Mtakatifu Yohane Bosco ni mwalimu wa karibu na vijana
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 31 Januari ya kila mwaka Mama Kanisa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, anayejulikana duniani Kote kwa jina Don Bosco. Ujumbe wa Mtakatifu Yohane Bosco kwa wakati huu na daima bado unaendelea kuwa msaada mkubwa kwa vijana katika matatizo au kwenye umaskini na hali zote ambazo zinamzunguka kijana wa jana, leo na kesho. Na hiyo inahusu wito wake wa utume katika kufundisha thamani ya familia kwa ngazi ya kimataifa, kikanda, kitaifa na kiamii kwa ujumla. Katika Familia ya Wasalesiani daima wamekuwa wakiendeleza kufanya mapokezi kwa njia nyepesi, ya upendo wa moja kwa moja kwa familia zote kuanzia kwa vijana wadogo.
Ndoto ya kinabii
Yohane Bosco alizaliwa tarehe 16 Agosti 1815 na Baba Francesco Bosco na mama yake Margherita Occhiena, karibu na Castelnuovo ya Asti, leo hii inaitwa Castelnuovo Don Bosco, Torino Italia na Baba yake alifariki mbamo mwaka 1917 akimuachia mke wake na watoto watatu. Ilikuwa miaka migumu sana kwa maradhi na njaa, lakini mama yake alijitahidi kuwatunza watoto na kuwalea malezi bora na vizuri. Alipokuwa na miaka 9, Yohane alipata ndoto ya kinabii iliyomtabiria utume wake kwa vijana na baadaye Mungu alizidi kumjalia karama nyingi za kipekee. Kufuatana na ndoto hiyo, Yohane aliamua kuwa padre, ingawa hakuweza kusoma hata shule ya msingi, kwa sababu shule ilikuwa mbali. Lakini taratibu mama alimfanyia mpango dhidi ya upinzani wa kaka yake. Wakati huohuo alianza utume wake akitumia vipawa vyake vya kiajabu. Tarehe 26 Machi 1826, siku ya Pasaka, alikubaliwa kupokea komunio ya kwanza kabla ya wakati. Kwa ushauri la Yosefu Cafasso, ambaye ni mtakatifu pia, tarehe 30 Oktoba 1835 alijiunga na seminari ya Chieri. Tarehe 3 Novemba 1837 alianza masomo ya taalimungu na tarehe 29 Machi 1841 akapewa daraja Takatifu ya ushemasi, ikifuatiwa mnamo tarehe 5 Juni 1841 daraja takatifu la upadre huko Torino, Italia.
Kuokoa watoto 7,184 waliokuwa wanafanya kazi viwandani
Badala ya kuitikia mialiko ya kufanya utume wenye malipo mazuri, mnamo Novemba 1841 alijiunga na Bweni la Torino, ambapo Padre Luigi Guala, akisaidiwa na Cafasso, alikuwa anakamilisha malezi ya mapadri vijana 45 ili waweze kukabili ulimwengu wa wakati huo. Huko Torino kulikuwa na watoto 7,184 chini ya umri wa miaka 10 waliofanya kazi viwandani. Yohane Bosco aliwatafuta ili kuwasaidia kijamii na mwongozo wa kidini. Pamoja na Cafasso alitembelea magereza akashtuka sana kuona hali ya wafungwa vijana, na kwa wema wake aliwavuta kumuahidia wamfuate mara baada ya kutoka.
Malezi yake na maarufu ziliangalia sana akili, dini, na upendo
Ilikuwa tarehe 8 Desemba 1841, Bartolomeo Garelli alikuwa wa kwanza kujiunga na kundi lake (Oratorio). Muda mfupi baadaye vijana walikuwa wengi hivi hata akahitaji msaada wa mapadre wengine watatu na vijana wakubwa kadhaa. Hatimaye tarehe 12 Aprili 1846 alipata nafasi kwa ajili ya vijana wake ambacho kilikuwa ni kibanda na kiwanja huko Valdocco. Yeye alijitahidi hasa kuwaelimisha watoto na vijana wa kiume wakati wa nyakati zake. Mbinu zake za malezi yake na maarufu ziliangalia sana akili, dini, na upendo. Hakutaka kurekebisha vijana kwa ukali, bali kuwakinga dhidi ya maovu kwa njia ya wema. Upendo wake wa ajabu kwa vijana ndio ilikuwa siri ya mafanikio yake ya ajabu katika malezi na ambayo ameacha urithi mkubwa kwa wafuasi wake ili kuendeleza utume wake huo popote ulimwenguni.
Alitangazwa Mtakatifu na Papa Pio XI mnamo tarehe 1 Aprili 1934
Mwaka 1854 alianzisha shirika la mapadre kwa ajili ya utume wa vijana (kwa kifupisho chake ni SDB) na miaka 10 baadaye alianza ujenzi wa mahali patakatifu pa Bikira Maria Msaada wa Wakristo yeye binafasi ndivyo alivyopendelea kumuita Mama wa Yesu. Mwaka 1872, pamoja na Maria Domenica Mazzarello, walianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaidizi, ili walee wasichana kwa roho ileile aliyokuwa ameanzisha. Mwaka 1875 alianza kutuma Wasalesiani wa kwanza nchini Argentina, na wakati huohuo alianzisha kundi la watawa wasaidizi alio waona kama “Wasalesiani wa nje”.Mtakatifu Yohane Bosco alifariki tarehe 31 Januari 1888 na Papa Pio XI alimtangaza mwenyeheri mnamo tarehe 2 Juni 1929 na kuwa Mtakatifu tarehe 1 Aprili 1934.Tangu wakati huo, Sikukuu yake ikawa kila tarehe 31 Januari ya kila mwaka.
Makardinali wa Salesiani ni 9
Kadinali wa kwanza wa Msalesiani alikuwa Giovanni Cagliero, iliyechaguliwa mnamo 1915 na Papa Benedikto XV, Tarehe 5 Oktoba, Papa Francisko aliunda makardinali wapya 13, akiwemo Kardinali Cristóbal López Romero, SDB. Sasa kuna Wasalesiani 9 ambao ni washiriki Baraza la Makardinali, 5 ni wapiga kura na kwa hivyo watakuwa na haki ya kupiga kura katika mkutano ujao: Kardinali Cristóbal López Romero, Kardinali Óscar A. Rodríguez Maradiaga, Kardinali Ricardo Ezzati Andrello, Kardinali Daniel F. Sturla Berhouet, Kardinali Charles Maung Bo. Na wanne (4) wasio piga kura ambao ni; Kardinali Angelo Amato, Kardinali Tarcisio Bertone, Kardinali Raffaele Farina na Kardinali Joseph Zen Ze-kiun.
Maaskofu wa Salesiani 132
Kuna maaskofu wa Wasalesiani 132. Askofu wa kwanza alikuwa Askofu Giovanni Cagliero, aliyetangazwa mnamo mwaka 1884. Askofu wa mwisho wa Kisalesiani aliyeteuliwa ni Lucas Jeimphaung Dau Ze aliyeteuliwa kuwa askofu mwandamizi wa Lashio, nchini Myanmar, tarehe 18 Oktoba 2019. Kuhusiana na shughuli za utume wa Padre watawa na vyama vyake ni vingi mno, ulimwenguni kote.