2021.08.30 Bukoba,Tanzania:Misa kwa ajili ya kuwaombea marehemu maaskofu wa jimbo Katoliki Bukoba tangu 1892 - 2013 iliyoongozwa na Askofu Desiderius Rwoma wa jimbo hilo. 2021.08.30 Bukoba,Tanzania:Misa kwa ajili ya kuwaombea marehemu maaskofu wa jimbo Katoliki Bukoba tangu 1892 - 2013 iliyoongozwa na Askofu Desiderius Rwoma wa jimbo hilo. 

Tanzania:Ask.Rwoma aongoza misa kuombea maaskofu wa jimbo tangu 1892-2013!

Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba,Tanzania ameongoza misa kuwaombea maaskofu pia mapadri waliotumikia Kanisa tangu 1892-2013.Hawa ni Ask.Joseph Hirth,W.F(1892-1912),Ask.Joseph Sweens,W.F (1912-1929),Ask.Burchard Jubilee,W.F(1929-1948),Ask.Laurent Tetrault,W.F(1948-1952),Ask.Alfred Lanctot,W.F(1952-1960),Kard.Laurean Rugambwa,(1960-1969),Ask.Gervase Nkalanga,(1969-1974) na Ask.Nestor Timanywa,(1974-2013).

Na Sr. Angela Rwezaula–Vatican na Patrick P. Tibanga-Radio Mbiu,Kagera.

Wakristo wakatoliki wametakiwa kuwaombea, kuwakumbuka na kuwaenzi kwa vitendo maaskofu na mapadri waliolitumikia Kanisa pamoja na kuwasihi mapadri na viongozi wa Kanisa kuzitembelea familia za wakristo ili kuwaimarisha katika upendo wa sala. Wito huo umetolewa Jumapili tarehe 29 Agosti 2021 na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Desderius Rwoma wakati wa  mahubiri yake kwenye misa Takatifu maalum ya kuwaombea na kuwaenzi maaskofu walioongoza jimbo Katoliki  la Bukoba tangu mwaka 1892 - 2013.

Haya ni makaburi ya maaskofu wa Bukoba likiwemo hata la Kardinali Rugambwa
Haya ni makaburi ya maaskofu wa Bukoba likiwemo hata la Kardinali Rugambwa

Katika homilia yake Askofu Rwoma amesema kuwa, kila mkristo anatakiwa kuwaombea na kuwaenzi kwa kufufua na kuendeleza mashirika ya kitawa yenye historia ya jimbo la Bukoba na kuanzisha mashirika yenye historia ya utendaji wa kazi za kitume na kuimarisha vyama vya kitume vilivyokuwepo wakati wa maaskofu na kuwashukuru wanaoendeleza vyama vilivyoanzishwa na maaskofu hao.

Askofu Desiderius Rwoma mbele ya makaburi ya maaskofu wa jimbo la Bukoba
Askofu Desiderius Rwoma mbele ya makaburi ya maaskofu wa jimbo la Bukoba

Askofu Rwoma amehitimisha homilia yake kwa kuwataka mapadri na viongozi wa Kanisa kuzitembelea familia za wakristu ili kuwaimarisha katika upendo wa sala, Imani pamoja na kuwatia moyo katika maisha na kusonga mbele bila kurudi nyuma na kamwe wasije kuwasahahu maaskofu ambao hawakupata nafasi ya kuwaona, kwani walikuwa watu wa Imani na uvumlivu na kutimiza wajibu wa Imani katika mazingira magumu ikiwemo lugha, mira na desturi za kiafrika. Katika misa hiyo maaskofu walioombewa ni Askofu. Joseph Hirth, (White Fathers) (1892-1912), Askofu  Joseph Sweens, W.F (1912-1929), Askofu Burchard Jubilee, W. F (1929-1948), Askofu Laurent Tetrault, W.F (1948-1952), Askofu Alfred Lanctot, W. F (1952-1960), Kardinali  Laurean Rugambwa, (1960-1969), Askofu Gervase Nkalanga, (1969-1974), Askofu Nestor Timanywa, (1974-2013) na kwa sasa jimbo hilo linaongozwa na Askofu Desderius Rwoma akisaidiwa na Askofu Methodius Kilaini.

