WAWATA Imezindua Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake nchini Tanzania. Kilele cha Maadhimisho haya ni Septemba 2022. WAWATA Imezindua Kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya maisha na utume wake nchini Tanzania. Kilele cha Maadhimisho haya ni Septemba 2022. 

WAWATA Tanzania Kuelekea Jubilei ya Miaka 50 ya Utume, 2022! Yaani!

Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kuomba msamaha, neema na baraka ya kusonga mbele tena kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Muhimu: Utakatifu, Familia, Mazingira na Udugu!

Na Evaline Malisa Ntenga, WAWATA, Tanzania.

Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA kuanzia tarehe 22 hadi 26 Julai 2021 wamefanya mkutano wa maandalizi na hatimaye uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC lilipoanzisha WAWATA kunako mwaka 1972. Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake kwa WAWATA katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, ili kuomba msamaha, neema na baraka ya kusonga mbele tena kwa ari na moyo mkuu katika maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe ya Miaka 50 ya WAWATA umefanywa na Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa Ibada ya Misa Takatifu, Kurasini, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Katika kipindi hiki kuelekea Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA, wanaongozwa na Nyaraka zifuatazo: Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ambao kimsingi ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Ni wosia unaotoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni wosia unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Pili, ni Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa.

Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuitya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Udugu wa kibinadamu unakita mizizi yake katika umoja na ushirikiano. Kwa njia ya utamaduni wa udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia dhana ya upendo kwa watu wote, ili kujenga mahusiano, sheria, kanuni na taratibu zinazopania kudumisha amani na kuboresha maisha ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao. (Rej. Hotuba ya Kardinali Pietro Parolin, Uzinduzi wa Waraka wa “Fratelli tutti, tarehe 4 Oktoba 2020.)

Tatu, ni utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ambao WAWATA wanaalikwa kuutafakari kwa kina na kuchukua hatua muhimu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Nyaraka zote hizi, zikiwekwa kwa pamoja zinaunda kauli mbiu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya WAWATA yaani “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji”. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu Lk. 1:39: Mapendo kwa jirani: “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda…” WAWATA katika maisha na utume wake katika kipindi cha Mwaka 2021-2022 imejiwekea Mpango Mkakati wa Kazi. WAWATA itaendelea kutoa semina na kuhakikisha kwamba, inawafikia wanawake wengi zaidi, ili waweze kufahamu na hatimaye kushiriki kutumikia na kuwajibika kama Wanawake Wakatoliki.

Wanawake wanapaswa kuwa ni kiungo na daraja ndani ya Kanisa na familia. Viongozi wa WAWATA Jimbo, wanapaswa kusimamia hili kwa utekelezaji zaidi. Ni wajibu wa WAWATA kuhakikisha kwamba, kauli mbiu ya “Upendo, Mshikamano na Uadilifu wa Uumbaji”, inatangazwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya WAWATA. Viongozi waanze kuitumia na kuitafsiri kwa vitendo. Kutakua na mafundisho na malezi endelevu na fungamani kwa WAWATA katika majimbo mbalimbali nchini Tanzania yatakayozingatia Nyaraka za Baba Mtakatifu mintarafu Injili ya upendo ndani ya familia, urafiki wa udugu wa kibinadamu sanjari na utunzaji bora nyumba ya wote. Ni vyema ikiwa kama WAWATA wataweza walau kufahamu kwa undani zaidi kuhusu Nyaraka hizi za kitume kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Ikumbukwe kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA yanafanyika wakati ambapo Kanisa linasherehekea Mwaka wa Mtakatifu Yosefu. Mwaka wa Mtakatifu Yosefu ulizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na unatarajiwa kufungwa hapo tarehe 8 Desemba 2021.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu. Anasema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania. Jumuiya hii ilianzishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kunako mwaka 1972 kwa lengo la kuwasaidia wanawake kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”.

Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi!  Huu ni mwaka wa kufunga, kusali, kutafakari na kufanya hija kwenye vituo mbalimbali vua hija, kijimbo, kitaifa na Kimataifa kadiri ya hali itakavyoruhusu. Kutakuwa na Sala Maalum ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA, mwaliko kwa WAWATA wote kuisali. WAWATA chipukizi, wahamasishwe, ili kusaidia kuwaanda WAWATA wa leo na kesho sanjari na kuwasaidi wasichana wa Kikatoliki kujitambua na kujiheshimu. Semina za kiuchumi zitafanyika, ili kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, ili waweze kuchangia kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Majimbo yote yanatarajiwa kuzindukia maadhimisho haya kabla ya mwezi Oktoba 2021 na baadaye uzinduzi huu, utafanyika kwenye ngazi ya Dekania, Parokia na Vigango. Huu ni wakati wa kupanda miti, kama sehemu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. WAWATA ioteshe miti na kuitunza kama mboni ya jicho lao. WAWATA wafuatilie malezi na makuzi ya watoto, ili kuwajengea ari na moyo wa kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu miongoni mwa watoto wenzao.

Mafunzo, malezi na majiundo ya ndoa na familia yawasaidie WAWATA kutambua, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika: Ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbali mbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Kimsingi, taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi yake na wajibu wake wa Kikristo. Huu ni wajibu unaoanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, Jamii na Taifa kwa ujumla. Pia ni kuwasaidia wanawake kupata maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii, na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa taa na nuru katika Ulimwengu kama mawakili wema wa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Muundo wa WAWATA unapata chimbuko lake katika Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, Vigango, Parokia, Dekania, Jimbo hadi kufikia ngazi ya Taifa, kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki. Ikumbukwe kwamba, kila mwanamke mtanzania ni mwanachama wa WAWATA kutokana na Ubatizo wake. Kimataifa, WAWATA ni mwanachama hai wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, UMOFC, lililoanzishwa kunako mwaka 1910. Itakumbukwa kwamba, Mkutano mkuu wa kwanza wa WAWATA uliofanyika Jimbo kuu la Tabora Septemba 1972 ulimchagua Bibi Bernadette Nampombe Kunambi kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa WAWATA. Kwa sasa WAWATA inapojielekeza kwenye maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake inaongozwa na: Mama Evaline Malisa Ntenga, Mwenyekiti kutoka Jimbo kuu la Arusha. Mama Paschasia Rugumila, kutoka Jimbo Katoliki la Bukoba, Makamu Mwenyekiti. Mama Stella Kahwa, Katibu mkuu kutoka Jimbo Katoliki la Dar es Salaam. Mama Faraja Mbenna kutoka Tunduru-Masasi, Katibu Msaidizi. Na Mama Getrude Mtiga, Mtunza Hazina, kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Itakumbukwa kwamba, Mpango Mkakati wa utekelezaji wa maazimio kwa mwaka 2019-2022: Ni wanawake kujitakatifuza ili waweze kutakatifuza jamii. (Rej. Apostolic Exhortation Gaudete et exsultate: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote (Rej. Encyclical Laudato si). WAWATA inatarajia kutenga siku moja katika mwaka ili kutoa elimu juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kusimama kidete kupiga rufuku matumizi ya taka za plastiki. Ni wajibu wa wanawake kupanda miti kuzunguka maeneo yao ili kuboresha mazingira. Ni wakati muafaka wa kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kuwa na mipango ya kusaidia familia zenye matatizo na mahitaji maalumu. Kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu ya awali na endelevu ya katekesi makini, Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu kwa wakati muafaka. Kuunda na kuboresha Jumuiya ndogo ndogo za watoto, ili wawe na viongozi wao, Ibada ya Misa zao na Kwaya za watoto kwenye Parokia na vigango vyao.

Watoto kuanzia darasa la kwanza wahimizwe kuingia Shirika la Utoto Mtakatifu ili kuwafunda wamisionari wa baadaye! Kuendeleza Mpango kazi wa Wasichana kama sehemu muhimu ya WAWATA. Kupiga vita ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya Wanawake na ulinzi wa mtoto katika hatua zote tangu kutungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika mtu. WAWATA wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Maandalizi ya sherehe ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA (1972-2022): Septemba 2022 WAWATA Kama Jumuiya itatimiza Miaka 50 tangu kuidhinishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

WAWATA 50 Yrs
29 July 2021, 16:30