Tafuta

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anawaalika watanzania kutafakari kuhusu mauaji yanayoendelea nchini Tanzania: Injili ya Uhai, Malezi na Mahangaiko ya watu. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anawaalika watanzania kutafakari kuhusu mauaji yanayoendelea nchini Tanzania: Injili ya Uhai, Malezi na Mahangaiko ya watu. 

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi: Mauaji ya Kutisha Tanzania

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, anawaalika watu wa Mungu nchini Tanzania kufanya tafakari ya kina kuhusiana na mauaji ya kutisha yanayoendelea kujitokeza nchini Tanzania. Katika kipindi cha takribani miaka kumi iliyopita kulitokea mauaji dhidi ya walemavu wa ngozi, balaa, janga na aibu kubwa kwa Taifa. Injili ya uhai, malezi na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waziri mkuu wa zamani Mizengo Kayanza Peter Pinda katika Maadhimisho ya Siku ya Walemavu wa Ngozi Tanzania tarehe 4 Mei 2010 alisema kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sehemu ya Tatu Ibara ya 12(1) na 14 inasema: “Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa. Kila Mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika Jamii Hifadhi ya Maisha yake kwa mujibu wa Sheria”. Moja ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania kupambana na mauaji ya walemavu wa ngozi ni pamoja na kuitisha Kura ya Maoni kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya Mapambano dhidi ya Vitendo vya Ukatili kwa Watu wenye Ulemavu wa Ngozi. Serikali iliwataka Wananchi kutaja Watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na Mauaji au kukata Viungo vya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi, wawataje Waganga wa Jadi wanaohusika, Wauaji, Wauzaji wa Viungo na wafanyabiashara wanaotumia Viungo hivyo. Zoezi la Kura ya Maoni lilifanyika kwa Mikoa yote mwezi Machi 2009. Mauaji ya walemavu wa ngozi yalisikitisha, kutikisa na kuliahibisha taifa la Tanzania. Hili lilikuwa kuwa kama balaa na janga la Kitaifa.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, anawaalika watu wa Mungu nchini Tanzania kufanya tafakari ya kina kuhusiana na mauaji ya kutisha yanayoendelea kujitokeza nchini Tanzania. Katika kipindi cha takribani miaka kumi iliyopita kulitokea mauaji dhidi ya walemavu wa ngozi, balaa, janga na aibu kubwa kwa Taifa. Kwa siku za hivi karibuni yamejitokeza matukio ya mauaji ambayo yanafikirisha sana kwani haya yanatokea ndani ya familia. Haya ni matukio yanayohitaji tafakari ya kina kutoka katika jamii na taifa la Tanzania katika ujumla wake. Watanzania wanalo jukumu zito la kujitazama kwa undani na kujiuliza ni kitu gani kinachojiri na sababu zake msingi. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anakiri kwamba, hapa hakuna majibu ya mkato. Lakini ni mambo mazito yanayopaswa kufanyiwa tafakari ya kina kuhusu thamani ya uhai!

Matukio ya mauaji nchini Tanzania yanatisha
Matukio ya mauaji nchini Tanzania yanatisha

Mababa wa Kanisa wanafundisha kwamba: Uhai au uzima wa kibinadamu ni kitu kitakatifu kwa sababu tangu mwanzo wake unahusiana na tendo la Mungu la uumbaji na daima unabaki na uhusiano na mafungamano ya pekee na Mungu Muumbaji aliye peke yake kikomo chake. Mungu peke yake ndiye mwanzo wa uhai, tangu mwanzo wake hadi mwisho wake. Hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujitwalia haki ya kuharibu moja kwa moja kiumbe cha kibinadamu kisocho na hatia. Uhai wa binadamu sharti uheshimiwe na ulindwe kwa namna iliyo kamili tangu nukta ya kutungwa mimba. Toka nukta ya uwepo wake, kiumbe cha kibinadamu lazima kitambuliwe kama kina haki za kibinadamu, miongoni mwao, ikiwa ni haki ya uhai isiyovunjwa ya kila kiumbe kisocho na hatia. Rej. KKK 2259-2270.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema uhai ni mali ya Mungu anayetoa, anayetawala na kuuthamini. Mwanadamu yeyote hana fursa wala ruhusa ya kuchezea, kudhalilisha au kuharibu uhai wa mwanadamu mwenzake, tangu kutungwa kwake mimba hadi mauti ya kawaida yanapompata. Kiumbe huyu ni mali ya Mungu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wake. Anao: utu, heshima na haki zake msingi. Inawezekana kabisa Tanzania wamesahau thamani ya uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu? Haya mauaji yanayoendelea ndani ya jamii yanaweza kuwaondolea watanzania mtazamo sahihi kuhusu Injili ya uhai. Kwa hakika kuna changamoto za kijamii mintarafu: mahusiano, mshikamano na mafungamano ya kijamii kuhusiana na mambo yanayowaandama watu wa Mungu nchini Tanzania au yale yanayopewa thamani zaidi.

Dumisheni Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.
Dumisheni Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasikitika kusema kwamba watu wamepotoka kuhusiana na mtazamo wa maisha; kanuni maadili na utu wema. Hii ni changamoto kubwa kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Katika malezi, Je, ni tunu gani ambazo watoto na vijana wanarithishwa katika jamii? Watanzania wamepoteza dira na mwamko wa kutoa malezi na makuzi bora, safi, sahihi na bayana kuanzia kwenye familia, shule na kwenye taasisi za malezi na hta katika jamii katika ujumla wake. Kuna mahangaiko makubwa katika jamii kutokana na ukata, umaskini na hali ngumu ya maisha; mambo yanayochangia watu kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha. Mwishoni wa tafakari yake, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam anachukua fursa hii kutoa mwaliko kwa watanzania kujitafiti, kujipima na kujitazama kwa undani kabisa ili kuona wako wapi! Wanakwenda wapi na kwa njia gani? Matukio ya mauaji na ukosefu wa maadili na utu wema yapewe uzito wa pekee na watanzania wajipime vyema, ili hatimaye, kujirekebisha; kwa kufanya toba na wongofu wa ndani. Kila mtanzania kadiri ya nafasi na wajibu wake ndani ya jamii ajibidiishe kuyatafakari matukio haya kwa kina, ili hatimaye waweze kuibuka na majibu muafaka yanayotosheleza kujibu changamoto hizi.

Mauaji Tanzania
14 February 2022, 15:15