IMBISA ina laani ghasia na mipasuko ya kijamii inayoendelea kujitokeza nchini Eswatini, Kusini mwa Afrika. IMBISA ina laani ghasia na mipasuko ya kijamii inayoendelea kujitokeza nchini Eswatini, Kusini mwa Afrika. 

Tamko la IMBISA Kuhusu Hali Tete ya Kisiasa na Kijamii huko Eswatini

IMBISA, katika tamko lake kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii linasikitika na kulaani machafuko ya kisiasa nchini Eswatini ambayo yamepelekea watu kadhaa kupoteza maisha pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ambayo ni muhimu sana katika kukoleza maendeleo fungamani ya binadamu! IMBISA inaunga mkono tamko la Papa Francisko na Askofu Josè.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kwenda kulazwa na hatimaye kufanyiwa upasuaji mkubwa, Jumapili tarehe 4 Julai 2021, baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliyageuzia mawazo yake hadi nchini Eswatini, ambako katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na machafuko ya kisiasa ambayo yamepelekea hadi wakati huu watu zaidi ya 40 kupoteza maisha na wengine 150 kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu ametoa wito kwa viongozi wenye dhamana, mamlaka na wananchi wanaoandamana wakitaka maboresho katika maisha yao, kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuanza kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi, ustawi na mafao ya wengi. Iwe ni fursa ya kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki na amani licha ya tofauti zao msingi. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na maandamano makubwa nchini Eswatini kudai demokrasia zaidi lakini kwa mshangao mkubwa, waandamanaji wamekuwa wakikumbana na “mkono wa chuma”.

Watetezi wa haki msingi za binadamu wanautaka utawala wa nchi ya Eswatini kujielekeza katika kujenga na kudumisha demokrasia na utawala bora unazozingatia sheria. Umefika wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini Eswatini kutotumia nguvu kupita kiasi kupambana na waandamanaji. Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, “Inter-Regional Meeting of the Bishops of Southern Africa” IMBISA, katika tamko lake kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii linasikitika na kulaani machafuko ya kisiasa nchini Eswatini ambayo yamepelekea watu kadhaa kupoteza maisha pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ambayo ni muhimu sana katika kukoleza maendeleo fungamani ya binadamu! IMBISA inaunga mkono tamko la Baba Mtakatifu Francisko kuhusu mustakabali wa familia ya Mungu nchini Eswatini pamoja na tamko lililotolewa na Askofu José-Luis Ponce de Leòn, IMC., wa Jimbo Katoliki la Manzini nchini Eswatini anayewataka watu wa Mungu nchini Eswatini: kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea, haki, amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa.

Waamini na wananchi wote katika ujumla wao, wawe ni mashuhuda na vyomnbo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Wasichoke kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Amani, huku wakisali Rozari Takatifu. Majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Eswatini ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na wadau mbalimbali katika mgogoro unaoendelea kufuka moshi wa hatari nchini Eswatini. Vurugu, ghasia na uvunjifu wa haki msingi za binadamu ni jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na kuachwa liendelee. Serikali, pamoja navyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na ulinzi wa kutosha kwa watu na mali zao. Hiki ni kipindi muafaka cha kukuza na kudumisha majadiliano ya kweli. IMBISA inaiomba Jumuiya ya Kimataifa na kwa namna ya pekee kabisa, Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika, SADC kuingilia kati ili kuweza kupata suluhu ya kudumu kabla mambo hayajaharibika zaidi. Ujuzi halisi wa uongozi unajionesha pale ambapo watu wanaangalia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mamlaka za kisiasa hazina budi kubeba wajibu na dhamana yake katika mchakato wa ujenzi na ustawi wa Taifa husika. Rej. Laudato si, 178.

IMBISA inawataka watu wa Mungu kuendelea kuzingatia itifaki dhidi ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ili kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! IMBISA inawakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha au kujeruhiwa pamoja na kuombea utulivu na amani ya kudumu. IMBISA inawataka Emaswati wote kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa anasema Askofu Lúcio Andrice Muandula wa Jimbo Katoliki la Xai-Xai, nchini Msumbiji ambaye pia ni Rais wa IMBISA.

Tamko la Imbisa

 

 

08 July 2021, 15:41