Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni. Kauli mbiu "Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia" Mdo 4:20. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania 

Maaskofu Katoliki Tanzania Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni 2021

TEC: Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Pongezi kwa Ndugu Wakapuchini Kanda ya Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Uinjilishaji. Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mwaka 2022, Kutangazwa kuwa Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, Muasisi wa Shirika la Uenezaji wa Imani na Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu.

Na Askofu mkuu Damian Denis Dallu, Mwenyekiti Tume ya Uinjilishaji, - DSM.

Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Uinjilishaji, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ametoa ujumbe katika Maadhimisho ya Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2021 yananogeshwa na kauli mbiu: “Sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Mdo 4:20. Katika ujumbe huu, anaelezea kwa muhtasari Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 95 ya Kimisionari Ulimwenguni, Pongezi kwa Ndugu Wakapuchini Kanda ya Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Uinjilishaji yaani kuanzia Mwaka 1921 hadi mwaka 2021. Anagusia pia maandalizi ya Jubilei ya Miaka 400 ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu hapo mwaka 2022, Kutangazwa kuwa Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, Muasisi wa Shirika la Uenezaji wa Imani sanjari na Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayoongozwa na kauli mbiu: Ushirika/Umoja, Ushiriki na Utume au Umisionari!

UTANGULIZI: Mwaka huu katika nafasi ya Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni Baba Mtakatifu Francisko anatualika kuwa tunapopata nguvu ya upendo wa Mungu, na kutambua uwepo wake kama Baba katika maisha yetu ya binafsi na ya jamii, hatuwezi kuacha kutangaza na kushirikisha yale tuliyoyaona na kuyasikia. Uhusiano wa Yesu na wanafunzi wake na ubinadamu wake, kama ulivyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, katika Injili yake na katika Pasaka yake, hutuonesha kwa kiwango gani Mungu anaupenda ubinadamu wetu (taz. Gaudium et spes, 22). Kila kitu kuhusu Kristo kinatukumbusha kwamba Yeye anaufahamu vema ulimwengu wetu na hitaji lake la ukombozi, na anatuita kushiriki kikamilifu katika utume huu: “enendeni hata njia panda za barabara, na wote muwaonao waiteni arusini” (Mt 22:9). 

Uzoefu wa Mitume: Uinjilishaji unaanza na Bwana mwenyewe anayewaita mitume baada ya kuongea nao, kila mmoja peke yake (taz. Yn 15:12-17). Mitume hao walikuwa wa kwanza kushuhudia upendo wa Bwana, siyo tu katika mafundisho yake, bali pia katika matendo na maisha yake, ambayo yalipendekeza maisha ya HERI na yalikuwa kama mafundisho yenye mamlaka na ya namna mpya iliyoamsha mshangao, furaha na shukrani. Nasi kwa imani yetu kwa Kristo tumeona, tumesikia na tumeguswa hivi kwamba mambo yanaweza kuwa tofauti. Tutambue kwamba “tuliumbwa kwa ajili ya utimilifu ambao unapatikana katika upendo” (Fratelli tutti, 68).  Tunaalikwa kuwaiga wakristo wa kwanza walioishi imani yao katika mazingira magumu sana, wakisongwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kutengwa na jamii, kufungwa gerezani na kuwa na mahangaiko mengine ya ndani na nje. Wakristo hao waliichukulia hali hiyo ngumu kuwa ni fursa kwa ajili ya utume.

Sisi leo pia tunakutana na changamoto katika utume wetu. Janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kwa mfano, limeongeza maumivu, upweke, umaskini, na dhuluma. Pia limetufanya tuvunjike moyo, tukose furaha, tuwe wachovu. Yote hayo tumkabidhi Kristo Mfufuka. Tahadhari dhidi ya ugonjwa huu isitufanye tuhalalishe hali ya kutojaliana, kunyanyapaana; utengano mzuri wa kijamii (social distance) utupeleke kwenye utume wa huruma, na yote hayo yawe ni fursa ya kukutana, kujaliana na kuinuana. Katika yote hayo tuongozwe na Neno la Bwana, ambalo litatuelekeza kwenye ukweli. Nasi leo tunaweza kusema pamoja na Mitume: “Hatuwezi kukaa kimya juu ya yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo. 4:20). Mwaliko kwa kila mmoja wetu Kaulimbiu ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni mwaka huu 2021 ni: “Hatuwezi kukaa kimya juu ya yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo. 4:20) ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kukitunza na kuwashirikisha wengine kile tulichokibeba moyoni mwetu. Huo ndio wito wa Kanisa, ambalo lipo ili kuinjilisha (Rej. Paulo VI, Evangelii Nuntiandi, 14). Tunaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko kwamba tuwakumbuke kwa shukrani Wamisionari wote, ambao kwa ushuhuda wa maisha yao wametusaidia kupyaisha ahadi zetu za Ubatizo na wametuvuta tuwe mitume wakarimu na wenye furaha ya Injili. Tusichoke kuomba ili “Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake” (Lk 10:2).

