Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 14 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Unyenyekevu wa Kiimani. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 14 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Unyenyekevu wa Kiimani. 

Tafakari Jumapili 14 ya Mwaka B: Unyenyekevu wa Kiimani Muhimu

Masomo ya Dominika hii yanatutafakarisha juu ya uwepo wa Mungu kati yetu na anayefanya kazi kati ya watu na ndani ya watu wake. Tunapaswa kujiuliza: Je, tunayo imani ya kutosha kutambua uwepo wa Mungu kati yetu? Tunahitaji unyenyekevu wa kiimani kuweza kuutambua uwepo wa Mungu na kulipokea Neno lake ambalo ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele! Imani Thabiti

Na Padre Andrew Mlele Mtaki, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya 14 ya mwaka B wa Kanisa. Masomo ya Dominika hii, kati ya mambo mengi, yanatutafakarisha juu ya uwepo wa Mungu kati yetu na anayefanya kazi kati ya watu na ndani ya watu wake. Tunapaswa kujiuliza: Je, tunayo imani ya kutosha kutambua uwepo wa Mungu kati yetu? Je, tunao unyenyekevu wa kutosha wa kupokea ukweli wa Injili pasipo kutazama sana mazingira au njia ambayo kwayo ukweli huo unatufikia? Tunahitaji unyenyekevu wa kiimani kuweza kuutambua uwepo wa Mungu na kulipokea Neno lake ambalo ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele.

TAFAKARI: Katika somo la kwanza Nabii Ezekieli anapokea nguvu ya kimungu na anatumwa apate kuitenda kazi ya Bwana. Hata hivyo nabii anaonywa juu ya uasi wa taifa ambalo kwalo anatumwa kupeleka ujumbe wa Mungu. Ni taifa lenye kuasi. Hata hivyo bado anatumwa na anahimizwa kuifanya kazi yake pasipo kujali uasi wa watu anaowaendea. Ni Mungu anafanya kazi ndani yake; naye nabii ni chombo cha kufanikisha kazi hiyo ya Mungu. Nguvu ya nabii iko katika imani kwamba ni Mungu ndiye anayetenda kazi ndani yake. Nabii ni msemaji wa Mungu, hivyo watu wanaolisikia neno la nabii wanapaswa kutambua kuwa Mungu mwenyewe amekuwako miongoni mwao kwa hali halisi. Si uwepo tu wa nabii kama mwanadamu bali uwepo wa Mungu anayetenda kazi kupitia nabii huyu. Katika somo la pili Mtume Paulo anadokeza kuhusu changamoto anazopitia katika utume wake; anapitia majaribu mengi; anao wapinzani na hata mjumbe wa Shetani anampatia taabu.

Hata hivyo Mtume Paulo anapokea yote haya kama jambo la kumkumbusha kwamba asijitazame yeye mwenyewe katika juhudi zake za kitume bali amtazame daima Kristo aliyemuita kuifanya kazi hiyo. Kwa maneno mengine Mtume Paulo anajikumbusha kwamba nguvu yake katika utume inatokana na karama za kipekee alizopewa na Mungu. Na anayo sababu ya kuvumilia magumu yote na kusonga mbele kwa matumaini kwa sababu ana imani katika yule aliyemuita kuifanya kazi yake. Katika Injili Yesu anakataliwa na watu wa kwao. Kijijini kwao Yesu, watu walidhani walijua Yesu alikuwa nani. Hawakujua kuwa Nafsi halisi ya Yesu haikuwa imefunuliwa kikamilifu kwao. Tatizo si ujumbe anaoutoa Yesu bali wana tatizo na historia na ufahamu walio nao juu yake. Wanashindwa kukubali mabadiliko makubwa wanayoyaona ndani ya Yesu. Kwa miaka 30 ya ukimya wake alihesabika kama mmoja wao aliyefikiri na kutenda kama walivyofanya wengine katika jamii aliyoishi. Lakini mabadiliko makubwa yanayotokea baada ya miaka mingi yanakuwa sababu ya kuwashtua. Wanajiuliza: huyu ameyapata wapi haya? Ni kwanini siku hizi hafanani na sisi tena? Kwanini anaonekana kuwa na kitu cha ziada kutuzidi sisi? Hata hivyo, kukataliwa na watu wa kwao hakumfanyi Yesu aiache kazi yake, bali anasonga mbele kwa nguvu zaidi. Anadumu katika unabii wake kwa kuwa anajua anao wito mkubwa zaidi kuliko upinzani mdogo anaopokea kutoka kwa watu wa kwao.

