Wosia wa Padre Raymond Saba kwa familia ya Mungu nchini Tanzania: Katekesi makini  na endelevu sanjari na Utume wa familia. Wosia wa Padre Raymond Saba kwa familia ya Mungu nchini Tanzania: Katekesi makini na endelevu sanjari na Utume wa familia. 

Wosia wa Padre Raymond Saba: Katekesi Endelevu na Utume wa Familia!

Wosia wa Padre Raymond Saba kwa familia ya Mungu nchini Tanzania: Umuhimu wa Katekesi endelevu na fungamani ili kuimarisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Matakatifu pamoja na maisha ya Sala. Kanisa nchini Tanzania halina budi kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kuziokoa familia kutokana na majanga yaliyopo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Padre Raymond K. S. Saba wa Jimbo Katoliki la Kigoma, aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kati ya Mwezi Julai, 2013 hadi Juni 2018 amefariki dunia tarehe 3 Agosti 2021 akiwa anapatiwa matibabu huko “Rabininsia Memorial Hospital” iliyoko Jijini Dar es Salaam. Tangu wakati huo wote, familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Kigoma na Tanzania katika ujumla wake, imekuwa ikiomboleza kifo cha Padre Raymond Saba. Radio Vatican inapenda kukushirikisha wosia wa Padre Raymond Saba kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Mambo makuu mawili ya kuzingatia ni: Umuhimu wa Katekesi endelevu na fungamani ili kuimarisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Matakatifu pamoja na maisha ya Sala. Kanisa nchini Tanzania halina budi kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kuziokoa familia kutokana na “majanga yanayoendelea kuziandama kila kukicha!

Padre Raymond K. S. Saba kama sehemu ya wosia wake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania anafafanua kwa kusema kwamba, Katekesi endelevu na fungamani inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na chombo cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji mpya. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Huu ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.

Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama kiini cha Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Padre Raymond Saba anakaza kusema, Katekesi ni mafundisho ya imani katika hatua mbalimbali za maisha ya waamini. Mara nyingi Katekesi imetolewa kabla ya kupokea Sakramenti za Kanisa na baadaye, kukosa mwendelezo. Kumbe, kuna umuhimu wa kukazia Katekesi ya awali, endelevu na fungamani katika maisha na utume wa Kanisa.

Lengo ni kuwawezesha waamini kuzamisha katika undani wa maisha yao, mafundisho msingi ya imani. Programu ya Kikatekesi kwa ajili ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri za Mungu na Sala iwe ni endelevu katika Kanisa. Wakristo Wakatoliki wakiimarishwa katika mambo msingi yaliyobainishwa kwenye Katekesi, wataweza kuwa kweli ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na hivyo kutoshawishika kwa urahisi kukimbilia katika Madhehebu mengine ya Kikristo. Padre Raymond Saba anakaza kusema, huko wanatafuta miujiza ya: uponyaji, utajiri na mafanikio ya chapuchapu. Katekesi makini na endelevu inaweza kukabiliana na changamoto mamboleo kwa kuzipatia majibu muafaka. Anasema, “Mungu wetu si Mungu wa vitu vinavyoshikika tu. Bali imani ya kweli inakita mizizi yake katika maisha ya mtu, wenye uwezo au maskini; wakati wa raha na shida na hiki ni kielelezo makini cha Mkristo wa kweli asiyeyumbishwa katika imani na maadili yake! Katekesi isipopewa kipaumbele cha pekee, hapo udhaifu wa imani utaonekana mara moja!

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, inayowawezesha waamini kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Katekisimu hii imekwisha kutafsiriwa katika lugha mbali mbali duniani, ikiwemo pia na lugha ya Kiswahili, iliyochapishwa kunako mwaka 2000.  Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafumbata utajiri mkubwa wa: Maandiko Matakatifu, Mababa wa Kanisa, Mafundisho ya Mitaguso Mikuu, Mchango na mafundisho ya waalimu wa Kanisa, Watakatifu na viongozi wa Kanisa. Katekisimu iliidhinishwa rasmi kwa Waraka wa Papa Yohane II “Fidei depositum” yaani “Amana ya Imani” uliosindikiza kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, hapo tarehe 11 Oktoba 1992 na kuanza kutumika rasmi kama kitabu cha kufundishia: imani na maadili ya Kanisa Katoliki tarehe 15 Agosti 1997. Padre Raymond Saba anasikitika kusema kwamba, watu wengi hawajajitaabisha kusoma, kujifunza na kutafakari yale yaliyoandikwa kwenye Katekisimu hii. Hii ni amana na utajiri mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Katekisimu ambayo imeandaliwa kukidhi wigo mpana zaidi wa maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Padre Raymond Saba anasema wosia wake wa Pili kwa familia ya Mungu nchini Tanzania ni kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili zitambue na kuwajibika barabara, kama shuhuda na chombo cha uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda. Mababa wa Kanisa wanasema, Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii.

Padre Raymond Saba anakaza kusema, ikiwa kama familia ni imara, itaweza kuwa ni chombo cha kujiinjilisha na kuwainjilisha wengine. Msingi wake imara unabubujika kutoka katika Katekesi makini, endelevu na fungamani. Kumbe, kuna haja ya kuwa na Katekesi ya kifamilia, ili kuziwezesha familia kutambua dhamana na wajibu wake katika kufundisha imani, maadili na utu wema. Familia ziendelee kujikita katika maisha ya sala, imani, uvumilivu, umoja na upendo thabiti; kwa kuelekezana na kuchukuliana kwa upole, ili kuheshimiana na kuthaminiana! Kwa ufupi kabisa, Wosia wa Padre Raymond K. S. Saba wa Jimbo Katoliki la Kigoma, aliyewahi kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kati ya Mwezi Julai, 2013 hadi Juni 2018 amefariki dunia tarehe 3 Agosti 2021 ni Katekesi makini endelevu na fungamani sanjari na Kanisa kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili familia ziweze kujiinjilisha na kuwainjilisha wengine.

Huu ndio mwelekeo wa Kanisa la Kiulimwengu wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani, tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu” Furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1.

Pd Raymond Saba
09 August 2021, 14:23