PONGEZI KWA NDUGU WAKAPUCHINI KANDA YA TANZANIA KWA KUADHIMISHA JUBILEI YA MIAKA 100 YA UINJILISHAJI (1921-2021)

Watawa Wakapuchini ni sehemu ya Watawa Wafrancisko waliodhamiria toka mwanzoni mwa karne ya kumi na sita kuyaiga maisha ya Mtakatifu Francisko kwa undani zaidi. Vazi lao lenye kofia ndefu inayoitwa “kapuchi” (kwa kiitaliano: capucino) ni chanzo cha jina lao Wakapuchini. Msingi wa maisha yao ni kutumikia kama Kristo aliyekubali kutoa uhai wake kwa faida ya wengi (Rej. Mt 20:28). Wakapuchini wanafanya utume wao wakijikita katika sala na katika kuwa wajumbe wa amani. Tamaa yao kubwa ni kupenda kuliko kupendwa, na kutoa kuliko kupokea. Kwa sasa, watawa wa shirika hili wapo katika nchi zaidi ya 100 wakitekeleza utume wao. Kwa Tanzania wapo karibu 250, na uwepo wao ulianza mwaka 1921, baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Walifika Tanzania kuchukua nafasi ya Wabenediktini kutoka Ujerumani ambao mazingira hayakuwaruhusu kuendelea kuwepo Tanzania kwa utume. Ofisi kuu ya Idara ya Uinjilishaji wa Watu iliwatuma Wamisionari kutoka Uswisi, taifa ambalo halikujihusisha na Vita ya Kwanza ya Dunia. Wakapuchini ni watawa waliokuwa na imani thabiti, ujuzi, vipaji, juhudi, nia njema na ari ya maendeleo. Waliingia Tanzania tarehe 18 Juni 1921. Makazi yao ya kwanza yalikuwa katika Misioni ya Mtakatifu Yosefu Dar es Salaam. Baadaye, baadhi yao walisonga mbele na kufika Kwiro, Mahenge tarehe 30 Julai 1921, siku ambayo walikabidhiwa kuiongoza Vikarieti ya Dar es Salaam, iliyojumuisha maeneo ya Dar es Salaam, Mahenge, Ifakara na Misioni ya Kipatimu, huko Kilwa. Kwa sasa Wamisionari hao wakapuchini wanafanya utume katika majimbo 14 yakiwemo majimbo makuu ya Dar es Salaam, Songea, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma. Majimbo mengine ni Ifakara, Mahenge, Morogoro, Moshi, Mbulu, Musoma, Kahama na Tanga. Tunawapongeza sana na tunawaombea Baraka za Mungu.

MIAKA 400 YA BARAZA LA KIPAPA LA UINJILISHAJI WA WATU

Mwaka 2022 tutaadhimisha Jubilei ya Miaka mia nne ya kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, mojawapo wa Mabaraza kumi na mbili ya Sekretarieti kuu ya Vatican. Kwa wakati huu, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kutoka Ufilipini. Katibu wake Mkuu ni Askofu Mkuu Protase Rugambwa, aliyewahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma (2008-2012), na baadaye akateuliwa kuwa Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa. Baraza hili litaadhimisha miaka 400 ifikapo mwaka 2022. Baraza ilianzishwa na Papa Gregori wa Kumi na Tano tarehe 22 Juni mwaka 1622 kwa Waraka wa “Inscrutabili Divinae.” Tangu kuanzishwa kwake Baraza hili la Kipapa limejulikana kama Baraza la Kipapa la Uenezaji wa Injili (Sacra Congregatio de Propaganda Fide). Mtakatifu Paulo VI aliiunda upya mwaka 1967 na kuiita Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

