Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa. Vueni nguo za huzuni, jivikeni nguo za utukufu. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka C wa Kanisa. Vueni nguo za huzuni, jivikeni nguo za utukufu. 

Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Acheni Huzuni, Vaeni Utukufu

Masomo ya dominika hii ya pili ya majilio yamebeba ujumbe wa matumaini unaotualika tuvue nguo za huzuni na kuvaa nguo za utukufu kwa sababu Bwana anakuja kutukomboa. Hivyo, anatualika kwa njia ya Neno lake kuitengeza njia yake nyoyoni na kuyanyoosha mapito yake, tukiyaondoa yote yanayotuletea huzuni na tuweke juhudi kuyadumisha: furaha, amani na upendo.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Majilio mwaka C.  Masomo ya dominika hii ya pili ya majilio yamebeba ujumbe wa matumaini unaotualika tuvue nguo za huzuni na kuvaa nguo za utukufu kwa sababu Bwana anakuja kutukomboa, maana wokovu ni zawadi kutoka kwake anayotujalia bure kabisa, kwa upendo mkuu pasipo mastahili yetu. Ni Yeye tu awezaye kutuokoa. Hivyo anatualika kwa njia ya Neno lake kuitengeza njia yake katika mioyo yetu na kuyanyoosha mapito yake, tukiyaondoa yale yote yanayotuletea huzuni na tuweke juhudi kuyadumisha yale yote yatuleteayo furaha na amani. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Baruku (5:1-9). Baruku alikuwa katibu wa Nabii Yeremia aliyeishi miaka 600 kabla ya Kristo. Kawaida katika maandiko Matakatifu Manabii wanailinganisha Yerusalemu na mwanamke au mama, na watoto wake wakiwa ni watu wa Israeli. Baruku anailinganisha Yerusalemu na Mjane anayewalilia watoto wake waliochukuliwa mateka na kupelekwa uhamishoni Babeli. Kwa mjane huyu, kibinadamu, watoto wake walionekana kama wamekufa. Hapakuwa na matumaini yoyote kwao kurudi tena Nyumbani-Yerusalemu kutoka uhamishoni Babeli. Ndiyo maana Baruku anamwonesha Mjane-Yerusalemu akiwa amevaa mavazi meusi akisikitika na kuomboleza juu ya wanawe walioko uhamishoni, kana kwamba wameshakufa.

Nabii anamfariji Mjane-Yerusalemu akimwambia: “Ee Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni, uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu wa milele.” Baruku anaialika Yerusalemu kufurahi kwa sababu, siku yaja ambapo Mungu atawarudisha tena wanawe kwake kutoka uhamishoni. Masimulizi yanasema kuwa walipochukuliwa mateka kupelekwa uhamishoni, walifungwa minyororo na kuteswa sana na maaskari. Lakini sasa wanaambiwa, siku inakuja ambapo badala ya kuteseka watarudi wakiwa na wingi wa furaha wakishangiliwa kama wana wa Mfalme Mkuu. Mungu atahakikisha kwamba safari yao ya kurudi nyumbani ni safari ya furaha na mafanikio kwani watatembea kwa furaha kama watu huru. Na watakaporudi nyumbani, wataanza kuishi maisha matakatifu wakiwa na mahusiano mazuri na mema na Mungu wao kuliko hapo mwanzo maana Mwenyezi Mungu mwenyewe atawatakasa na dhambi zao zilizosababisha wakapelekwe uhamishoni. Yahweh atakuwa Mungu wao tena baada ya kutaabika na kurandaranda mbali naye, watakuwa watu wake waaminifu kweli.

Unabii huu wa Baruku ulianza kukamilika wakati Cyrus, Mfalme wa Persia, alipowatangazia uhuru wa yeyote anayetaka kurudi Yerusalemu na aende. Lakini waliorudi ni wale waliokuwa katika hali ya umaskini. Ijapo walifurahia kurudi nyumbani Yerusalemu, maisha bado yalikuwa magumu kwa kukosa uhuru wa kisiasa na kiuchumi. Ni wazi walifanikiwa kulijenga upya Hekalu na kuta za mji wao zilizobomolewa na baada ya muda mageuzi ya kiroho yalianza kujionesha kati yao. Lakini haikuchukua muda maskini walianza kugandamizwa tena na ndugu zao, waliofaidika na rasilimali za mji ule. Viongozi wa serikali na dini waliochukua madaraka, hawakuwa watetezi wa watu wao, bali watesi kinyume kabisa na kile alichowaambia Nabii Baruku. Furaha aliyowatangazia Baruku ikawa ndoto. Hii ni kwa sababu tangazo la kurudi kwao nyumbani ni utabiri tu wa kitakachotokea siku ya mwisho wakati wa hukumu ya mwisho huko mbinguni iliko Yerusalemu Mpya.

