Iraq,Kard.Sako:Mivutano na migawanyiko isitishwe
Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.
Amani hupatikana wakati inapogeuka kuwa sehemu ya tabia na mwenendo binafsi. Hii inahitaji uwezo wa kufanya mazoezi ya uvumilivu, msamaha, mshikamano na ushirikiano. Amekumbusha hayo Patriaki wa Wakaldayo wa Baghdad, Kardinali Louis Raphael Sako, katika ujumbe wake wa mwaka 2022. Kwa mujibu wa Patriaki anaandika kuwa, Nchini Iraq wamepitia mazingira magumu sana, si tu baada ya kuanguka kwa utawala, bali katika historia yao yote. Wamekumbana na changamoto na mapambano ambayo yamewashinda watu na nchi. Sasa ni wakati wa kukagua kwa umakini fikra zao na misimamo yao ili kutoka katika hali hii ya kufa.
Mabadiliko ya Iraq yaanzie kwenye elimu
Ili kuanzisha mabadiliko na kufanya mema yaweze kutawala, kwa mawazo ya Patriaki amesema, ni lazima wasimame kidete dhidi ya uovu, bila kukata tamaa na kila mmoja atekeleze jukumu lake mwenyewe inavyotakiwa. Amani ni hitaji la mwanadamu, kidini na kitaifa. Ka sababu hiyo wajaribu kupatanda maadili makubwa kama vile amani, uvumilivu, msamaha na upendo ndani ya mioyo yao. Wawe wapenda amani, kama Kristo alivyotaka wote kuwa na aman na pia kuwa waaminifu kwa nchi yao, ambayo inawakilisha utambulisho wa na historia yao. Kwa kukazia Patriaki Sako ametoa ombi kuu la kuwajibika kwa kila mmoja.
Iraq ni nchi yao na historia yao
Katika ujumbe wake kwa maana hiyo Patriaki ameandika kwamba hawapaswi kuishia kwenye migawanyiko na mivutano, bali wabadilishe hali yao kwa kujiamini. Wafanya mageuzi ya elimu, afya na miundombinu. Mabadiliko hayo lakini yanaanza na elimu ya nyumbani, shuleni, makanisani na misikitini na kwenye vyombo vya habari, kwa kukizingatia ukweli kwamba ni lazima waishi furaha ya kweli kwa kupendana na kuheshimiana kama kaka na dada. Kwa sababu Iraq ni nchi yao na historia yao.