Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limezindua rasmi maadhimisho ya Mkutano Mkuu 20 wa AMECEA utakaoadhimishwa nchini Tanzania Julai 2022. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limezindua rasmi maadhimisho ya Mkutano Mkuu 20 wa AMECEA utakaoadhimishwa nchini Tanzania Julai 2022. 

Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa AMECEA 2022 Yazinduliwa Mwanza

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., tarehe 7 Novemba 2021 limezindua Maandalizi ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Tanzania ndiye mwenyeji wa Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA utakaofikia kilele chake mwezi Julai 2022. Pia uzinduzi wa Sinodi ngazi ya Kijimbo na Harambee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake tarehe 10 Oktoba 2021 mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” alikazia mambo makuu matatu: Kukutana, Kusikiliza na Kung’amua. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati wa Sala, Ibada na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu. Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume katika ukweli, uwazi, uwepo na ujasiri! Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., tarehe 7 Novemba 2021 limezindua Maandalizi ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Tanzania ndiye mwenyeji wa Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA utakaofikia kilele chake mwezi Julai 2022. Hili ni tukio ambalo limenogeshwa pia na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya Jimbo kuu la Mwanza pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Mwanza ulioanzishwa na Hayati Askofu mkuu Anthony Petro Mayala. Ukaendelezwa na Askofu mkuu Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi na sasa ni zamu ya Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande.

Kumbe, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza. “Shikome” ni neno la lugha ya Kisukuma lenye maana ya kikao cha kifamilia wakati wa jioni ambapo wanafamilia wa kiume huuzunguka moto ulio katikati na kushirikishana masuala mbalimbali ikiwemo kazi za siku, kujadiliana mipango ya familia, kushauriana na kuonyana, pamoja na kusimuliana hadithi za kale zenye lengo la kujenga na kufundishana. Hayati Askofu mkuu Anthony Petro Mayala alipenda kutumia neno na mfumo huo kwa maana ya kwamba ni mfumo wa kifamilia unaoakisi vema kielelezo cha Kanisa la Afrika kama familia ya Mungu inayojali na kuwajibika (Sura ya Sinodi ya kwanza ya Afrika na pia dira ya Sinodi ya Mwanza).  Ni mfumo wenye uhuru kwa wote katika kushirikishana, ni namna ya kuweka wazi shughuli zote za kifamilia na za kila mmoja kwa kutafuta ufumbuzi unaofaa kwa changamoto mamboleo au kwa kuzipyaisha na kuziboresha shughuli hizo, na ni namna ya kurekebishana kwa upendo wa kifamilia panapokuwa na mapungufu ya kibinadamu!

Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., ndiye aliyetoa mahubiri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Malkia wa Kawekamo, Jimbo kuu la Mwanza ambayo chimbuko lake ni tukio la kihistoria la Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kunako mwaka 1990. Tangu wakati huo Kawekamo imebaki kuwa "kumbukumbu hai" ya Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania ambaye ndiye aliyebariki Jiwe la Msingi wa Kanisa kuu Jimbo kuu la Mwanza. Askofu mkuu Dallu amefafanua awamu mbalimbali za Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo kilele chake ni Mwezi Oktoba 2023. Miaka miwili ya kuwasikiliza waamini walei. Mtendaji mkuu katika maadhimisho ya Sinodi ni Roho Mtakatifu! Katika Hotuba yake ya Ufunguzi, Jumamosi ya tarehe 9 Oktoba, 2021, Baba Mtakatifu alihimiza kuwa Mtendaji Mkuu wa Sinodi ni Roho Mtakatifu. Sinodi itazamwe siyo kama bunge na wala siyo utafiti wa maoni ya watu, bali ni Wasaa wa Kanisa.

Kama hakuna Roho Mtakatifu, hakutakuwa na Sinodi. Kwa hiyo, ni lazima kuiishi Sinodi kwa moyo wa sala. Ushirika, Umoja, Ushiriki na Umisionari, Utume! Katika kuelezea maneno msingi matatu katika Sinodi, yaani: Ushirika/Umoja (communion), Ushiriki (participation) na Utume (mission); Baba Mtakatifu Francisko anahimiza kuwa Ushirika na Umisionari vinatambulisha fumbo la Kanisa kulingana na Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tena ushirika na umisionari havikamiliki bila ushiriki. Aidha, Baba Mtakatifu anahimiza kuwa Sinodi zote lazima ziandaliwe vema, hususani katika ngazi ya Kanisa Mahalia likitoa nafasi kwa wote ili ziweze kuzaa matunda. Hatari tatu za kuepa na fursa tatu za kuchangamkia katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Kwa upande mmoja, Baba Mtakatifu Francisko anatahadharisha hatari za aina tatu zinazoweza kujitokeza, kama ifuatavyo:(1) Sinodi kuishia kuwa tukio nje nje la kinadharia: badala ya kuwa fursa ya kufanya tafakari na maazimio ya pamoja ya maisha ya Kanisa, kugeuka na kuwa nafasi ya kujitambulisha wenyewe (formalism); (2) Usomi-bandia (elitism / intellectualism): Iko hali inajitokeza baina ya mapadre ya kujiona kuwa ni wasomi na hivyo kushindwa kutoa nafasi ya kutosha kwa mijadala huru inayogusa mahitaji halisi ya kichungaji. (3) Mawazo mgando (complacency): ni matokeo ya kufanya mambo kwa mazoea na kutokuwa tayari kuruhusu mabadiliko.

