, kuungana na familia na jamii zao katika ujumla wake. Kamwe wasikate tamaa! Pia Askofu Niwemugizi amekuwa ni tunu kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Amekuwa na msimamo usioteteleka, umakini wa kazi na ushujaa katika kuchukua maamuzi magumu na mazito. Na Kwa sababu hiyo katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi cha Miaka yake 25 ya Uaskofu kila mara amepewa majukumu nyeti.

Baada ya miaka Mitatu tu ya kuwekwa wakfu kuwa Askofu alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania na akaliongoza Baraza vizuri sana kwa vipindi viwili akiwa Askofu kijana kabisa. Baada ya kupumzika kidogo alichaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais wa Baraza, hivyo kila mara Maaskofu walihakikisha Askofu Niwemugizi yupo na majukumu muhimu na kwa muda mrefu yupo kwenye kamati tendaji ya Baraza la Maaskofu. Pia katika vitengo muhimu na nyeti kwa mfano kitengo cha maadili na ukaguzi wa fedha ya Kanisa hasa katika Taasisi za Baraza la Maaskofu amekua ni Mwenyekiti na hapa sehemu mambo yalipokuwa ndivyo sivyo yeye aliyanyoosha bila ya kusita. Mpaka sasa yupo kwenye kitengo cha kudhibiti madeni ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akiwa ndiye Mwenyekiti. Licha ya majukumu yote hayo bado amekuwa Chancellor wa Chuo Kikuu cha Mt. Agustino na vyuo vingine kadhaa pia vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Haya yote yameweza kusaidiwa na masomo yake aliyoyasoma Roma hasa kuhusu masuala ya Sheria. Tunamshukuru kwa kufuata nyayo za Bwana wetu Yesu Kristo ya kuchunga wake. Lakini, kazi ya kuchunga kondoo wa Bwana bado inaendelea na Mwenyezi Mungu akujalie nguvu za Roho na Mwili na Hekima ya Mungu ikuongoze kama ilivyo nembo yako ya kiaskofu na kila mara useme nitakipokea kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana. 

Askofu Niwe ametoa ushauri kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Askofu Niwe ametoa ushauri kwa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Baba Askofu NiweMugizi. Naye mwana shangwera Askofu Severine Niwemugizi akitoa neno la Shukrani alimshukuru Mungu kwa mema yote aliyomjalia katika maisha yake na utumishi wake ndani ya Kanisa. Aliwashukuru watu wote waliofika kakatika sherehe hiyo na wageni mbali mbali. Alimshukuru Rais Samia kwa kufika na kumpa heshima kubwa kutokana na majukumu na ikikumbukwa kwamba ni siku chache tu Rais alikua nje ya nchi katika majukumu ya kimataifa. Askofu Niwemugizi akakumbusha kuwa anakumbuka wakati wa kusimikwa kwake miaka 25 iliyopita alikuwepo Rais wa Kwanza wa Tanzania Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na William Benjamin Mkapa aliyekuwa Rais wakati huo. Na Kwa uwepo wake Rais Samia kwenye Jubilei hii ni ishara ya upendo na ni ishara ya kutaka pia kuwasikiliza watu wa pembezoni hasa wale wa Rulenge-Ngara.  Askofu Severine aliendelea kwa kusema karibu unatimia Mwaka mmoja tangu Rais Samia aliposhika madaraka ya kuiongoza nchi huku akiendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nchi. Na akaahidi kuwa ataendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kustawisha haki na ukweli, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi.

Askofu Niwemugizi amemwelezea Rais baadhi ya changamoto ambazo alimwomba amsikilize na aweze kusaidia. Yapo maeneo ambayo kwa Hati yanajulikana ni mali ya Kanisa lakini kwa wakati huu yana mgogoro wa umiliki kati ya Kanisa na taasisi nyingine za kiserikali hivyo akaomba wasaidiwe kupata ufumbuzi, pia kuna taasisi za Kanisa (hospitali) ambazo zina changamoto za madeni ya TRA kumbe, aliomba ikiwezekana kusamehewa madeni hayo lakini pia kuweza kupata vibali vya kuajiri watenda kazi katika vituo hivi vya huduma ya Afya. Tena shida ya maji kwenye mji wa Ngara ipatiwe ufumbuzi wa kudumu. Amezungumzia pia changamoto ya wakulima kunyonywa na baadhi ya watu au vikundi vya watu wanaochukua na kununua mazao kwa bei isiyo na tija wala manufaa kwa wakulima. Katika mradi wa uchimbaji wa madini ya “Nickel” kuna watu wanajipenyeza ambao sio wazawa na kujifanya ni wamiliki wa maeneo ili waweze kujipatia fidia, Pia ipo hali ya mauaji, ajali au watu kujiua katika jamii. Sababu zinazotolewa ni kutafuta utajiri au urithi, wivu wa mapenzi, ramli chonganishi na Mambo kama hayo. Akapendekeza kuwa ipo haja kwa viongozi wa dini na watu mbalimbali kukaa chini na kujadili ili kupata ufumbuzi nini chanzo cha mauaji haya na nini kifanyike. Kinachooneka ni kwamba dhamili za watu zimekufa hivi kwamba utu na thamani ya zawadi ya maisha haionekani kwa watu wengine, watu wanaona ni rahisi na sio shida kuutoa uhai wa mtu mwingine. Akabainisha kuwa ndani ya jamii mahali fulani maadili na utu wema na mafundisho ya dini yamepungua na hata yameachwa kufundishwa katika mashule. Amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan akuze haki ili haki izae amani ili hatimaye, kuweza kukuza mshikamano ili uongozi wake uendelee kuiheshimisha Tanzania.

23 February 2022, 15:54