Tafuta

Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi ni Kitovu cha Uinjilishaji wa Kina, Mahali ya kuadhimisha: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi ni Kitovu cha Uinjilishaji wa Kina, Mahali ya kuadhimisha: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Parokia ya Mt. Yosefu Mfanyakazi Morogoro: Uinjilishaji wa Kina!

Askofu Lazarus Msimbe, wa Jimbo Katoliki Morogoro, hivi karibuni amezindua Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi iliyopo eneo la Mkundi, Jimbo Katoliki la Morogoro, sanjari na kuwaimarisha Wakristo 116 kwa Sakramenti ya Kipaimara. Parokia hii imezinduliwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kuanzia tarehe 8 Desemba 2020 hadi 8 Desemba 2021.

Na Angela Kibwana Morogoro na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., -Vatican.

Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” uliochapishwa tarehe 29 Juni 2020 unapania kupyaisha ari na mwamko wa wito na utume wa kimisionari katika Kanisa. Unakazia umuhimu wa Parokia kama kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Parokia, ni mahali ambapo maisha ya Kisakramenti yanapewa uzito wa pekee sanjari na ushuhuda wa upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji. Parokia ni mahali ambapo, utamaduni wa watu kukutana unapaswa kujengwa na kudumishwa, ili kukoleza majadiliano ya: kitamaduni, kidini na kiekumene; mshikamano pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa ajili ya watu wote. Hapa ni mahali muafaka pa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kukutana, kusikiliza na hatimaye, kufanya mang’amuzi ya pamoja!

Jumuiya ya Kiparokia inapaswa kuwa ni wasanii wa utamaduni wa ujirani mwema, kama kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa kwa namna ya pekee katika Injili ya huduma. Pamoja na ukweli huu, Mama Kanisa anatambua kwamba, kuna uhaba mkubwa wa miito ya Kipadre katika baadhi ya maeneo, kiasi kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache katika shamba la Bwana. Kumbe, kuna haja ya kuwa na mwelekeo na utambuzi mpya wa “dhana ya Parokia”. Parokia ni mahali muafaka pa waamini kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara.

Ni wakati wa kutumia rasilimali muda na uwepo kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kwa kuthamini familia kama shule ya kwanza ya uinjilishaji, huruma na upendo. Hapa ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Wote wanaitwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani unaofumbatwa katika ari na mwamko wa kimisionari!

Ni katika muktadha huu, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro, hivi karibuni amezindua Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi iliyopo eneo la Mkundi, Jimbo Katoliki la Morogoro, sanjari na kuwaimarisha Wakristo 116 kwa Sakramenti ya Kipaimara. Parokia hii imezinduliwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Mtakatifu Yosefu kuanzia tarehe 8 Desemba 2020 hadi 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi katika maisha.

Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Mtakatifu Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika katika ndoto. Lengo la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu Yosefu anasema Baba Mtakatifu, ni kuwasaidia waamini kumfahamu na kumpenda Mtakatifu Yosefu aliyekuwa na mang’amuzi ya kibinadamu kama walivyo waamini wengi duniani. Ni Mtakatifu ambaye hakushtushwa sana na mambo, hakuwa na karama maalum wala kati ya watu wa nyakati zake, hakuwa mtu mashuhuri. Na wala Maandiko Matakatifu hayaoneshi maneno yaliyotoka kinywani mwake hata kidogo, lakini machoni pa Mwenyezi Mungu, aliweza kutenda matendo makuuu katika maisha na utume wake.

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe amewasihi waamini kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda wa maisha yao adili na matakatifu pamoja na kuwajibika kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni pamoja kutoa sadaka na kulipa zaka kama sehemu ya mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa mahalia. Wajibu wa kutoa sadaka na kulipa zake, uwe ni utamaduni na vinasaba vya waamini kama sehemu ya ushiriki wao katika utume wa Kanisa. Askofu Msimbe amemteua Padre Cyprian Mvanda wa Shirika la Wamisionari wa Consolata, IMC kuwa Msimamizi wa Parokia hadi hapo Paroko atakapoteuliwa rasmi.

Amemshukuru na kumpongeza pia Padre Oktavian Msimbe, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Monika ambaye pia ni Dekano wa Dekania ya Morogoro mjini ambaye kwa muda mrefu amesimamia ujenzi wa Kigango hiki na hadi sasa kimekuwa ni Parokia rasmi. Amewashukuru pia wamisionari wa Consolata kwa ari na mwamko wa kimisionari waliounesha katika huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu Parokiani hapo. Changamoto kubwa mbele yao kwa sasa ni kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mapadre na kuanza mchakato wa ujenzi wa Kanisa litakalokidhi mahitaji ya watu wa Mungu kwa wakati huu. Lakini kabla ya kuanza ujenzi wa Kanisa kama jengo, Wakristo wajenge na kuimarisha maisha yao katika: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma. Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi ilianza kama Jumuiya ndogo ndogo ya Kikristo kunako mwaka 1973. Hadi kufikia Mwezi Oktoba 2021 ina jumla ya Jumuiya 58 na Vigango 3 na waamini wabatizwa 4, 150, wanaosimamiwa na kuongozwa na Mapadre wamisionari wa Shirika la Consolata.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Padre Erasto Mgalama, Mkuu wa Shirika la Waconsolata Kanda ya Tanzania, ambaye amewahi kutoa huduma ya kimisionari Parokiani hapo, amemshukuru na kumpongeza Askofu Lazarus Vitalis Msimbe kwa kuweka historia na kuwa ni Parokia ya kwanza kuzinduliwa naye tangu alipowekwa wakfu wa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Morogoro kama Askofu Jimbo. Amewataka waamini kuendeleza umoja, ushirikiano na upendo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Parokiani hapo. Wakati huo huo, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. wa Jimbo Katoliki Morogoro ametangaza kwamba, tarehe 18 Novemba 2021 itakuwa ni Siku ya Tegemeza Jimbo la Morogoro. Watu wa Mungu kutoka katika Parokia mbalimbali za Jimbo la Morogoro wakiwa wameambatana na Mapadre wao, watafika kwenye Uwanja, “wenyewe wanauita Mkeka” wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro kwa Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa mchango wao kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu kama sehemu ya mchakato wa kulitegemeza Kanisa ili liendelee kutoa huduma stahiki kwa watu wa Mungu!  

Parokia
20 October 2021, 15:28