KATIKA MAISHA: Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, wewe na mimi kama ilivyokuwa kwa nabii Ezekiel na kwa mtume Paulo sisi sote tumepokea wajibu wa kinabii kwa njia ya ubatizo na kushirikishwa kazi ya Kristo, kuhani, nabii na mfalme. Ni wajibu tunaopaswa kuutekeleza kwa maisha yetu yote tukiwa wakristo. Tumeitwa kuwa vyombo vya Mungu tupate kuifanya kazi yake. Kila mmoja wetu anatumwa kuwa mjumbe wa Mungu pale alipo, kwa watu wanaomzunguka na katika mazingira aliyo nayo. Lazima kukumbuka kwamba kutangaza Habari Njema si kazi ambayo tunajipatia sisi wenyewe bali tunatumwa na Mungu. Tunapotimiza wajibu huo mkubwa lazima kujiaminisha kwa Mungu na daima kumpa yeye nafasi ya kwanza. Lazima watu wajue kuwa ni Mungu anayetenda kazi kati yao na kwamba sisi ni vyombo vya kufanikisha kazi hiyo. Ni kwa sababu hiyo Yesu alitaka watu wa kwao waonje zaidi uwepo wa Mungu kuliko kumtazama yeye kama mmoja wao.

Aidha, siku hii ya leo tunakumbushwa kwamba katika kutimiza wajibu wetu wa kutangaza Habari Njema na kumshuhudia Kristo tutakutana na changamoto; yatakuwepo majaribu, kutakuwa na shida na watajitokeza wapinzani. Haya yote tuyategemee na tujue kwamba haitakuwa lelemama. Hata hivyo ni kwa changamoto hizi mbegu ya Ukristo ilimea na kuwa na mizizi na hata kuzaa matunda. Habari njema ya Ufalme wa Mungu na mbegu ya imani ya Kikristo vimekuja kwa gharama kubwa sana. Nasi tuwe na hakika ya kuwa tutakutana na masumbufu mengi na kukataliwa lakini tudumu katika njia njema na tutapata matunda mema. Zaidi ya hayo, katika Dominika ya leo tunapewa tumaini kuwa Mungu hatukatii tamaa bali anataka tupate wokovu. Tazama jinsi ambavyo alimtuma nabii Ezekieli kwa taifa lenye kuasi. Uasi wa watu hawa si kikwazo kwa Mungu. Mungu hajawakatia tamaa sababu ya uasi wao. Anamtuma nabii kwao iwe watamsikiliza au watagoma kumsikiliza.

Mtume Paulo hakuchoka kutangaza Injili sababu ya wapinzani aliokutana nao. Vivyo hiyvo Yesu anadumu katika utume wao ingawa anakataliwa na watu wa kwao. Vikwazo visizime ari ya kutenda kutenda kazi njema. Usikate tamaa na kuacha kazi njema sababu ya vikwazo. Kama ni mzazi usikate tamaa juu ya wanao; usikate tamaa juu ya kazi yako; usikate tamaa juu ya wito wako. Daima mtegee Mungu na tenda kazi yako kwa msaada wake. Katika Dominika hii tuombe neema ya Mungu ili tuwe na ujasiri wa kusonga mbele katika kumshuhudia Kristo, na pia tuwe na uvumilivu tunapokutana na changamoto. Tuibebe kazi ya Mungu kwa ujasiri na kusonga mbele. Ninakutakia Dominika Njema na Mungu akubariki.

Liturujia J14 Mwaka B
02 July 2021, 15:58