Waamini Someni na Kuliishi Neno la Mungu Ili Kupambana na UKIRO
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, “Motu Proprio”: “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia Akili Zao” alianzisha Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Jumapili ya Tatu ya Mwaka wa Kanisa. Na kwa mwaka 2022, Dominika ya Neno la Mungu imeadhimishwa tarehe 23 Januari 2022. Hii ni Dominika kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari na kulieneza Neno la Mungu. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani huu ni wakati wa kuombea Umoja wa Wakristo. Juma la 55 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka 2022 linanogeshwa na kauli mbiu “Tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mt 2:2. Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Dei verbum” yaani “Neno la Mungu”, wanafafanua: maumbile na maana ya ufunuo; urithishaji wa ufunuo wa Mungu; Uvuvio wa Kimungu na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, Agano la Kale na Agano Jipya. Neno la Mungu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa.
Umoja wa Wakristo upate chimbuko lake kwa kusikiliza Neno la Mungu, linalofafanuliwa na wachungaji, kiasi kwamba, hata Mahubiri yanachukuliwa kuwa kama “Kisakramenti” muda muafaka wa kufafanua uzuri wa Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha ya waamini. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameadhimisha Dominika ya III ya Neno la Mungu kwenye Parokia ya Bikira Maria Mtakatifu, Kimara, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Amezindua maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki wa Tanzania, WAWATA katika ngazi ya Parokia sanjari na uzinduzi Kituo cha Maendeleo Parokiani. Katika mahubiri yake, amegusia historia ya Taifa teule la Mungu na zawadi ya huruma, upendo na wema wa Mungu; Kristo Yesu ni utimilifu wa Ufunuo wa Mungu kwa binadamu; Haki na wajibu wa kulisoma, kulitafakari na hatimaye kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi amesema, Mwenyezi Mungu alionesha upendeleo, huruma na wema kwa Waisraeli na kuwafanya wawe ni watu wake daima. Lakini katika historia ya maisha yao, ni watu waliokengeuka na kuasi Amri na maagizo ya Mwenyezi Mungu. Walikwenda kinyume cha mapenzi ya Mungu na kwenda kwenye njia za Mataifa, kiasi hata cha kutekwa na kupelekwa uhamishoni. Huko wakadhalilishwa, wakadhulumiwa na kunyanyasika sana. Walionja mateso na masumbuko ya wakimbizi na wahamiaji kiasi cha kumlilia Mwenyezi Mungu ambaye alisikiliza na kujibu kilio chao. Waisraeli wakiwa mbali na nchi na makazi yao walikosa fursa ya maadhimisho ya Ibada mbalimbali na kukosa ushuhuda wa imani yao. Waliporejea kutoka uhamishoni walianza kwa kujikita katika Neno la Mungu, kwa kusikiliza kwa shahuku na umakini mkubwa; kwa imani na heshima Kitabu cha Torati, Sheria za Musa zilipokuwa kizisomwa kati yao. Na huo ukawa ni mwanzo mpya.
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi amewakumbusha Wakristo kwamba, hata Kanisa ni Taifa la Mungu kama walivyo Wakristo nao ni watoto na Taifa la Mungu. Kristo Yesu ni utimilifu wa ufunuo wa Mungu, alionesha utii, unyekevevu, huruma na mapendo makuu kiasi cha kuwainua watoto wa Mungu katika hadhi na enzi, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Kristo Yesu alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina. Waisraeli walikuwa na hekalu mahali ambapo walikwenda kusali, kumwabudu, kumtukuza na kumtolea Mungu sadaka zao. Kila kijiji kilikuwa na Sinagogi lililotumika kwa ajili sala, kusoma, kutafakari na kufafanua Neno la Mungu. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi amewataka Wakristo kuondokana na “Ukristo uchwara” unaopelekea ugonjwa hatari sana wa UKIRO, yaani Ukosefu wa Kinga za Kiroho Mwilini kwa kushindwa kusoma, kulitafakari, kulitangaza na kulishuhudia katika uhalisia wa maisha.
Amewahimiza waamini wote kuhakikisha kwamba, wanakuwa na Biblia ya Kikatoliki yenye Vitabu vyote. Waamini wajenge utamaduni wa kutenga muda kwa ajili ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili liweze kuwa ni kanuni, dira na mwongozo wa maisha yao. Waamini wahakikishe kwamba, wanatumia vyema rasilimali muda ili kurutubisha maisha yao ya kiroho sanjari na kuimarisha imani, maadili na utu wema. Kila mwamini ajitambue kuwa ni mpenzi wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Theofilo yaani mpenzi wa Mungu. Kila Mbatizwa anapaswa kuwa ni mpenzi mwa Mungu ili aweze kuishi, kutangaza na kulishuhudia Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yake. Watambue kwamba, Kristo Yesu yuko kati pamoja nao katika Neno na Sakramenti zake. Kumbe, wanapaswa kumtukuza Mwenyezi Mungu ili mwanadamu aweze kutakatifuzwa. Watambue kwamba, wao ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, wenye dhamana na wajibu wao, kwani wanahitajiana na kukamilishana. Wakristo wahakikishe kwamba, wanajenga mwili wenye tija kwa unyenyekevu na uthabiti wa maisha adili na matakatifu. yanayompendeza Mungu na jirani.