Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa: Utambulisho wa Kristo Yesu: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao ukombozi na maisha ya uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa: Utambulisho wa Kristo Yesu: Mateso, Kifo na Ufufuko uletao ukombozi na maisha ya uzima wa milele! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 29: Ubatizo na Kikombe Cha Yesu!

Kiini cha ujumbe wa Injili kwa Dominika ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa kimelala katika sentensi ifuatayo: “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45. Huu ndio utambulisho unaotolewa na Yesu mwenyewe kama ulivyosimuliwa pia katika Somo la kwanza na Nabii Isaya 53:10-11. Yesu ni Kuhani mkuu wa Agano Jipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 29 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa. Leo Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu ambayo ningependa kuyagusia kidogo tu! Uzinduzi wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ngazi ya kijimbo. Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka wakfu Maaskofu wawiili walioteuliwa hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 10 Oktoba 2021 alizindua rasmi Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya yamegawanyika katika awamu kuu tatu kuanzia Mwezi Oktoba 2021 hadi Oktoba 2023. Awamu ya kwanza ni kwa ajili ya Makanisa mahalia pamoja na taasisi zote zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki ni kuanzia tarehe 10 Mwezi Oktoba 2021 hadi Aprili 2022.

Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023. Awamu ya Tatu, Kanisa la Kiulimwengu ni kuanzia mwezi Oktoba 2023. Baba Mtakatifu anakazia ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kukutana na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho, ili kweli maadhimisho ya Sinodi yaweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Hili ni tukio la neema na mchakato wa uponyaji unaotekelezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kristo Yesu anawataka waamini kutomezwa na malimwengu; kuwa wazi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kuondokana na tabia ya kutekeleza shughuli za kichungaji kwa mazoea, ili hatimaye, kutambua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake katika nyakati hizi na wapi anataka kulipeleka.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 17 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Uhusiano na mafungamano ya Kristo Yesu na wafuasi wake na binadamu katika ujumla wake, yamewawezesha kufunuliwa Injili na Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka kielelezo cha ushuhuda wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anagusia uzoefu wa Mitume wa Yesu wanaoshuhudia upendo, huruma na msamaha ulioneshwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Anaelezea matatizo na changamoto zilizojitokeza kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo katika mwanzo wa safari yao ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo hii, walimwengu wanakabiliwa na changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu aliyefufuka na kutukuzwa ndiye chemchemi ya matumaini ya waja wake. Katika mchakato wa uinjilishaji, Wakristo wanahamasishwa pia kulinda na kutunza mazingira. Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha, mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo vya uinjilishaji. 

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi cha dominika kadhaa, Liturujia ya Neno la Mungu imetupatia nafasi ya kutafakari umuhimu wa ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Kashfa ya Fumbo la Msalaba na kwamba, mali na utajiri wa dunia hii visiwe ni kikwazo vya kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Yote haya ni ufafanuzi wa Neno la Mungu mintarafu ukweli wa maisha ya mwanadamu. Hiki ni kiini cha ufunguo wa ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu. Lengo ni kuwawezesha waamini kukuza na kuimarisha: imani, matumaini na mapendo. Watambue kwamba, Maandiko Matakatifu ni kiini cha ukweli mfunuliwa kuhusu mpango wa Mungu kwa kujitahidi kumfahamu Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Na kwa njia hii, waamini wanapata nafasi ya kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo.

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa inatuletea sehemu muhimu sana ya utambulisho wa Kristo Yesu. Injili kama ilivyoandikwa na Marko 10:25-45 imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni ombi la Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo wanaotaka mmoja wao akae kushoto na mwingine kulia katika Ufalme wa Mungu. Kwa maneno mengine, Mitume hawa wanataka nafasi ya juu kabisa katika Ufalme wa Mungu, kiasi kwamba wako tayari kubatizwa Ubatizo wa Yesu yaani: kuteseka, kufa na kufufuka kwa wafu na kukinywea kikombe chake cha: baraka, mateso na shukrani kama yalivyokuwa kadiri ya mapokeo ya Agano la Kale. Mama Kanisa daima anawakumbusha watoto wake kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma makini kwa watu wa Mungu.

Kiini cha ujumbe wa Injili kwa Dominika ya 29 ya Mwaka B wa Kanisa kimelala katika sentensi ifuatayo: “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45. Huu ndio utambulisho unaotolewa na Kristo Yesu mwenyewe kama ulivyosimuliwa pia katika Somo la kwanza na Nabii Isaya 53:10-11. Nabii Isaya anamtumbulisha Mtumishi mwaminifu wa Mungu; mtu wa mateso na huzuni nyingi, mtu mwenye haki ambaye atawafanya wengi kuwa wenye haki. Huyu ni Mtumishi wa Mungu ambaye amejisadaka kwa ajili ya huduma na hivyo kubahatika kutangaza na kushuhudia ukweli wa Kimungu kwa mateso, kifo na ufufuko wake amewafanya wengi kuwa wenye haki na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mateso ya Kristo Yesu ni chemchemi na mwanga wa ukombozi.

Sehemu hii ya Injili inaonesha mabadiliko makubwa yaliyoletwa na Kristo Yesu mintarafu dhana ya Masiha, kinyume kabisa na jinsi ilivyofahamika. Waisraeli walimngoja Masiha mwenye nguvu za kijeshi, kisiasa na kiroho. Na dhana hii ndiyo chimbuko la mawazo ya Mtakatifu Petro Mtume, Yakobo na Yohane, Wana wa Zebedayo. Kristo Yesu alipenda kujitambulisha kama Mwana wa Adamu. Siku moja aliwauliza Je, watu wanasema Mwana wa Mtu ni nani? Yesu anawaletea mabadiliko kwa kuwatangazia hatima ya Masiha wa Mungu! Anatangaza mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu. Ni Masiha aliyejenga Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake, katika hali ya unyenyekevu. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45.

Hii ndiyo Hekima ya Mungu iliyofunuliwa na Kristo Yesu pale juu Msalabani. Kristo Yesu ni Masiha na Mtumishi wa Bwana mteseka. Kashfa ya Fumbo la Msalaba inaweza kupokelewa kwa imani kwa maana Kristo Yesu ni nguvu na hekima ya Mungu. Rej. 1Kor.1:23. Hata katika ulimwengu mamboleo bado kuna mateso, kilio na ugumu wa maisha. Kuna janga la ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, njaa na magonjwa. Somo la Pili kutoka Waraka kwa Waebrania 4:14-16 linamwonesha Kristo Yesu, Kuhani mkuu aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa wafu. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Liturujia J29
16 October 2021, 14:56