Tafuta

Shirika la Maria Imakulata, SMI linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu lilipoingia nchini Tanzania tarehe 26 Desemba 1972 Shirika la Maria Imakulata, SMI linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu lilipoingia nchini Tanzania tarehe 26 Desemba 1972 

Jubilei ya Miaka 50 ya Masista wa Maria Immakulata, SMI, Tanzania

Tunapozindua kufungua mwaka wa Jubilei ya Shirika tangu Shirika lifike Tanzania, tunapenda kutazama wakati uliopita kwa shukrani kubwa, kuishi wakati wa sasa kwa mapendo makubwa na kutazama wakati ujao kwa matumaini thabiti, tukiongozwa na kauli mbiu yetu hii “kuishi kwa umoja na upendo’’. Masista wa kwanza wa SMI walifika Tanzania tarehe 26 Desemba 1972. Yaani!

Na Sr. Maria Agnes Mwanajimba, SMI, - Dar Es Salaam, Tanzania.

Shirika la Maria Imakulata lilianzishwa mnamo mwaka 1854 huko Wroclaw, nchini Poland, na Mtumishi wa Mungu Padre Johanne Schneider. Shirika lilisajiliwa na kupata hati ya Kipapa tarehe 22 Desemba 1897.  Lilithibitishwa na hatimaye kupewa Hati ya Sifa. Mtumishi wa Mungu Padre Yohanne Schneider, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Maria Imakulata, SMI katika wosia wake alisema‘’ Mkitaka kunishukuru mtende matendo ya huruma kwa jina langu.’’ Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi.Hivyo basi tunapoelekea uzinduzi wa Jubilei ya miaka 50  hapo tarehe 8 Desemba tangu kuanzishwa kwa Shirika letu hapa Tanzania, ni nafasi pekee kwetu Wanaimakulata ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote aliyomtendea kila mmoja wetu, Shirika na Kanisa katika ujumla wake.

Masista wamisionari wa kwanza watatu kutoka Jimbo la Wroclaw nchini Poland, walifika nchini Tanzania tarehe 26 Desemba1972  kufuatia mwaliko wa hayati Askofu Arnold Cotey, SDS wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na kuwakaribisha kwa wakati ule katika kijiji cha Kilimarondo. Masista walipofika maisha yalikuwa ni magumu na hata upatikanaji wa vitu muhimu ilikuwa ni ngumu, hivyo walipata chakula na mahitaji muhimu kutoka nyumba kuu ya Shirika kwa ajili yao na jamii iliyowazunguka. Pia walipata changamoto ya lugha, hivyo mara walienda kusoma lugha ya Kiswahili kwenye Shule ya Lugha Makoko, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania ili waweze kuwasiliana vyema na watu mahalia na hata waliweza kujifunza lugha ya Kindonde ambayo ni lugha ya wanakilimarondo ili kuweza kuendesha utume wao vizuri. Baada ya kukaa, kutafakari na kupanga na Paroko, wakafikia muafaka kwamba, Masista wajielekeze zaidi katika Katekesi, Semina na Mafundisho ya Kikristo ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa watu wa Mungu.

Jambo la msingi lilikuwa ni ushuhuda wa maisha ya pamoja kati yao na wananchi wa Kilimarondo. Waliwaandaa waamini kuweza kupokea Sakramenti za Kanisa pamoja na kuadhimisha vipindi mbalimbali vya Liturujia ya Kanisa kwa uelewa na ushiriki mkubwa zaidi. Ibada ya Misa Takatifu chanzo na kilele cha maisha ya Kanisa ilipewa kipaumbele cha kwanza. Juhudi za katekesi na ushuhuda wa maisha ya watawa hawa zilikuwa ni msingi wa watu wengi kumwongokea Mwenyezi Mungu. Masista waliwashirikisha pia waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Hivyo basi asili ya kufaulu kwa Masista wetu wa kwanza kulitegemea bidii yao ya kujua maisha ya kimisionari katika juhudi walizofanya, kuungana na Kristu kati ya watu, kutembea katika nuru yake, na kuishi katika upendo kati yao wenyewe. Lengo ni kumsogeza Kristo kati ya watu. Hivyo maneno haya ya Baba mwanzilishi, ‘’Msimamo wa kiroho hasa katika kuhudumia na kujitoa bila kuchoka’’ yaliwaongoza na kuwaletea heri na baraka tele!