KUTANGAZWA MWENYE HERI MTUMISHI WA MUNGU PAULINE MARIE JARICOT, MWANZILISHI WA SHIRIKA LA KIPAPA LA UENEZAJI WA IMANI, MEI 2022

Tunaposali kuombea utume wa Kanisa tunafurahi kuwa Mwanzilishi wa Shirika la Uenezaji Injili, Pauline Jaricot, atatangazwa kuwa Mwenye Heri hapo tarehe 22 Mei 2022, huko Lyon, Ufaransa, katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 ya kuanzishwa kwa Shirika la Uenezaji wa Imani. Tangazo hilo litafanyika katika adhimisho la Misa takatifu itakayoongozwa na Kardinali Luis Antonio Tagle. Pauline Marie Jaricot ni mfano kwetu wa maisha ya sala na Ibada kwa Ekaristi takatifu. Zaidi ya hayo, yeye ni mfano wa roho ya umisionari. Tuliombee tukio hilo muhimu katika historia ya umisionari.

SINODI YA XVI YA MAASKOFU: OKTOBA 2021 HADI OKTOBA 2023: Ushirika/Umoja! Ushiriki! Utume/Umisionari

Utangulizi: Siku ya Dominika ya tarehe 10 Oktoba, 2021 Baba Mtakatifu Francisko alifungua rasmi SINODI YA MAASKOFU yenye kuongozwa na Mada Kuu inayosema:“Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Ushirika, Ushiriki na Umisionari” Kwa kifupi inaweza kutambulika kuwa ni “Sinodi juu ya Usinodi”(A Synod on Synodality). Aidha, neno USINODI (synodality) linamaanisha kutembea pamoja na kusikilizana sisi kwa sisi na hasa kumsikiliza Roho Mtakatifu. Hii itakuwa ni Sinodi ya 16 ya Maaskofu katika historia ya Kanisa, na itadumu kwa kipindi cha miaka miwili, yaani kuanzia mwaka 2021 hadi 2023. Sinodi ya Pekee. Sinodi hii inategemewa kuwa ya pekee ukilinganisha na zile zilizopita. Inaanza na  kushirikisha waamini wote katika Makanisa Mahalia kokote ulimwenguni, na kuwasikiliza wote, hasa waamini walei. Ndiyo maana sinodi hii itadumu kwa miaka miwili tangu tarehe 10 Oktoba, 2021 hadi Oktoba 2023. Hatua ya kusikiliza maoni ya waamini kwa ngazi ya majimbo itadumu hadi Aprili 2022 na kufuatiwa na ngazi ya mabara tangu Septemba 2022 hadi Machi 2023. Hatua ya mwisho ya kiulimwengu itafikia ukomo wake katika mtindo ule asilia wa Kanisa wa Sinodi ya Maaskofu mjini Vatican mwezi Oktoba 2023.

Roho Mtakatifu – Mtendaji Mkuu katika Sinodi. Katika Hotuba yake ya Ufunguzi, Jumamosi ya tarehe 9 Oktoba, 2021, Baba Mtakatifu alihimiza kuwa Mtendaji Mkuu wa Sinodi ni Roho Mtakatifu. Sinodi itazamwe siyo kama bunge na wala siyo utafiti wa maoni ya watu, bali ni Wasaa wa Kanisa. Kama hakuna Roho Mtakatifu, hakutakuwa na Sinodi. Kwa hiyo, ni lazima kuiishi Sinodi kwa moyo wa sala. Ushirika, Umoja, Ushiriki na Umisionari, Utume! Katika kuelezea maneno msingi matatu katika Sinodi, yaani: Ushirika/Umoja (communion), Ushiriki (participation) na Utume (mission); Baba Mtakatifu Francisko anahimiza kuwa Ushirika na Umisionari vinatambulisha fumbo la Kanisa kulingana na Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Tena ushirika na umisionari havikamiliki bila ushiriki. Aidha, Baba Mtakatifu anahimiza kuwa Sinodi zote lazima ziandaliwe vema, hususani katika ngazi ya Kanisa Mahalia likitoa nafasi kwa wote ili ziweze kuzaa matunda. 

