WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam: Shukrani! Tathmini, Maadili na Malezi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha ya Kanisa. Ni muhtasari wa imani ya Kanisa na kielelezo cha juu kabisa cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Ni ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Hii ni Liturujia Takatifu na ya Kimungu inayowaunganisha na Kristo Yesu na hivyo kuwafanya kuwa ni washiriki wa Mwili na Damu yake Azizi, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao ya kila siku, yaani utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Ibada ya Misa Takatifu ina utajiri mkubwa wa Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Kwa kifupi kabisa, Ibada ya Misa Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka, shukrani, kumbukumbu na uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake.
Katika kipindi hiki kuelekea kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, hapo mwezi Septemba 2022, wanaongozwa na kauli mbiu “Nuru Yetu Iangaze! Tuyatakatifuze Malimwengu. Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, mshikamano na uadilifu wa uumbaji. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu Lk. 1:39: Mapendo kwa jirani: “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda…” Ni katika muktadha huu wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba OSA., wa Jimbo kuu la Da res Salaam, tarehe 22 Januari 2022 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa wema, upendo na huruma yake ya daima. WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam wametumia siku hii, kumwilisha imani katika matendo kwa kutoa msaada wa vifaa tiba, baiskeli za walemavu na kuchangia Bima ya Afya kwa watoto 30 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Na kabla ya hapo, walishiriki katika semina kuhusu moyo wa shukrani iliyoendeshwa na Padre Christian Likoko Nyumayo, Paroko wa Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Magomeni, Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba OSA., katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa Ibada ya Misa Takatifu katika maisha ya waamini kwani hiki ni kielelezo cha juu kabisa cha Sala ya Shukrani. Ni wakati wa kutathimini maisha, wajibu na utume wao kwa: Familia, Kanisa na Jamii, ili kukuza: Upendo, imani, maadili na utii, daima wakiwa wanyenyekevu. WAWATA watambue kuwa ni washiriki wakuu katika mchakato wa malezi na makuzi ya watoto na jamii katika ujumla wake. WAWATA wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu, WAWATA wanapaswa kujichunguza na kufanya tathmini ya kina katika ngazi ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Kwa kuangalia mahusiano na mafungamano katika maisha ya ndoa na familia: kwa kuchunguza: imani, uaminifu na amani, ili waweze kukuza umoja, ushiriki na utume. Bikira Maria ni mfano bora wa fadhila za Kikristo na tunu msingi za Kiinjili. Kiburi kinabomoa tunu msingi za maisha na kufunga milango ya neema na baraka. WAWATA wajenge kiu ya Neno la Mungu wanalopaswa kulisikiliza kwa makini, kulitafakari na hatimaye kulimwilisha, ili kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, yanayosimikwa katika: imani, huruma na mapendo kamili. Waamini wajitahidi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, ili iweze kukata kiu ya imani, matumaini na mapendo.
Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba OSA., amewataka waamini kamwe wasihudhurie Ibada ya Misa Takatifu kwa mazoea, kwani watabaki “watupu” na “wakavu” katika maisha ya kiroho. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yawakirimie amani, faraja na matumaini. Ekaristi Takatifu ijenge umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, Mungu yuko kati pamoja nao. Pale penye chuki, uhasama, magomvi na kiburi si rahisi sana kumwona Mungu. Huu ni wito kwa WAWATA kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo kwa kuonesha: Utii, unyenyekevu na kuendelea kuwajibika kwa vitendo. Wanawake Wakatoliki watambue kwamba, wao ni walezi muhimu sana wa maisha na tunu msingi za kiroho kwa watoto wao na jamii katika ujumla wake. Wanawake wajitahidi kuwa imara na thabiti katika mchakato wa malezi na makuzi ya watoto wao, daima wakiendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa uwepo wa Kristo Yesu kati pamoja nao. Wawe imara katika imani na kamwe wasikubali kuyumbishwa yumbishwa kama “daladala iliyokatika usukani.”