Elimu ambayo haina mwisho ni nguvu ya mwanadamu, walihakikisha watoto wanapata elimu ya awali hivyo walijishughulisha na chekechea, pia waliwakaribisha watoto wote bila kujali dini wala uwezo wao wa kiuchumi ili waweze kujua kusoma na kuandika, vinginevyo watoto hawa wangebaki  nyumbani na hivyo kukosa fursa ya kujiendeleza na masomo. Wale ambao walikuwa hawana uwezo waliwasaidia hata kuwapeleka kusoma zaidi. Pia walijali vipaji vyao,  waliwapa maarifa ya nyumbani kwasababu ya utambuzi wa kijamii wakijaribu kutoa huduma za kutuliza shida za nyakati. Ili kutimiza utumishi waliokabidhiwa na Shirika na Kanisa kwa ujumla. Masista waliheshimu na kuzingatia: mila, desturi na utamaduni wa watu mahalia na hivyo, iliwawezesha kuwasaidia kukusanya taarifa za mila na desturi hasa kuhusu tohara ya wavulana na unyago kwa wasichana, kupitia mila hii walipata njia nzuri  kwa ajili ya kufundisha katekesi! Waliwashauri wavulana kufanyiwa tohara hospitalini badala ya porini. Wakawa wanakaa Parokiani katika bweni maalum wakitibiwa na kupatiwa dawa. Ilikuwa ni fursa nzuri kwa Mapadre na Makatekista kuwafundisha katekesi pamoja na kuwapatia malezi bora ya Kikristo

Na kwa wasichana pia masista walitumia nafasi hiyo kuwafundisha katekesi, kwa hiyo hao watoto wakawa mfano mzuri kwa watoto wenzao na majirani. Na siku ya kutoka jando na unyago waliadhimisha misa pamoja na wazazi na wakapata zawadi na baada ya hapo walirudi nyumbani kusherehekea  na wazazi wao. Zote hizi zilikuwa ni juhudi za utamadunisho kwa hiyo kwa mtindo huu uliwafanya watu waelewe vizuri Ukristo. Shukrani kubwa sana kwa wamisionari wetu waliofanya kazi kwa juhudi na maarifa bila kuchoka na kujitoa bila kujibakiza kwa upendo, wanastahili pongezi kwani walifanya kazi kwa moyo mkuu. Kwa vipaji na karama kwa madokezo na maarifa, kwa moyo wa bidii na nia ya kuhudumia, roho ya Baba mwanzilishi iliwasukuma kujaribu kujenga tabia njema na kuheshimu nafasi za wengine. Walikwenda katika njia za haki na kudumu katika upendo na umoja.

Majitoleo yao kwa wasiojiweza, wazee na wagonjwa. Huduma hii iliyotolewa na wamisionari hawa wa Maria Immakulata inaendelea hadi leo katika Zahanati ya Nanjota na katika baadhi ya nyumba zetu. Mchango wao ulikuwa wa hali ya juu kiasi cha kuokoa maelfu ya watoto waliokuwa na utapia mlo wa kutisha pamoja na vitisho vya imani na mila potofu. Walisaidia pia kuboresha hali ya maisha na makazi ya watu. Kwa mara ya kwanza Shirika liliwapokea wasichana kutoka Tanzania tarehe 8 Desemba 1988. Hawa walikuwa wamehitimu elimu ya msingi na maarifa ya nyumbani. Idadi yao walikuwa ni wasichana 10. Lengo lilikuwa ni kuendeleza karama ya Baba mwanzilishi Johanne Schneider. Pia ilikuwa ni nafasi nzuri ya kuwafundisha mafundisho ya dini kwa kuwapatia elimu, ujuzi, maarifa na stadi za maisha. Kweli Masista walifanya kazi kubwa sana bila kujibakiza, kulea vijana siyo rahisi changamoto hazikosekani lengo lilikuwa ni kujenga roho ya uchaji wa Mungu, kusali, kuabudu, kutafakari Neno la Mungu pamoja na kujikita katika maadili na utu wema. Kati ya vijana hawa wengi wao walibahatika kuwa ni watawa na wengine, waliolewa na kuanzisha familia zao, leo hii wengi wao ni mfano bora wa kuigwa. Kwa utume wao walitekeleza nafasi ya kinabii. Hakika masista hawa wamisionari katika mstari wa mbele wameitikia ujumbe ule ule wa utume wa Yesu Kristo wa kwenda kuwafanya wote kuwa wanafunzi wake.

Utume wao ni somo, walishirikiana katika furaha na huzuni, walieneza Injili ya Mungu kwa upendo mkubwa kwa kuyaishi maisha ya kiroho. Kwa Roho ya mwanzilishi walijitoa katika kusaidia ulimwengu. Furaha yao ilkuwa kuwashirikisha wengine katika ukuaji na mwendelezo wa Habari Njema. Hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kazi kubwa ya Masista wetu wamisionari, kwa bidii yao waliyoifanya katika utume, kutembea katika nuru ya Kristo, kuishi katika upendo kati yao, yote hayo ni zawadi. Walivutwa na maneno ya Baba yetu “saidieni kuokoa roho zilizo katika hatari ya kupotea” kutokana na moto huo wakaona uhitaji kwa vijana hasa wasichana waliokuwa katika hatari ya kupotoka kimaadili. Kwa moto huo Sr, Innosensia na Sr. Consolata waliamua kuchukua uamuzi wa kwenda ngazi za juu serikalini kuomba Kilimarondo ifunguliwe shule ya wasichana ya maarifa ya nyumbani lengo lilikuwa kusaidia hasa wasichana walioizunguka Parokia ya Kilimarondo, Mbondo, Chimbendenga, Matekwe, Kiegei, Lionja na Mnero. Kunako mwaka 1986 Masista wao walitoa bweni kwa wasichana na chakula ili wale wasichana ambao hawakuchaguliwa kwenda sekondari wasome shule ya Maarifa ya Nyumbani ambayo ilifunguliwa rasmi mwaka 1988.

