Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17: Upendo na huruma ya Kristo kwa waja wake iwabidiishe waamini kujisadaka kwa ajili ya huduma inayosimikwa katika huruma na upendo. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 17: Upendo na huruma ya Kristo kwa waja wake iwabidiishe waamini kujisadaka kwa ajili ya huduma inayosimikwa katika huruma na upendo. 

Tafakari Jumapili 17 ya Mwaka B: Huduma ya Huruma na Upendo!

Ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa huruma na upendo. Yesu anawaonea watu huruma anawapatia chakula maana walikuwa na njaa. Muujiza huu ni maandalizi ya muujiza mkubwa wa Sakramenti ya Ekaristi. Katika maadhimisho la Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anatulisha kwa Neno lake na pia kwa Mwili na Damu yake azizi, ili tuwe pia sadaka.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka B wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa masomo ya dominika hii ni kuwahudumia wahitaji kwa moyo wa huruma na upendo. Yesu anawaonea watu huruma anawapatia chakula maana walikuwa na njaa. Muujiza huu ni maandalizi ya muujiza mkubwa wa Sakramenti ya Ekaristi. Katika maadhimisho la Ekaristi (Misa Takatifu) Kristo anatulisha kwa Neno lake na pia kwa Mwili na Damu yake. Kwa ishara hizi Kristo anatuonyesha namna ya kuwa wachungaji wema. Mchungaji mwema anashughulikia uhai na usatawi wa kondoo wake. Somo la kwanza la kitabu cha pili cha wafalme (2Fal. 4:42-44); linatufundisha kuwa manabii walifanya miujiza kwa sababu Mungu alikuwa pamoja nao. Elisha anafanya muujiza wa kuwalisha watu mia kwa chakula alicholetewa na mtu kutoka Baal-shalisha. Ni chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano gunia moja. Watu walikula na kusaza sawasawa na neno la Bwana. Kumbe tukimtumainia Mungu hatutapungukiwa na chochote.

Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 4:1-6); Mtume Paulo anawaonya Wakristo wa Efeso wawe na umoja, ndiyo kiini cha maisha ya kikristo. Kwa vile sisi wakristo tumejiunga na Yesu sharti tuwe na umoja kati yetu. Tukitengana twabomoa kazi ya Mungu. Ekaristi Takatifu, mwili na Damu Azizi ya Kristo tunayoipokea inatudai kuishi kwa umoja na upendo. Kuishi kwa umoja na upendo kama jamii ya kikristo ndiko kuishi Ekaristi kwani tunashiriki meza moja ambayo inatutaka ushirika katika maisha ya kijamii pia ili Ekaristi iwe na maana na ukristo wetu uwe na maana yatupasa kuishi kwa umoja na upendo. Katika Injili ilivyoandikwa na Yohane (6:1-15): Mwinjili Yohane anaona kuwa kama Yesu anaweza kuwalisha watu kwa chakula cha kawaida, anaweza pia kuwalisha kwa chakula cha mbinguni. Tunakula chakula hiki ambacho ni mafundisho yake na Ekaristi Takatifu, tukisadiki kwamba na Yeye ni Mwana wa Mungu aliyetumwa na Baba kutukomboa.

