Moja ya Ndege ya kijeshi katika harakati za kuwachukua watu kutoka Kabul Moja ya Ndege ya kijeshi katika harakati za kuwachukua watu kutoka Kabul 

Afghanistan:WCC,sala kwa watu wa Afghanistan kutokana na hofu ya vurugu

Baraza la Makanisa ulimwenguni,linawaombea watu wa Afghanistan kutokana na kukua kwa hofu ya vurugu kwa sababu ya Wataleban kuiweka mikononi mwao nchi hiyo.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC), Marianne Ejdersten, kwa niaba ya Mchungaji Ioan Sauca, katibu mkuu wa WCC amethibitisha kuwa "Watu ambao tayari wameteseka kwa miongo kadhaa kutokana na vita vya kijeshi, makazi yao, ukandamizaji, ufisadi na utawala mbaya wametupwa kwa hofu na kutokuwa na uhakika kwa sababu vurugu kubwa za siku za hivi karibuni. Tunawaombea hasa wanawake na wasichana wa Afghanistan, ili hadhi yao, haki na matakwa yao yasinyimwe tena, lakini wapate fursa ya kupata elimu na haki na uhuru ambao umeahidiwa na wale walio madarakani na Jumuiya ya kimataifa”. Ni kutokana na hali halisi iliyo nchini humo mara baada ya nchi hiyo kuwekwa mikononi mwa utawala wa Watalebani, ambapo katika nchi hiyo hofu na mashaka mengi yametanda na kusababisha wengi kuanza kuikimbia nchi hiyo. Bi Ejdersten akiendelea katika taarifa hiyo amesisitiza kwamba “Wataliban lazima waheshimu hadhi na utu na haki za watu wote katika maeneo wanayodhibiti sasa. Na tunatoa wito kwa mamlaka zote zenye uwezo nchini Afghanistan na kwingineko kuhakikisha usalama wa watu wote wa Afghanistan, pamoja na wale wanaokimbia nchi hiyo kwa kuogopa ghasia, dhuluma na mateso”.

Ndege za kijeshi zinazowabeba wanadiplomasia kuanza tena

Hata hivyo inasadika kuwa ndege za kijeshi zinazowabeba wanadiplomasia na raia kutoka Afghanistan zimeanza tena safari zake mapema Jumanne 17 Agosti 2021, siku moja baada ya maelfu ya watu kuvamia uwanja wa ndege wa Kabul kwa matumaini ya kukimbia nchi hiyo.  Wanajeshi wa Marekani walijaribu kutawanya umati huo kwa kufyatua risasi huku wengi wao wakijaribu kuning'inia katika ndege ya kijeshi ya Marekani wakati ikianza kuondoka. Hali hiyo ilisababisha safari za ndege kusitishwa Jumatatu. Ripoti nyingine za vyombo vya habari zinasema kuwa watu wawili walianguka kutoka pembeni mwa ndege hiyo baada ya kupaa na kufariki.

Watu wakiwa wamepanda ndege juu kwa matumaini ya kukimbia nchi
Watu wakiwa wamepanda ndege juu kwa matumaini ya kukimbia nchi

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema ndege yake ya kijeshi iliyoondoka Kabul Jumatatu jioni ilifanikiwa kuwabeba watu saba tu. Msemaji huyo aliongeza kuwa hapakuwa na uhakika jana usiku kwamba raia zaidi wa Ujerumani na watu wengine wanaotakiwa kuhamishwa kama wangeweza kufika uwanja wa ndege bila ya ulinzi wa wanajeshi wa Ujerumani. Mwandishi mmoja wa Afghanistan ameripoti kuwa baadhi ya shughuli zimeanza kurejea kawaida. Wakati huo huo kundi la Taliban limetangaza msamaha Afghanistan yote na kuwahimiza wanawake kujiunga na serikali yake na kujaribu kutuliza hali katika mji mkuu wa Kabul baada ya ghasia zilizoshuhudiwa katika uwanja wa ndege. Kauli hiyo imetolewa na Enamullah Samangani, mwanachama katika tume ya kitamaduni ndani ya Taliban, ikiwakilisha maoni ya kwanza juu ya uongozi.

Watu wakiwa wa Taifa la Ufaransa wakiingia kwenye ndege katika uwanja wa Kabul
Watu wakiwa wa Taifa la Ufaransa wakiingia kwenye ndege katika uwanja wa Kabul
17 August 2021, 14:13