Kwa upande mwingine, Baba Mtakatifu anaainisha fursa kuu tatu zinazotokana na Sinodi, ambazo ni: (1)Kutembea pamoja sio mara kadhaa tu bali kimfumo kabisa tukielekea kuwa Kanisa la Kisinodi. (2) Sinodi inatufanya pia tuwe Kanisa linalosikiliza. (3) Sinodi ni nafasi ya kuwa Kanisa lililo karibu zaidi na watu. Siyo kuunda Kanisa jingine bali Kanisa tofauti:Mwisho, Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha kwa kuhimiza tena juu ya nafasi ya Roho Mtakatifu kama Mtendaji Mkuu wa Sinodi. Tunaalikwa tumruhusu Roho huyo atende kazi yake, tumwite kwa nguvu zaidi na kumsikiliza kwa unyenyekevu na kuwa tayari kutembea pamoja naye, mwumbaji wa Ushirika na Umisionari. Kipindi chote cha Sinodi kijawe na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Barani Afrika ilikuwa ni AMECEA ambayo ilikuja na mpango mkakati madhubuti wa kuunda ‘Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo’. Kuanzia Mkutano Mkuu wa AMECEA wa mwaka 1973 Maaskofu walianza kusisitiza juu ya mpango wa kujikita kwenye Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Mwaka 1976 katika Mkutano Mkuu uliofanyika mjini Nairobi, Kenya Maaskofu walitangaza rasmi kwamba "Mfumo wa kuunda Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, ndio mkakati rasmi wa uinjilishaji katika Kanisa la Afrika ya Mashariki na utapewa kipaumbele katika miaka ijayo.” Tangu wakati huo Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zimekuwa agenda ya kudumu katika mikutano ya AMECEA. Katika azimio la mwaka 1992 kule Zambia walisema “ Jumuiya Ndogo ndogo sio za hiari katika kanisa, ila ni kitovu cha maisha ya Imani na utume wa uinjilishaji.” Hii ndiyo sababu katika kukaribisha mkutano mkuu wa Amecea Dar es Salaam mwaka 2002 katika kuadhimisha miaka 25 ya Jumuiya Ndogondogo, wajumbe walikaribishwa na mabango yaliyosema "Karibu AMECEA, Mama wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Askofu mkuu Damian Denis Dallu amekumbumbishia kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kunako mwaka 1986 wakati wa kumweka wakfu na kumsimika Hayati Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi, ilitangaza kwamba, mchakato wa Uinjilishaji katika nchi za Afrika Mashariki na Kati ni Jumuiya Ndogondogo za kikristo!

Mama Kanisa anapenda kuwekeza zaidi katika maisha na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa kwa kuwajengea uwezo ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ni Kanisa dogo mahalia la familia zinazopakana na jukumu lake hasa ni kusali pamoja, kusikiliza na kutafakari pamoja Neno la Mungu na kulieneza. Wanajumuiya wanahamasishana kuishi maisha ya Kikristo na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani yao. Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo msingi wake ni Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu ambavyo huwaimarisha katika Imani, Upendo na Matumaini katika umoja (Koinonia - Umoja), wakimshuhudia Kristo Yesu aliyefufuka na kumtangaza kama Mungu na Mwokozi ndiyo kiini cha imani (kerygma - Imani); na kushuhudia imani hiyo kwa huduma wanayotoa miongoni mwao wenyewe na kwa maskini (Diakonia - Utumishi). Mfumo huu uliingizwa katika mikakati yote ya uinjilishaji katika Kanisa la Afrika Mashariki na Kati. Kumbe, dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa nchi za AMECEA ni sawa na chanda na pete. Kwa upande wa Sekretarieti kuu ya AMECEA, iliwakilishwa na Padre Emmanuel Chimombo Mkurugenzi wa Idara ya Kichungaji, AMECEA.

AMECEA 2021

 

09 November 2021, 16:24