Ekaristi Takatifu ndicho chakula chetu cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuelekea Mbinguni. Ekaristi Takatifu inatupa nguvu ya kupambana na magumu katika safari hii kama malaika alivyomwambia Eliya; “Inuka ule, la sivyo safari hii itakuwa ngumu kwako” (1Wafalme: 19:7). Muujiza wa Yesu kuwalisha watu elfu tano una uhusiano wa moja kwa moja na Ekaristi. Mfululizo wa vitenzi: “Akaitwa, akaibariki, akaimega, akawapa”; unadokeza Sadaka ya Ekaristi Takatifu. Katika miujiza ya kuwalisha watu; muujiza wa Elisha na muujiza wa Yesu, wote wawili hawakutumia chakula chao bali ni chakula walichotoa watu wengine kwa moyo wa ukarimu bila kuangalia maslahi yao binafsi wala wingi au udogo wa kile walichokuwa nacho. Hicho kidogo kilichotolewa kwa ukarimu kwa upande wa Elisha na kwa upande wa Yesu kilikuwa kingi cha kuwatosha watu wote kwani neema na baraka za Mungu hazijawahi kupungua hata kidogo. Katika injili; mikate mitano na samaki wawili walikula watu elfu tano wakasaza vikapu 12 na katika somo la kwanza watu mia walikula na kusaza maana Elisha aliamini kuwa; “Mungu amekwisha ahidi kuwa watakula na kusaza.”

Tusiogope kutoa kwa kuhofia tutabaikiwa na nini? Tumkumbuke mwanamke mjane wa Serapta aliyemsaidia Eliya kwa kumtengenezea mkate kwa unga ni kidogo lakini kama alivyosema Eliya; “kopo la unga halikuisha wala chupa ya mafuta haikupungua” (1Wafal.17: 8-24). Kama hiyo haitoshi mtoto wa yule mama alipofariki Eliya alimfufua.  Wapeni watu ili wale, Mungu atawabariki maana mkono utoao ndio upokeao. Katika maisha tunaweza kuwa tunalalamika juu ya uchache wa raslimali. Hii inapelekea kuwa na mioyo ya uchoyo na ubinafsi na kusema tulichonacho hakitutoshi sisi na wao. Ndivyo Andrea alivyomwambia Yesu; “Yupo mtoto aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hii ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yn. 6:8). Yesu akajibu; “Waketisheni watu.” Ndivyo mtu kutoka Baal-shalisha alivyomwambia Elisha; “Je niwaandikie hiki watu mia?” (2 Wafalme 4:42). Elisha akasisitiza; “Uwape watu, ili wale, kwa kuwa Bwana asema hivi: Watakula na kusaza” (2 Waf. 4:42).  Kila tulichopewa tumepewa kama mifereji ili kipitie kwetu kiwafikie wengine. Hivyo tulichojaliwa tunaalikwa kuwa; “wapeni watu ili wale.” Mungu atakibariki hicho kidogo.

Kristo atabariki juhudi zetu. Si lazima uchangie mali; changia ulichonacho. Elimu yako; wape watu ili wale, karama ulizojaliwa, wape watu ili wale; nguvu ulizojaliwa, wape watu ili wale; muda ulio nao, wape watu ili wale. Kumbuka kujilimbikizia mali wakati wengine wanakufa njaa ni kula hukumu yako mwenyewe. Tuweni watu wa shukrani. Yesu kabla ya kuwapa mitume mikate na samaki ili wawagawie watu, alishukuru kwanza. Ekaristi ni Sadaka ya shukrani, tujifunze kushukuru kwa kila jambo. Lakini tujue pia kila mmoja wetu anapaswa kutoa mchango wake katika mafanikio ya kimaisha kwa maana Mungu wetu ni Mungu anayeshirikisha juhudi zetu ndiyo maana Yesu na Elisha hawakufanya miujiza kutoka hewani bali kwa vile vilivyokuwepo. Mtakatifu Josemaria Escriva: anasema; Yote yawezekana kwake yule anayesadiki. Tumwombe Mungu atujalie viongozi katika familia zetu, katika Kanisa, katika jamii na katika nchi yetu na dunia kwa ujumla wenye moyo wa kushughulikia ustawi, maendeleo na maslahi ya watu wote bila ubaguzi. Tumwombe Mungu pia atujalie moyo wa ukarimu wa kuchangia alivyotujalia kwa maendeleo ya jamii zetu na kwa kuwasaidia wengine na atuondolee ubinafsi na ufisadi na rushwa na wizi wa mali ya umma.

J17 Mwaka B

 

22 July 2021, 16:12