Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia: Familia 58 zafunga ndoa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo ndani ya Familia: Familia 58 zafunga ndoa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, Jimbo kuu la Dar es Salaam. 

Furaha ya Upendo Ndani ya Familia: Ndoa 58 Zafungwa DSM!

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi hivi karibuni ameshuhudia kwa niaba ya Kanisa, wanandoa 58 kutoka Parokia ya Bunju, Jimbo kuu la Dar es Salaam wakifunga pingu za maisha. Kwa Mzee Beda Tarimo mwenye umri wa miaka 64 na Bibi Sophia Sumbari mwenye umri wa miaka 55, siku hiyo waliamua “kubwaga manyanga” na kuachana na uchumba sugu! Bado hujachelewa! Amua!

Na Remigius Mmavele, Dar es Salaam na Pd. Richard Mjigwa, C.PP.S, Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” yalizinduliwa hapo tarehe 19 Machi 2021 na yatahitimishwa rasmi mjini Roma wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la maadhimisho ya ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni: kujitahidi kunafsisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Pili, hii inapaswa kuwa ni fursa ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani; shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Tatu, waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ndoa inapyaisha upendo wa kibinadamu. Kuna changamoto za kisiasa, kijiografia na kitamaduni mintarafu utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia mambo yanayolitaka Kanisa kuwa karibu sana na waamini kama Msamaria mwema; Mama mwenye huruma na mapendo, anayefundisha, anayeganga na kutaka kuponya madonda yanayowaandama watoto wake katika uhalisia wa maisha! Changamoto ya kwanza ni kuporomoka kwa Injili ya matumaini miongoni mwa waamini sanjari na upendo wa Kikristo mintarafu kweli na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hali hii inawapelekea vijana wa kizazi kipya, kushindwa kufanya maamuzi machungu katika maisha yao, kwa kuwajibika kikamilifu katika maisha ya ndoa na familia, hadi pale Mwenyezi Mungu atakapowaita waja wake, kwenye maisha ya uzima wa milele. Matokeo yake ni ndoa za mpito ambazo hazidumu hata kidogo!

Kuna matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema; uwepo wa utamaduni wa kifo na mwelekeo tenge wa tendo la ndoa unaogeuzwa kuwa ni fursa ya kukidhi tamaa za mwili badala ya kuwa kweli ni kielelezo cha utimilifu wa upendo kati ya bwana na bibi. Dhamana na utume wa familia katika nchi nyingi duniani, haupewi msukumo unaostahili na matokeo yake, familia imekuwa kama “mpira wa danadana au mpira wa kona unaogombaniwa na wengi. Elimu makini kwa watoto ni dhamana ambayo kwa sasa inaondolewa polepole kutoka kwa wazazi na walezi na matokeo yake ni mwelekeo tenge wa usawa wa kijinsia unaotaka kufuta tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kimsingi, wazazi wanapaswa kuwa ni walezi na warithishaji wa imani, maadili na utu wema kwa watoto wao, lakini utume huu sasa unafanywa na baadhi ya taasisi pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umekuja kwa wakati muafaka ili kusaidia kujibu changamoto pevu zinazowaandama waamini katika utume wa maisha ya ndoa na familia.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam nchini Tanzania, hivi karibuni ameshuhudia kwa niaba ya Kanisa, wanandoa 58 kutoka Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, Jimbo kuu la Dar es Salaam wakifunga pingu za maisha. Kwa Mzee Beda Tarimo mwenye umri wa miaka 64 na Bibi Sophia Sumbari mwenye umri wa miaka 55, siku hiyo waliamua “kubwaga manyanga” na kuachana na uchumba sugu uliokuwa umewakamata miguu tangu mwaka 1984 walipokuwa wameoana kimila! Kulikuwa pia kuna msigano wa kiekumene kwani, wazazi wa Mama Sophia kutoka Kanisa Anglikan hawakuwa tayari kuona mtoto wao anaolewa na Mkatoliki. Malumbano haya yalipelekea Mzee Beda Tarimo na Bibi Sophia Sumbari kushindwa kufunga ndoa ya Kikatoliki, hadi mwezi Julai 2021, baada ya wazazi wao kufariki dunia kwa nyakati tofauti. Lakini katika kipindi chote hiki, walikuwa wanahudhuria Ibada ya Misa Takatifu kama kawaida, lakini hawakuweza kushiriki Ekaristi Takatifu. Waliendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kama waamini kwenye Familia na Jumuiya ndogondogo za Kikristo.

Mzee Beda Tarimo na Bibi Sophia Sumbari wanawataka wazazi na walezi kutoendekeza mila na desturi zilizopitwa na wakati kwa kuwanyima uhuru watoto wao kufanya maauzi ya busara na hekima, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya maisha yao ya kiroho, kiutu na kijamii. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amewataka wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, maisha yao yanaongozwa na neema na baraka za Mwenyezi Mungu na kamwe wasikubali kupotoshwa na kutumbukia katika mila na desturi zilizopitwa na wakati sanjari na ushirikina. Waamini wawe imara katika imani, matumaini na mapendo. Matatizo, changamoto na fursa zinapojitokeza katika safari ya maisha yao, wajitahidi kujikita katika sala na sadaka kwa Mwenyezi Mungu ambaye ndiye tiba, njia, ukweli na uzima katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, viongozi wanaosimamia na kutekeleza shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia, wanapaswa kutambua fika changamoto hizi, ili kuweza kujizatiti kikamilifu, kwa kujivika fadhila ya uvumilivu na udumifu katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuwa na sera na mikakati inayotekelezeka na wala si mambo yanayoelea kwenye ombwe! Wawe makini kwa utu na heshima ya binadamu; wasaidie kuelimisha umuhimu wa uhuru unaowajibisha, ili kuwasaidia wahusika kukomaa katika imani, maadili na utu wema. Wanandoa wasaidiwe kutambua ukweli kuhusu maisha yao; uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Wawaoneshe wanandoa ambao katika uvumilivu na udumifu wao, hadi leo hii wamekuwa ni mfano bora wa kuigwa. Majiundo makini ya awali na endelevu ni muhimu sana kwa wanandoa ambao wanapaswa kuishi maisha yao yote katika kifungo cha upendo usiogawanyika hata kidogo!

Wanandoa watambue dhamana na wajibu wao, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari ndani ya familia, ili kujenga umoja na mshikamano ndani ya Kanisa, ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wa nyakati hizi. Utakatifu wa maisha ya wanandoa ni changamoto endelevu katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji. Maandalizi ya wanandoa watarajiwa, dhamana na wajibu wa Kanisa kuwasindikiza wanandoa wapya; malezi na majiundo makini ya maisha ya ndoa na familia; utume kwa wazee ni kati ya changamoto ambazo Mama Kanisa anapaswa kuzivalia njuga kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia duniani.

DSM Ndoa na Familia
18 July 2021, 15:35