Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana Jimbo Kuu la Dodoma: 163 Wapata Kipaimara Nkuhungu
Na Ndahani Lugunya, - Dodoma na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S - Vatican
Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho “vitae spiritualis ianua” na kwa njia hii, mwamini anaweza kupata Sakramenti nyingine zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanafanywa huru toka dhambi na wanazaliwa upya kama watoto wa Mungu, viungo vya Kristo Yesu, wanaingizwa katika Kanisa na kufanywa washiriki katika utume wa Kristo Yesu. Kimsingi Mababa wa Kanisa wanasema, Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na katika neno na hivyo kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini hushiriki mauti ya Kristo Yesu, huzikwa na kufufuka pamoja naye na hivyo kumvaa Kristo Yesu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Sakramenti ya Ubatizo inakuwa ni kuoshwa kunakotakasa, kunakotakatifuza na kuhesabiwa haki. Kwa njia ya Ubatizo dhambi zote huondolewa, dhambi ya asili na dhambi zote za mtu binafsi na pia adhabu zote za dhambi. Kumbe mbatizwa anakuwa ni kiungo cha Kristo, mrithi pamoja na Kristo Yesu, na Hekalu la Roho Mtakatifu na hivyo kupata neema ya utakaso na neema ya kufanywa haki kwa njia ya fadhila za Kimungu, Mapaji ya Roho Mtakatifu na Fadhila za Kimaadili.
Sakramenti ya Ubatizo, humwingiza mwamini katika Kanisa na hivyo kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo. Wabatizwa wanao wajibu wa kukiri, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ubatizo unamtia Mkristo alama ya mhuri wa kiroho usiofutika wa kuwa ni mali ya Kristo. Ubatizo hutolewa mara moja kwa daima, hauwezi kurudiwa. Ubatizo ni mhuri wa uzima wa milele. Rej. KKK 1212-1274. Ni kutokana na umuhimu huu, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wao. Kwani hii ni alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu, kwa njia ya Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni viumbe wapya, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, katika sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, tarehe 9 Januari 2022 ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa wakristo 163 kutoka katika Parokia ya Mtakatifu Gemma Galgani, Nkuhungu “kwa wajanja” Jimbo kuu la Dodoma.
Wakristo hao sasa watambue kwamba, kwa kupokea Sakramenti ya Kipaimara wamefanywa kuwa wakamilifu na kutajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivyo wanalazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Rej. KKK 1285. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amewakumbusha waamini kwamba, maji ni alama ya nje ya kile kinachofanyika kwa ndani. Kuna Ubatizo mmoja tu ambao umegawanyika katika makundi makuu matatu yaani: Ubatizo wa Maji na Roho Mtakatifu unaoadhimishwa katika mazingira huru kabisa. Ubatizo wa tamaa, huu ni Ubatizo kwa mtu ambaye yuko tayari kumkiri Kristo Yesu lakini anashindwa kupata huduma hii kutokana na mazingira mbalimbali, ingawa roho yake, iko tayari kubatizwa. Ubatizo wa damu ni kwa waamini ambao wako tayari kujisadaka na kumwaga damu yao kama kielelezo cha imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, kafa na kufufuka kwa wafu hata kama bado hawajabatizwa.
Hii ni changamoto kwa Wabatizwa kuwa makini katika imani yao na wala wasikubali kuyumbishwa yumbishwa kama “daladala iliyokatika usukani.” Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Sakramenti za Kanisa, tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Amewataka watu wa ndoa kuimarisha ndoa zao kwa tunu msingi za maisha ya Kikristo, huku wakisaidiana ili kwa pamoja waweze kuwa mawe hai katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wanawake katika familia wahakikishe kwamba, wanajijengea nguvu ya uchumi ili kuweza kupambana na kupanda kwa gharama ya maisha. Wanawake wasaidie kuchangia kuongezeka kwa pato la familia kwa kufanya kazi halali, kwa juhudi na maarifa.
Askofu mkuu Kinyaiya anawataka wanandoa wajitahidi kugawana majukumu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini watambue kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, Jimbo kuu la Dodoma hadi kufikia tarehe 9 Januari 2022 lina Parokia 51. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya amekitangaza kigango cha Mtakatifu Cecilia Muungano kilichoko chini ya Parokia ya Mtakatifu Gemma Galgani, Nkuhungu, kuwa ni Parokia teule na hivyo kulifanya Jimbo kuu la Dodoma kuwa na Parokia 51 na Parokia 1 teule.