Tafuta

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, Jimbo Katoliki Iringa, tarehe 24 Oktoba 2021 imezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wao nchini Tanzania. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, Jimbo Katoliki Iringa, tarehe 24 Oktoba 2021 imezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Maisha na Utume wao nchini Tanzania. 

Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA: Maisha na Utume Wao!

Mama Evaline Malisa Ntenga katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu Siku ya 95 ya Umisionari Ulimwenguni, dhamana na wajibu wa walei. Anamwangalia Mtumishi wa Mungu Marie Pauline Jaricot, Mwamini Mlei kama mfano bora wa kuigwa katika sala na huduma. Mwishoni anagusia Matarajio yake kwa Kanisa la Tanzania katika mchakato wa kujitegemea!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, WAWATA TAIFA, -Iringa, Tanzania.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, jamii na Taifa kwa ujumla, pia wanawake wanakuwa na maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wa Yesu Kristo.

Askofu Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 amezindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA katika ngazi ya Kijimbo. Amewapongeza na kuwashukuru WAWATA kwa upendo, sadaka na uvumilivu katika maisha na utume wao. Mama Evaline Malisa Ntenga Mwenyekiti wa WANAWAKE wakatoliki Tanzania na mjumbe wa Bodi ya Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC., ameshiriki katika uzinduzi huu utakaofikia kilele chake hapo Mwezi Septemba 2022. Mama Evaline Malisa Ntenga katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia kuhusu Siku ya 95 ya Umisionari Ulimwenguni, dhamana na wajibu wa waamini walei kulitegemeza Kanisa. Anamwangalia Mtumishi wa Mungu Marie Pauline Jaricot, Mwamini Mlei kama mfano bora wa kuigwa katika sala na huduma. Mwishoni anagusia Matarajio yake kwa Kanisa la Tanzania katika mchakato wa kujitegemea! Tiketi ya kuwa mwanachama katika umoja huu ni UBATIZO.

Kwa njia ya ubatizo tulipokea hadhi ya kuwa wafalme,makuhani na manabii na hivyo tunaitwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sawa na Injili ya Marko Sura 16:15 Basi, akawaambia, "Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu. Wanawake Wakatoliki tumeitwa kuwa watakatifu ili kuyatakatifuza Malimwengu. Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa kutoa shukrani kwa Mungu kwa utume wetu toka ulipoanzishwa mwaka 1972 na kwa mwaka mzima hadi kilele hapo Mwezi Septemba 2022 ili tuweze kujitathimini kuhusu nafasi na utume wetu katika Kanisa na jamii. Ni muda wa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa yale ambayo ama kwa uzembe ama kwa bahati mbaya tumeshindwa kuyatekeleza kama wanawake wakatoliki! Ni muda wa kuomba neema na baraka ya kuweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, tukijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa maongozi ya Roho Mtakatifu.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Mhasham Baba Askofu katika mahubiri yake ametukumbusha kutoa kwa Ukarimu. Katika maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni napenda kuchukua fursa hii kumwalika kila Mbatizwa atafakari wito wake wa kimisionari kama mbatizwa. Rej. Luka 4:18 “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao, na vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa.

Mtumishi wa Mungu Marie Pauline Jaricot, Mwamini Mlei. Tunaposali kuombea utume wa Kanisa tunafurahi kuwa Mwanzilishi wa Shirika la Uenezaji Injili, Pauline Jaricot, atatangazwa kuwa Mwenye Heri hapo tarehe 22 Mei 2022, huko Lyon, Ufaransa, katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya kuanzishwa kwa Shirika la Uenezaji wa Imani. Maadhimisho haya yatafanyika katika Ibada ya Misa takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Kardinali Luis Antonio Tagle Rais wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Mtumishi wa Mungu Pauline Marie Jaricot ni mfano kwetu wa maisha ya sala na Ibada kwa Ekaristi takatifu. Zaidi ya hayo, yeye ni mfano wa roho ya umisionari. Tuliombee tukio hilo muhimu katika historia ya umisionari linasema Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Mtumishi wa Mungu Marie Pauline Jaricot, akiwa mdogo alikuwa na mazoea ya kutembelea Ekaristi Takatifu, mazoea ambayo yalimruhusu kuwa karibu na Mungu na hivyo kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu katika maisha yake. Mwaka 1819, baada ya kujua mateso waliyokuwa wanayapata wamisionari, aliamua kuwasiliana na wamisionari kujua mahitaji yao. Kwa hiyo akaamua kuwaombea na kuwasaidia kwa vitu mbalimbali. Pauline Marie Jaricot alikuwa na karama ya pekee ya kimisionari,  ambayo  iliyofanya izaliwe  Rosari hai  iliyo chini ya Shirika la Uenezaji wa Imani.  Akiwa na miaka ishirini (20) pamoja na marafiki zake walianzisha mfuko wa kusaidia wamisionari, ambao Pauline aliuita mchango huo “senti ya Pauline”  Mchango huo ulilenga kusaidia wamisionari ambao waliishi katika kifungo cha kutangaza Habari Njema kwa sehemu  za pembezoni mwa jamii.

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu litaadhimisha miaka 400 ifikapo mwaka 2022. Baraza ilianzishwa na Papa Gregori wa Kumi na Tano tarehe 22 Juni mwaka 1622 kwa Waraka wa “Inscrutabili Divinae.” Tangu kuanzishwa kwake Baraza hili la Kipapa limejulikana kama Baraza la Kipapa la Uenezaji wa Injili (Sacra Congregatio de Propaganda Fide). Mtakatifu Paulo VI aliiunda upya mwaka 1967 na kuiita Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ambayo yako chini ya Baraza hili yameenea katika nchi 130 Ulimwengu ambako yanawahudumia wamisionari 354,000, makatekista milioni 3 na majimbo 114 katika maeneo ya kimisionari. Rej. 2 Kor 9:6-15 “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele."

Matarajio yangu kwa Kanisa la Tanzania: Kuona watu wa Mungu wakijitahidi kulitegemeza Kanisa mahalia kwa rasilimali watu, watakaojisadaka kwa ajili ya kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Tanzania yaani kuwa na Maaskofu, Mapadre, Watawa, Makatekista na Waamini walei watakaoliongoza Kanisa la Kristo. Natamani kuona Kanisa la Tanzania likiendelea kujizatiti zaidi katika kujitegemea, kwa kuitegemeza Mihimili ya Injili, ili iweze kutekeleza vyema wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa. Natamani kuwaona waamini walei wakishiriki zaidi katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu, ili Tanzania, Afrika na Ulimwengu katika ujumla wake, uwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya Habari Njema ya Wokovu!

WAWATA Tanzania
26 October 2021, 16:24