Askofu wa kwanza Joseph Hirth,(WF)

Askofu John Joseph Hirth alizaliwa manmo tarehe 26 Machi 1854 huko Spechbach-le-Bas (Niederspechbach), karibu na Altkirch huko Alsace. Wazazi wake walikuwa Jean Hirth, mwalimu, na Catherine Sauner. Hirth alikuwa hodari katika lugha ya Kifaransa na Kijerumani.  Baada ya shule ya msingi aliingia shule ya sekondari huko Altkirch, akasoma katika seminari ndogo za Lachapelle-sous-Rougemont na Zillisheim, na baadaye akahudhuria Chuo Kikuu cha Luxeuil-les-Bains. Baada ya Ujerumani kutwaliwa Alsace, alichagua uraia wa Ufaransa mnamo 1872, kwani alikataliwa kuwa na uraia wa nchi mbili. Alisomea taalimungu katika Seminari Kuu ya Nancy tangu 1873 hadi 1875, na baadaye akakubaliwa katika Shirika la Wamisionari  wa Afrika waitwao White Fathers kama novizi. Hirth alimaliza masomo yake ya kidini na kikuhani katika nyumba ya  Carrée, karibu na Algiers, nchini Algeria na  alifunga nadhiri kama mtawa wa shirika hilo mnamo tarehe 12 Oktoba 1876 na akapewa daraja la upadri mnamo tarehe 15 Septemba 1878.

Mnamo 1882 alifanywa kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa seminari ndogo ya Mtakatifu Anne huko Yerusalemu. Mnamo 1886, alichaguliwa kuwa Mkurugenzi wa seminari ndogo ya Mtakatifu Eugene huko Algiers. Hirth aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Teveste na Msimamzi wa Kitume wa Victoria Nyanza ya wakati huo na sasa ndlo Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza tarehe 4 Desemba 1889. Aliwekwa wakfu kuwa askofu tarehe 25 Mei 1890.  Eneo hili lilijumuisha sehemu za Uganda ya sasa, Rwanda, Burundi na kaskazini mwa Tanzania. Askofu Hirth aliweka lengo la kufanya maeneo yote  kuwa wakatoliki mwishoni mwa 1892, huku akiongoza shughuli za ujenzi wa makanisa na uhamasishaji wa Injili. Kwa miaka kadhaa alisafiri kupitia uwakilishi wake mkubwa huku akitembelea utume uliotawanyika. Wamisionari hao walilazimika kushughulika sana hasa mashindano kati ya watawala wa eneo hilo, ambao walikuwa wakifanya ushirika na nguvu za kikoloni za Ujerumani na Uingereza na wakati mwingine kuwa na uhasama kutoka kwa mamlaka ya kikoloni.

Uzinduzi wa jubilei ya miaka 100 ya Parokia ya Rutabo na kipaimara kwa watoto 530

Wazazi na walezi wameombwa kuwalea watoto katika maadili mema yanayompendeza Mungu na kuwafundisha kuipenda na kudumu katika imani na mafundisho ya kanisa  katoliki ili wawe mfano bora katika jamii. Wito huo umetolewa na Askofu Desderius Rwoma wa jimbo katoliki katika adhimisho la misa takatifu ya uzinduzi wa Jubilei ya miaka 100 ya Parokia ya Rutabo, tarehe 30 Agosti 2021. Katika fursa ya maadhimisho hayo, imetolewa hata sakramenti ya kipaimara kwa watoto 530 katika parokia hiyo. Katika mahubiri yake Askofu Rwoma amesema kuwa ni vema waimarishwa wakayaishi mapaji saba ya Roho Mtakatifu ili yapate kuwasaidia katika maisha yao na zaidi kumshirikisha Mungu kwa kila jambo wanalo litenda katika maisha yao ya kila siku. Aidha Askofu amewataka waimarishwa hao kuzingatia imani yao ikiwemo kuhudhuria maadhimisho ya misa mbalimbali na siku kuu zilizoamriwa  pamoja na kuzingatia sakramenti za kanisa ikiwemo sakramenti ya kitubio na kuwasihi waimarishwa kutovutwa na mali za ulimwengu na kukataa vishawishi vyote vya ulimwengu na kumpokea Roho Mtakatifu ili awaimarishe katika Imani.

KUOMBEA MAASKOFU NA JUBILEI PAROKIA RUTABO
30 August 2021, 15:40