Hatari tatu za kuepa na fursa tatu za kuchangamkia: Kwa upande mmoja, Baba Mtakatifu Francisko anatahadharisha hatari za aina tatu zinazoweza kujitokeza, kama ifuatavyo:(1) Sinodi kuishia kuwa tukio nje nje la kinadharia: badala ya kuwa fursa ya kufanya tafakari na maazimio ya pamoja ya maisha ya Kanisa, kugeuka na kuwa nafasi ya kujitambulisha wenyewe (formalism); (2) Usomi-bandia (elitism / intellectualism): Iko hali inajitokeza baina ya mapadre ya kujiona kuwa ni wasomi na hivyo kushindwa kutoa nafasi ya kutosha kwa mijadala huru inayogusa mahitaji halisi ya kichungaji. (3) Mawazo mgando (complacency): ni matokeo ya kufanya mambo kwa mazoea na kutokuwa tayari kuruhusu mabadiliko. Kwa upande mwingine, Baba Mtakatifu anaainisha fursa kuu tatu zinazotokana na Sinodi, ambazo ni: (1)Kutembea pamoja sio mara kadhaa tu bali kimfumo kabisa tukielekea kuwa Kanisa la Kisinodi. (2) Sinodi inatufanya pia tuwe Kanisa linalosikiliza. (3) Sinodi ni nafasi ya kuwa Kanisa lililo karibu zaidi na watu. Siyo kuunda Kanisa jingine bali Kanisa tofauti:Mwisho, Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha kwa kuhimiza tena juu ya nafasi ya Roho Mtakatifu kama Mtendaji Mkuu wa Sinodi. Tunaalikwa tumruhusu Roho huyo atende kazi yake, tumwite kwa nguvu zaidi na kumsikiliza kwa unyenyekevu na kuwa tayari kutembea pamoja naye, mwumbaji wa Ushirika na Umisionari. Kipindi chote cha sinodi kijawe na nguvu ya Roho Mtakatifu.

SHUKRANI NA MWALIKO: “Na sasa tunakushukuru, Ee Mungu wetu, na tunalisifu jina lako tukufu” (1Nya. 29:1). Kwa maneno hayo, tunapenda kumshukuru Mungu kwa kutulinda mwaka mzima, licha ya changamoto ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Yeye aliye mwingi wa huruma ametujalia Baraka zinazotuwezesha kuendelea kutoa ushuhuda kama mitume “kwa yale tuliyoyaona na kuyasikia” katika majimbo yetu. Tunamwomba aendelee kutuimarisha na kutusimamia katika utume wa mwaka ujao yaani 2022. Tunachukua nafasi hii kwa niaba ya Ofisi ya Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kutoa shukrani za dhati kwa ukarimu mlioutoa mwaka 2020 kwa ajili ya Uinjilishaji. Licha ya hali ngumu iliyosababishwa na changamoto za UVIKO-19, tumeweza kutoa ukarimu mzuri uliokwenda kwenye Mfuko wa Pamoja (Universal Solidarity Fund) wa Uinjilishaji. Asanteni sana. Tukumbuke kuwa “Apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu” (2Kor 9:6). Tunatoa shukrani za pekee kwa ukarimu kwa Majimbo, Parokia, Vyama vya kitume, Taasisi, Seminari Kuu na Ndogo, Mashirika ya Kitawa, Taasisi za Elimu, Familia, watu binafsi waliochangia kwa njia ya bahasha na simu; na watu wote wenye mapenzi mema, kwa ukarimu mkubwa mlioutoa mwaka 2020 katika Dominika ya Kimisionari.

Falsafa ya kushukuru ni kuomba tena! Hivyo, tunawaalika tena Majimbo, Parokia, Vyama vya kitume, Taasisi, Seminari Kuu na Ndogo, Familia, watu binafsi na wote wenye mapenzi mema kutoa ukarimu wenu ili kumsaidia Baba Mtakatifu katika mchakato wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu ametukumbusha kwamba hakuna mtu aliye maskini ambaye hawezi kuchangia chochote katika jumuiya, maana hata uwepo wa mtu ni mchango wa kutosha (World Mission Sunday, 2018). Michango yote iliyopelekwa Roma mwaka 2020, POSPA imeirudishwa huku kwa ajili ya baadhi ya Seminari zetu Ndogo hapa Tanzania. Hivyo, tunawaalika nyote kwa namna ya pekee kuongeza juhudi ili Kanisa letu la Tanzania liweze kuchangia kwa ukarimu zaidi ya kile tulichotoa mwaka 2020.

Maaskofu Tanzania
21 October 2021, 14:31