Tafuta

Patriaki Bartholomeo wa kwanza waraka wa mshikamano na Italia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Patriaki Bartholomeo wa kwanza waraka wa mshikamano na Italia katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! 

Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Majanga ya Moto Nchini Italia 2021

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema: Ni wajibu wa watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete, kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kimaadili na kiimani katika muktadha wa mafungamano kati ya Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mwanadamu pamoja na Mazingira yenyewe. Huu ni wajibu wa wote kabisa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya imani kwa Wakristo inayofumbatwa katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu. Maisha na utume wa Kanisa unamwilishwa katika matukio mbalimbali yanayogusa na kumwambata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Taalimungu ya kiikolojia inagusa pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa kujizatiti katika kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa kutokana na uchafuzi wa mazingira ambao unaendelea kusababisha athari kubwa katika mabadiliko ya tabianchi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa kazi ya uumbaji mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mambo msingi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mazingira ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo imepewa nafasi ya pekee katika Liturujia Takatifu, hususan katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha muhtasari wa utimilifu wa nyakati.

Hii ndiyo karamu kuu inayodhihirisha utimilifu wa utukufu wa Ufalme wa Mungu. Hiki ndicho kilichokuwa kiini cha ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote, inayoadhimishwa na Kanisa la Kiorthodox, likiungana na Kanisa Katoliki kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 1 Septemba hadi kufikia kilele chake tarehe 4 Oktoba, 2019 Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kudumisha ukweli kuhusu utu na heshima ya binadamu pamoja na uelewa wa kazi ya uumbaji kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni katika muktadha huu pamoja na kuguswa na athari kubwa zilizosababishwa na janga la moto Kusini mwa Italia, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, amemwandikia Waraka wa Mshikamano Rais Sergio Mattarella wa Italia. Anasema, udhaifu wa mazingira asili ni matokeo ya uchaguzi mbaya wa sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Ni wajibu wa watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete, kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kimaadili na kiimani katika muktadha wa mahusiano na mafungamano kati ya Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mwanadamu pamoja na Mazingira yenyewe. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anaendelea kusema kwamba, kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya mazingira kama kazi ya uumbaji na binadamu ambaye amepewa dhamana ya kutunza, kulinda na kuyaendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Inasikitisha kuona matumizi mabaya ya mali na rasilimali za dunia na matokeo yake ni athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kujitokeza kila kukicha! Ni matumaini ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwamba, janga la moto lililojitokeza hivi karibuni nchini Italia, litapewa ufumbuzi wa kudumu. Anawaombea kwa Mwenyezi Mungu wafanyakazi wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuzuia na kuzima moto unaoendelea kujitokeza sehemu mbalimbali za Italia kutokana na kuongezeka kiwango cha joto pamoja na hujuma zinazofanywa na baadhi ya watu kwa kuchoma moto misitu!

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI limeonesha masikitiko yake makuu pamoja na ukaribu kwa watu wote walioathirika kwa janga la moto uliojitokeza hivi karibuni na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao; pamoja na uharibifu wa miundo mbinu. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwamba, wahusika watasakwa, ili hatimaye, watiwe pingu, ili sheria iweze kushika mkondo wake. Kwa sababu hawa ni watu wanaotishia: maisha, usalama na mafungamano ya kijamii pamoja na mazingira nyumba ya wote. Wananchi wa Italia wanapaswa kutambua kwamba, mazingira nyumba ya wote ni sawa na bustani nzuri ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu kuitumia kadiri ya Mpango wa Mungu. Maaskofu Katoliki Italia, wanawaomba wanasiasa na watunga sera kuhakikisha kwamba, wanaibua sera na mikakati itakayosaidia mapambano dhidi ya majanga ya moto nchini Italia.

Janga la Moto

 

01 August 2021, 14:57