Kwa maongozi ya Mungu waliweza kumudu nyajibu zao siyo kwa sababu ya mali na fedha bali kwa moyo wa upendo, majitoleo na sadaka. Pamoja na juhudi kubwa waliofanya Masista wetu wa kwanza katika kuinjilisha, pia walipata changamoto mbalimbali kama ilivyo katika kila sekta mapungufu hayakosekani, Hivyo mnamo mwaka 1990-1991 ilitokea dhoruba katika utendaji wao na hivyo ikapelekea  mkuu wa Shirika duniani  Sr. Angela Cubon kufunga nyumba ya Kilimarondo na ikabaki nyumba moja tu ya Nanjota. Tunapoelekea kufungua mwaka wa Jubilei ya Shirika tangu Shirika lifike Tanzania, tunapenda kutazama wakati uliopita kwa Shukrani kubwa, kuishi wakati wa sasa kwa mapendo makubwa na kutazama wakati ujao kwa matumaini thabiti, tukiongozwa na kauli mbiu yetu hii “kuishi kwa umoja na upendo’’ ni maneno ya wosia ya Mtumishi wa Mungu baba Johanne Schneider Mwanzilishi wa Shirika letu. Hivyo tutakuwa na kipindi cha tafakari kwa mwaka mzima kwa mema mengi aliyotutendea kila mmoja pekee, Shirika na hata Kanisa katika ujumla wake.

Juhudi za hawa masista na uaminifu wao ndiyo umepeleke neema ya Mungu ya kufanya Shirika kukua na kuendelea kuongezeka kwa miito. Mbegu iliyopandwa Kilimarondo na wamisionari hawa ndiyo leo hii umekuwa mti mkubwa uliozaa matunda mengi mengi sana, matunda hayo sasa yameenea Jimbo la Tunduru-Masasi kwenye Parokia za Nanjota, Chikukwe, Masasi, Masasi – Macdonald, Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, Kurasini na Jumuiya ya Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania. Jimbo la Same tuko Mwanga na Kilomeni.  Jimbo kuu la Dodoma ni huko kwenye Parokia ya Kongwa pamoja na Jimbo la Morogoro, huko Mikumi na Msolwa. Kwa juhudi ileile waliyokuwa nayo Masista wetu wa kwanza ni tunu na hazina kubwa kwetu kuiendeleza, kwani hadi sasa Masista wengi wameelimishwa na wanaendeleza kazi na utume wa kimisionari na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Tunafanya utume wetu kama wauguzi, walimu na makatekista. Masista wanatoa semina kwa wanawake, vijana na watoto bila kujali dini wala itikadi zao. Pia katika kila Jimbo tunalofanya kazi tumejaribu kuanzisha Chama cha Kitume cha Bikira Maria ili kuwafundisha watoto maadili mema na kusali pamoja nao. Na kwa njia hii tunapata miito kutoka chama hiki kwa wale wanaopenda kujiunga nasi. Hivyo tasaufi na Ibada kwa Bikira Maria ni sehemu ya Shirika kwani toka mwanzo Shirika lilianza na chama tu cha Maria na ndipo baadaye kikapewa hadhi ya Shirika. Tunajivunia kwani hii ni sehemu ya mapokeo na utamaduni wa Shirika letu, tutauendeleza!

Tunapomshukuru Mungu hivi, tunaonja kwamba bado tunahitajika katika kuendeleza kazi ya ukombozi, tuwe tayari kutumwa kufanya kazi panapohitajika ili kuitikia mwaliko wa Kristo aliyesema, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt. 28:19-20. Hivyo basi Mungu amekuwa wapekee kwa kila mmoja wetu kwa namna yake anatualika tutambue wapi yuko wapi anatuongoza. Tunapoendelea kuishi hapa duniani tunaalikwa tutambue ukuu wake na tumfanye atambulikane popote tutakapokuwepo. Kila mmoja wetu amepewa mbegu iliyo bora tuipande, tuimwagilie na tuitunze ili ikue vizuri na izae matunda yaliyo bora. Hazina yetu kuu ni “upendo na umoja” ambayo itatuwezesha kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano wa kidugu kama hawa masista ambao ni mfano bora wa kuigwa katika utume wetu. Majitoleo yetu yanakuza upendo na kutufanya tuwe wamoja. Tuombeane baraka ya Mungu kwa kile tunachokifanya ili Mwenyezi Mungu aweze kutukuzwa na mwanadamu aweze kutakatifuzwa na kukombolewa!

Imeandaliwa na

Sr. Maria Agnes Mwanajimba, SMI

Mkuu wa Shirika la Masista wa Maria Imakulata

Kanda ya Tanzania.

Masista wa Immakulata
07 December 2021, 17:27