WAWATA wasaidiane katika safari ya maisha kwa kujenga na kudumisha ujirani mwema unaosimikwa katika: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani. Wajitahidi kuwa na matumizi bora ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wanawake wafanyakazi wawaheshimu na kuwathamini wafanyakazi wa ndani na kamwe wasiwanyanyase na kuwadhulumu, kwani matokeo yake ni majanga katika familia: ukatili na mauaji kwa watoto pamoja na ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa. Wafanyakazi wa ndani wakigeuzwa kuwa watumwa, jamii inaweza kukosa mwelekeo sahihi kwa siku za usoni kutokana na chuki na uhasama unaofichika katika malezi na makuzi. Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba OSA., amesema kuna viashiria vya kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ushoga na usagaji ndani ya jamii. Watoto wadogo, vijana na watu wazima kukosa adabu katika mavazi; moyo wa sala na ibada na matokeo yake ni maporomo ya ndoa.
Wanawake Wakatoliki wawe ni mfano bora wa malezi na makuzi kwa watoto wao na jirani zao, ili kupunguza wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sanjari na mimba za utotoni. Wawe ni vyombo vya huruma, upendo na msamaha na kamwe wasitake kulipiza kisasi kwani hawana kipimo sahihi cha haki. Kumbe, kuna haja ya kuwapenda adui zao na kuwaombea. Wajenge na kudumisha urafiki wa kijamii, kwa kuanzia katika familia zao. Bikira Maria Msaada wa Wakristo awasaidie na kuwaimarisha katika mchakato wa ujenzi wa kizazi kitakatifu kinachomcha na kumtukuza Mungu. Padre Christian Likoko Nyumayo, Paroko wa Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Magomeni, Jimbo kuu la Dar es Salaam wakati wa semina, amekazia umuhimu wa waamini kutambua kwamba, wakati mwingine shida na magumu katika maisha ni ngazi inayowawezesha kufikia katika mafanikio makubwa zaidi. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yosefu aliyetengwa na hatimaye, kuuzwa ugenini na ndugu zake, lakini hatimaye, akawa Waziri mkuu na kuikoa familia yake na baa la njaa na utupu wakati wa Mfalme Farao wa Misri.
Waamini wajifunze na kukuza moyo na utamaduni wa kushukuru kama alivyokuwa yule Mkoma kutoka Samaria alipogundua kwamba, amepona, akarudi kumtolea Mungu utukufu, sifa na shukrani. Ule muujiza wa Kristo Yesu kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na vipande viwili vya samaki ni kielelezo cha shukrani na moyo wa ukarimu. Kristo Yesu, alipokuwa nyumbani kwa Maria na Martha, alimshukuru Mungu na kumrejesha Lazaro aliyekuwa ananuka akiwa mzima kabisa. Harusi ya Kana ya Galilaya ni ishara ya kwanza iliyowarejeshea wanandoa wapya ile furaha ya maisha. WAWATA wametakiwa kuchukua hatua madhubuti kama kielelezo cha ujenzi wa umoja, ushiriki na utume kwa jirani zao wanaohitaji msaada zaidi. Waachane na tabia ya kulalama na kulalamika kwani haina tija wala mashiko. Wajitahidi “kugangamara” katika sala, maisha adili na matakatifu hadi kieleweke!
Kwa upande wake, Mama Stellah Rwegasira, Mwenyekiti WAWATA Jimbo kuu la Dar es Salaam na Katibu Mkuu WAWATA Taifa, amewapongeza Wakleri na wale wote walionogesha maadhimisho ya Sikukuu ya Shukrani kwa Mwaka 2021 na Kuomba Baraka na Neema kwa Mwaka 2022 wakati huu, WAWATA inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Katika kipindi cha mwaka 2021 WAWATA imepata mafanikio makubwa katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha kadiri ya katiba, taratibu, sera na mikakati waliyokuwa wamejipangia. Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Kijimbo kitakuwa ni Mwezi Agosti 2022. WAWATA Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama kielelezo cha imani tendaji, wametoa viti 13 kwa ajili ya walemavu, vifaa tiba pamoja na kuchangia gharama za Bima ya Afya kwa watoto 30. Mwaka 2022 kwa WAWATA ni mwaka imani, matumaini na mapendo thabiti!