Tafuta

Maadhimisho ya Dominika ya III ya Neno la Mungu: Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya waamini na Liturujia ya Kanisa: Utukufu kwa Mungu na Utakatifu kwa mwanadamu. Maadhimisho ya Dominika ya III ya Neno la Mungu: Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya waamini na Liturujia ya Kanisa: Utukufu kwa Mungu na Utakatifu kwa mwanadamu. 

Dominika ya III ya Neno la Mungu: Umuhimu Katika Maisha na Liturujia

Lengo la Dominika ya Neno la Mungu ni kuwakumbusha waamini umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ili kujijengea utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kuliishi. Linakazia umuhimu na uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika Sadaka ya Misa. Neno la Mungu linatusaidia kumtambua Kristo katika Ekaristi Takatifu (Luka 24:45) pamoja na jirani

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Neno la Mungu” na Baba Mtakatifu Francisko kupitia Waraka wake wa Kitume - “Motu Proprio” - Aperiut illis: “Aliwafunulia akili zao” ya 30/09/2019, katika kumbukumbu ya miaka 1600 baada ya kifo cha Mtakatifu Yeronimo Jalimu na Gwiji wa Maandiko Matakatifu. Lengo ni kuwakumbusha waamini umuhimu na thamani ya Neno la Mungu katika maisha ili kujijengea utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kuliishi. Zaidi sana ni kusisitiza umuhimu na uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika Sadaka ya Misa Takatifu. Neno la Mungu linatusaidia kumtambua Kristo katika Ekaristi Takatifu (Luka 24:45), katika kuumega Mkate, Ekaristi Takatifu, Mwili wa Kristo ulio chakula chetu cha kiroho. Ndiyo maana Mtakatifu Yeronimo aliweza kuandika: “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo.” Kumbe tunapoadhimisha Dominika hii tunatafakari umuhimu wa Neno la Mungu katika Maisha ya Kanisa na maisha ya mkristo binafsi kama masomo ya dominika hii yanavyodhihirisha hasa somo la kwanza na Injili.

Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Nehemia (Neh 8:2-4a, 5-6, 8-10), Ezra anasoma Neno la Mungu - Torati – mbele ya wana wa Israeli waliorejea toka uhamishoni kama ishara ya kufanya upya Agano lao na Mungu. Historia inasimulia kuwa Ezra kuhani alikuwa mmoja wa washauri wa Mfalme Cyrus na Nehemia muandaaji wa divai kwa ajili ya mfalme walipokuwa uhamishoni. Baada ya waisraeli kurudi kutoka uhamishoni, walitumwa kwenda Yerusalemu kuwahamasisha watu kuishika sheria ya Musa, na taratibu za Ibada ili wasiigeukie miungu mingine kwa usalama wa kisiasa na kusimamia upya ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu. Kumbe Nehemia na Ezra walifanya kazi pamoja kuhakikisha miundo mbinu ya kiutawala wa kisiasa, kiserikali na kidini inaimarika. Walipofika Yerusalemu, waliitisha kusanyiko la watu wakawasomea Torati ili kuwakumbusha mambo makuu aliyowatendea Mungu na namna wanavyopaswa kuishika na kuiishi. Watu walipoisikia, waliitikia, Amina, Amina, wakainua mikono yao juu, kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi, wakalia kwa sababu mioyo yao ilichomwa na maneno ya torati yaliyowakumbusha upendo wa Mungu kwao ambao wao waliupuuza na kuudharau kwa kutoifuata Torati kwa kuishi kinyume na maagizo ya Mungu. Ezra kuhani, mwandishi, akawafariji na kuwatia moyo na kuwakumbusha kuwa siku ya sababto ni takatifu kwa Bwana, Mungu wao, wasiomboleze wala wala wasilie bali wale na kunywa wakimshukuru na kumsifu Mungu na kutenda mema.

Baada ya tukio hili watu wote kwa pamoja walifanya maamuzi kuishika tena sheria ya Musa, kuachana na tamaduni za kipagani ikiwa ni pamoja na kuwaacha wanawake wao wapagani waliosababisha kuabudu miungu mingine, kuchangia maendeleo ya Hekalu jipya na kuboreshwa Ibada katika Hekalu ikiwa ni pamoja na kuwategemeza makuhani. Watu wakabadili mfumo na mtindo wa maisha, wakiishika sheria ya Musa. Wakati huu, ndipo vitabu kadhaa vya Agano la Kale viliandikwa. Ni mwaliko kwetu kulisoma na kuliishi Neno la Mungu, tusizisahau sheria na maagizo yake kamwe katika maisha yetu popote pale tunapokuwa. Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 12:12-30) ni mafundisho ya Mtume Paulo juu ya umoja wa kijumuiya na wa Kanisa. Paulo analinganisha jumuiya ya waamini na mwili wa mwanadamu, ulioundwa na viungo vingi, na kila kimoja kina umuhimu wake katika kuujenga mwili mzima. Hakuna kiungo kisicho cha maana wala umuhimu kiasi cha kudharauliwa. Paulo analinganisha Kanisa na mwili wa Kiroho, ambapo Kristo ni Kichwa chake, na waamini ni sehemu za huo mwili - kila mmoja akiwajibika kuchangia kuujenga huo mwili mmoja kwa namna yake. Hakuna asiye wa muhimu katika ujenzi wa mwili wa Kristo - Kanisa. Kila mbatizwa anazo haki na wajibu wa kutekeleza.

