Tafuta

Kardinali Joachim Ouédraogo, Askofu wa Ouagadougou- Burkina Faso. Kardinali Joachim Ouédraogo, Askofu wa Ouagadougou- Burkina Faso. 

Rais wa SECAM atoa wito kwa Tume ya Haki na Amani kusaidia wanaotengwa na jamii Afrika

Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM),Cardinal Ouédraogo wa Jimbo Kuu Katoliki la Ouagadougou,Burkina Faso ametoa wito kwa Tume za Haki na Amani kufanya juhudi zaidi hata kwa wale wanaoteseka na kutengwa na jamii.Ni katika muktadha wa Ujumbe wake kwa mwaka mpya 2022.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Katika Ujumbe wake wa Mwaka Mpya wa 2022, Kardinali Philippe Ouédraogo Nakellentuba, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki la  Ouagadougou, nchini  Burkina Faso, na  Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM), amesema Kanisa la Afrika linahitaji kuwa upande wa wale wanaoteseka. Kardinali kwa maana hiyo alihimiza Tume za Haki na Amani na Caritas za majimbo  kuongeza ufahamu kwa umma kuhusu haki za kijamii na kutetea haki za binadamu katika bara Afrika. Amesema hayo katika fursa ya ujumbe wake wa matashi mema ya Mwaka mpya 2022.

Bara la Afrika liwe na ufufuko wa kiuchumi

“Wapendwa wana na mabinti wa Bara la Afrika na Visiwani, mwanzoni mwa mwaka huu, ningependa kuwatakia afya njema, furaha na fanaka. Kwa 2022, ninalitakia Bara letu ufufuko mwema wa kiuchumi, bila ya madeni ambayo yamekuwa yakikabiliwa, Mshikamano uendelezwe katika baadhi ya nchi ambako njaa imeenea ili tatizo liweze kukomeshwa,” alisema Kardinali Ouédraogo.

Akiwalenga walioathiriwa na athari za kiafya na kiuchumi kutokana na UVIKO-19,  pamoja na waathirika wa  ghasia zisizo na maana ambazo zimesababisha wakimbizi na wasio kuwa na mazi wa ndani katika bara la Afrika, Kardinali amewaombea amani ya kweli. “Nawafikiria wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao, wahanga wa vita vya kindugu na ugaidi huku wakimkabidhi Mungu hatima yao ili suluhisho ipatikane kuwawezesha kutoka katika giza na uvuli wa kifo. Bwana hawaachi watu wake; anatutumia Mwanawe, ambaye tumesherehekea ukumbusho wake wa kuzaliwa wakati wa Noeli, ili atuokoe na atuletee amani kwa sababu yeye ndiye Mfalme wa Amani,” alisema Askofu Mkuu wa Ouagadougou.

Amani ni zawadi na tunda la kujitoa pamoja

Akirejea katika ujumbe wa Amani kwa mwaka 2022 wa Papa Francisko, Kardinali alisema: "Amani ni zawadi kutoka juu na ni tunda la kujitoa kwa pamoja.” Kwa maana hiyo alitoa wito kwa Wakristo wote barani Afrika kujenga madaraja ya udugu, ili kufikia utambuzi wa utamaduni wa kaka na dada. Kwa mujibu wa  Papa Francisko, "Sinodi ni mtindo, ni kutembea pamoja,na ni kile ambacho Bwana anatarajia kutoka kwa Kanisa la milenia ya tatu". Alikumbusha Kardinali

Mkutano Mkuu wa XVI  wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, ambao kwa kawaida hujulikana kama Sinodi utafanyika mwezi Oktoba 2023 jijini Vatican  ukiongozwa na kauli mbiu: "Kwa ajili ya  Kanisa la Sinodi: Ushiriki, Umoja  na Utume". Ufunguzi wa mchakato wa Sinodi ulifanyika kati ya tarehe 9 - 10 Oktoba 2021,  jijini Vatican na kufunguliwa baadaye kwenye majimbo yote ulimwenguni mnamo tarehe 17 Oktoba. Kwa maana hiyo, mashauriano haya ya ulimwenguni kuhusu Sinodi yanaendelea kwa sasa katika Kanisa duniani kote.

Kanisa lizidi kuwa katika njia ya sinodi na mashauriano ya sinodi

Kwa upande wake, Kardinali Ouédraogo amelialika Kanisa la Afrika kubakia katika mchakato wa njia ya sinodi kuhusu mashauriano ya sinodi. “Nuru ya Kristo iondoe giza la mashaka yetu na kutuangazia katika safari yetu ya kuelekea kwenye sinodi katika Kanisa letu, ambalo ni Kanisa-Familia ya Mungu katika huduma ya maskini na waliotengwa na jamii na daima tayari kuzungumza neno la kutia moyo wale wanaoteseka,” alisema Kardinali Ouédraogo.

04 January 2022, 14:36