Mtume Paulo katika Somo la pili la Waraka wake kwa Wafilipi (1:3-6, 8-11), anawasifu Wafilipi kwa uhodari katika maisha ya kikristo, ambayo yamewasukuma wengi kuiamini Injili. Paulo hajivuni kutokana na kazi aliyoifanya bali anasema kuwa mafanikio hayo ni kwa sababu ya Kristo mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu, aliyesukuma mioyo ya Wafilipi kuipokea Injili, na Kristo pekee ndiye mwenye uwezo wa kuhitimisha wokovu wao kwa furaha (Filp 1:6). Upendo wao kwa Yesu na kati yao ni lazima uongezeke siku baada ya siku. Zaidi sana wanapaswa kuendelea kuishi maisha yasiyo na lawama, ili kumwezesha Kristo akamilishe wokovu wao wakati wa ujio wake wa pili. Huu ndio mwaliko wa mama kanisa kwa wanae kipindi hiki cha majilio. Injili ilivyoandikwa na Luka (3:1-6); imegawanyika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inatueleza ni lini katika historia ya dunia na ya wokovu, Yohane alianza kazi yake ya kuhubiri juu ya matayarisho ya kumpokea mwokozi. Ni mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberia, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode (mtoto wa Herodi aliyewaua watoto wa Bathlehemu akijaribu kumwangamizi mtoto Yesu bila mafanikio) akiwa mfalme wa Galilaya na Filipo, ndugu yake akiwa mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa aliyeteuliwa na mamlaka ya Kirumi kuwa Kuhani Mkuu huko Yerusalemu, akichukua nafasi ya Anasi Baba mkwe wake, baada ya kuondolewa ukuhani na mamlaka hiyohiyo ya kirumi.

Lakini pamoja na kuondolewa Ukuhani mkuu, Anasi alikuwa bado na ushawishi mkubwa, kwani hakuna lililofanyika bila kupata ushauri wake. Ni wakati huu neno la Mungu lilipomfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani. Kutajwa kwa viongozi hawa ni kutudhihirishia kuwa mambo haya ni ya kweli na sio ya kutunga. Lakini kwa upande mwingine tunaona kuwa Mungu hakuwachagua hata mmoja wa hawa watawala wanaotajwa. Hii ni kutuonyesha kuwa wokovu wa wanadamu ni mpango wa Mungu na upo mikononi mwa Mungu na sio katika uwezo wa mwanadamu. Hakuna mtu aliye na mamlaka yakujikomboa mwenyewe au kuwaokoa wengine ndiyo maana hata Yohani Mbatizaji, aliyejawa na Roho Mtakatifu angali bado tumboni kwa mamaye Elizabeti (Lk 1:15, 41), kwa unyofu anang’amua na kudhihirisha udhaifu na dhambi zake, na kwamba hata yeye anamhitaji Yesu apate kuokoka: “Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?” (Mt 3:14). Sehemu ya pili ya Injili imebeba Ujumbe wa Yohane Mbatizaji juu ya Ubatizo ambayo ni alama ya toba na wokovu kwa wanaotubu.  Tunaalikwa kuitengeneza njia ya Bwana, kuyanyoosha mapito yake, palipo na mabonde tupainue, palipo na mlima na kilima tupashushe, palipopotoka tupanyooshe na palipoparuza tupasawazishe (Isa 40:3-4). Huu ndio ulikuwa wakati wa kuanza kutimia unabii wa Baruku (Bar 5:7). Jambo hili litakamilishwa kwa ujio wa pili wa Masiha, ni wakati huo tu, sote tutakuwa wana wa familia ya kifalme: Familia ya Mungu wa kweli huko mbinguni, Yerusalemu mpya.

Kumbe, tunaona kuwa Hekima na mamlaka ya kibinadamu pasipo Mungu hayawezi kutuokoa kutoka utumwa wa dhambi. Tukumbuke daima kuwa dhambi inatutenga na Mungu na hivyo tunapoteza furaha na kuwa na huzuni. Adamu anasema; “Niliposikia sauti yako niliogopa nikajificha” (Mwa 3:10). Hofu inaleta huzuni. Dhambi pia inatutenga na wenzetu na kuharibu mahusiano yetu na kutuletea chuki na huzuni. Adamu akasema; “Huyu mwanamke uliyemweka hapa pamoja nami alinipa nami nikala” (Mwa 3:12). Dhambi inatuharibia urafiki wetu na ulimwengu na viumbe wengine. Mwanamke akasema; Nyoka alinidanganya nami nikala. Ndipo sasa Mungu akatoa adhabu akisema; “Ardhi itakuzalia miiba na utakula kwa jasho” (Mwa 3:18), kwa sababu umefanya haya utazaa kwa uchungu, utamponda nyoka kichwa naye atakuponda kisigino” (Mwa 3:15). Dhambi hutufanya kuwa watumwa wa shetani. “Maana kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi” (Yn 8:34). Hivi ndivyo dhambi inavyoleta mtafaruku katika maisha yetu na kutuvisha mavazi ya huzuni. Baruku anamwambia kila mmoja wetu; “Vua nguo za matanga na huzuni, uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu.” Popote pale penye ugomvi, hasira, huzuni, malalamiko lazima kuna dhambi. Kwa hiyo tunaalikwa kuvua nguo za huzuni, kuondoa dhambi na kuvaa nguo za utukufu kwa kujipatanisha na Mungu. Yohane alihubiri toba kama maandalizi ya kumpokea Mwokozi. Sisi tunaalikwa kukiendea kitubio na kuvua dhambi ili tuvae neema ya utakaso ndipo tutakapofurahi na kuimba; “Nitafurahi sana katika Bwana, maana amenivika mavazi ya Wokovu, amenifunika Vazi la Haki” (Isa 61:10).

Majilio J2
02 December 2021, 15:19