Zaidi sana karama tunazojaliwa kwa kila mmoja, zote ni kwa ajili ya manufaa ya huo mwili mmoja. Hivyo kila mmoja anapaswa kutumia vyema karama na vipaji alivyojaliwa kwa maendeleo ya jumuiya ya waamini kwa manufaa yake na manufaa ya wengine. Injili tunayosoma mwaka C wa Kiliturujia ni ya Mwinjili Luka - mwandishi pekee wa Injili asiye Myahudi, mtu wa Mataifa, Mpagani, Tabibu wa Antiokia, aliyeongokea Ukristo. Sehemu tunayosoma katika dominika ya tatu imegawanyika sehemu kuu mbili: 1:1-4 na 4:14-21. Sehemu inayobaki ya sura 1:5-80, sura ya 2 na 3 zinazohusu habari za kuzaliwa kwa Yesu na Yohane Mbatizaji tulizisoma kipindi cha Majilio na Noeli. Na sehemu ya kwanza ya sura 4:1-13 ni sehemu ya majaribu ya Yesu Jangwani, tutakayoisoma kipindi cha Kwaresima. Katika sehemu ya kwanza 1:1-4, Luka anatomesha kuwa hakumfahamu Yesu kwa kukutana naye wakati wa maisha yake hapa duniani. Hata hivyo habari za Yesu alizoziandika ni za kweli kwasababu amefanya utafiti wa kihistoria kwa usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo na kutuandikia kwa utaratibu, ili nasi tupate kujua hakika wa habari za Yesu na mafundisho yake na kuamini. Luka alikuwa mtunza kumbukumbu wa Paulo katika safari zake za kimisionari.

Kumbe, amejifunza kwa Paulo habari za Yesu na za mitume kuziandika katika injili na kitabu cha Matendo ya Mitume. Na kuhusu habari za kuzaliwa kwa Yesu na Yohane Mbatizaji, mapokeo yanasema alipata masimulizi haya kwa Bikira Maria, maana wakati anaandika Bikira Maria alikuwa bado hai.Katika sehemu ya pili ya Injili ya dominika ya tatu (Lk. 4:14-21), Yesu anasoma Neno la Mungu katika Sinagogi la Nazareti siku ya Sabato. Itakumbukwa kuwa, baada ya kubatizwa na Yohane mtoniYordani, Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu mpaka jagwani akajaribiwa na shetani. Baada ya hapo alianza kazi ya kuhubiri na kufanya miujiza. Habari hizi zilifika Nazareti, kijijini kwake alikokulia. Naye aliporudi siku ya Sabato alienda kusali. Kwa kuwa walishasikia habari zake walimwomba asome neno. Wakampa chuo cha Isaya naye akasoma palipoandikwa – “Roho wa Bwana yu juu yangu, amenitia mafuta kuwatangazia maskini habari njema”. Alipomaliza kusoma; “alikifunga Chuo.” Hii inaonyesha kuwa amefunga na kukamilisha Agano la Kale na kufungua ukurasa wa Agano Jipya. Kisha aliwaambia watu kuwa; “Maneno yale yametimilika walipoyasikia.” Hii ni kusema kuwa Yeye ni mpakwa mafutwa wa Bwana. Hivyo ni Nabii, Mfalme na Kuhani wa Agano Jipya na la milele amekuja kuwatagazia watu habari njema.

Kumbe, tunaona kuwa Neno la Mungu linakuwa hai linaposomwa na kulisikilizwa katika kusanyiko la Kiliturujia kama alivyofanya Ezra katika Agano la Kale na Yesu katika Agano Jipya. Baada ya kusomwa na kulisikilizwa, Neno la Mungu lahitaji kumegwa kwa njia ya mahubiri na watu ambao Mungu anawachagua na kuwaangazia wawagawie watu kila mmoja apate sehemu yake. Ndiyo maana baada ya Ezra kulisoma neno, Nehemia na Walawi “waliwafundisha watu, wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.” Nasi tunapaswa kusikiliza kwa makini Neno la Mungu linapotamgazwa na mahubiri yanapotolewa ili kupata ujumbe unaotuhusu. Waisraeli walisikiliza Neno la Mungu likisomwa tangu asubuhi hata saa sita mchana. Baadaye Walawi wakaanza mahubiri kulifafanua neno. Basi tunapaswa tuwe na hamu ya kusikiliza Neno la Mungu katika mahubiri ili kila mmoja apate sehemu inayomuangukia kadiri ya maisha yake. Neno la Mungu ni Habari Njema ya furaha kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyosema; “Sheria ya Bwana ni kamilifu huiburudisha nafsi, maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo.”

Yesu anasisitiza; “Amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema; kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao; vipofu kupata kuona tena; kuwaacha huru waliosetwa; kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Nabii Amosi alisema; “Nyakati zaja ambapo nitawatumia watu njaa, si njaa ya chakula au kinywaji bali njaa ya kusikiliza Neno la Mungu” (Amo.8:11). Tunahitaji Neno la Mungu litushibishe, lituponye na udhaifu wetu tuweze kuishi kwa furaha. Neno la Mungu ni dira ya maisha yetu - si la kusikiliza tu bali ni la kuishi. Baada ya Walawi kumaliza mahubiri waliwaambia watu; “Enendeni mkale vilivyonona na mkawapelekee na wale wasio na kitu.” Neno la Mungu lilete mabadiliko katika maisha yetu. Lituletee faraja tukiwa na huzuni. Neno hili litujulishe mapenzi ya Mungu na kuyaongoza maisha yetu tuishi kama jamii moja. Neno hili litupatie maisha mazuri hapa duniani na baadaye mbiguni kwani maneno niliyowaambia ni roho tena ni uzima.

Dominika 3 Neno la Mungu
20 January 2022, 08:42