Kardinali Blase Joseph Cupich ameandika waraka wa kichungaji dhidi ya machafuko ya kijamii kwa kukazia ha, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Marekani. Kardinali Blase Joseph Cupich ameandika waraka wa kichungaji dhidi ya machafuko ya kijamii kwa kukazia ha, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Marekani. 

Waraka wa Kichungaji Dhidi ya Machafuko ya Kijamii Marekani

Kardinali Blase Joseph Cupich, ameandika Waraka wa kichungaji kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kushinda kishawishi cha kujitumbukiza katika machafuko ya kijamii, kisiasa na kiitikadi na badala yake, wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na majadiliano; kwa kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikilizana kwa makini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Uwezekano wa kuishi pamoja kati ya Mataifa mbalimbali unategemezwa na misingi ileile ambayo ingekuwa ni miongozo ya uhusiano kati ya binadamu: ukweli, haki, mshikamano wa kweli kimatendo na uhuru. Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu kanuni za kikatiba juu ya jamii ya kimataifa yanasema kwamba, mahusiano kati ya watu na jumuiya za kisiasa yanaratibiwa kimantiki, kihaki, kisheria na kwa maafikiano bila vurugu au vita wala aina yoyote ya ubaguzi, vitisho na udanganyifu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa rangi na maamuzi mbele kwa kutambua kwamba, kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila mtu anastahili kuheshimiwa, kupewa haki zake msingi sanjari na utu wake kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote! Ni katika muktadha huu, Kardinali Blase Joseph Cupich, Askofu mkuu wa wa Jimbo kuu la Chicago, nchini Marekani, ameandika Waraka wa kichungaji kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani kushinda kishawishi cha kujitumbukiza katika machafuko ya kijamii, kisiasa na kiitikadi na badala yake, wajitahidi kuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na majadiliano; kwa kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikilizana kwa makini.

Takwimu kutoka Jeshi la Polisi nchini Marekani zinaonesha kwamba, idadi ya mashambulizi ya silaha za moto imeongezeka maradufu na kufikia watu 2, 019 hadi kufikia tarehe 4 Julai 2021. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 13% ikilinganishwa na asilimia 58% kwa mwaka 2019. Kardinali Blase Joseph Cupich, katika Waraka wake wa kichungaji anasema, machafuko ya kijamii, kisiasa na kiitikadi pamoja na madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni tishio kwa amani, usalama na mafungamano ya kijamii miongoni mwa watu wa Mungu nchini Marekani. Watu wanaogopana kiasi kwamba, kuna kilio kikubwa cha kutaka Serikali kuu la Marekani ifanye marekebisho kuhusiana na; Jeshi la Polisi, Mfumo wa Makosa ya Jinai; Udhibiti wa biashara ya silaha pamoja na serikali kuyashughulikia magenge ya uhalifu nchini Marekani. Sanjari na jitihada zote hizi, lakini pia kuna haja ya wananchi wa Marekani kujikita katika kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia pamoja na elimu makini kwa vijana wa kizazi kipya. Zote hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa kanuni na tunu msingi za kimaadili.

Chuki, uhasama na utengano ni mambo yanayofumbatwa katika misingi ya ubaguzi wa rangi, ukabila, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa pamoja na misimamo mikali ya kisiasa, kidini na kiimani. Kwa bahati mbaya watu wengi wanashindwa kutambua kwamba, wote ni wamoja, licha ya tofauti zao msingi, dhana ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaipatia kipaumbele cha pekee katika Waraka wake wa Kitume:"Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Papa anagusia kuhusu magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Anahimiza maisha ya kiroho, mshikamano wa kidugu, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Siasa safi ni kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Kardinali Blase Joseph Cupich anakaza kusema, ikiwa kama wananchi wa Marekani watashindwa kutambua na kuthamini mafungamano haya ya kijamii, watu pia watapoteza dira na mwelekeo kuhusu: huruma, mapendo na utamaduni wa kuwajibikiana. Matokeo yake yana madhara makubwa katika maisha ya watu wa Mungu. Umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu sana katika kunogesha amani na haki jamii!

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kristo Yesu, Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Rej. LG 1. Hii ni changamoto kwa waamini kubaki katika utambulisho wao; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kibinadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe ni madaraja yanayowakutanisha watu kwa kujikita katika fadhila za Kimungu. Matumaini ni sawa na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, uwasaidie waamini kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Kristo Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, aliwafunuliwa wafuasi wake kiini cha maisha na utume wake, alipowashirikisha kuhusu mateso, kifo na ufufuko wake kama utekelezaji wa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na hivyo kuwaalika wanafunzi wake kushiriki kikamilifu katika utume wake wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu nyeti, Kardinali Blase Joseph Cupich, katika Waraka wake wa kichungaji anawataka waamini kujenga utamaduni wa kuuliza maswali, kusikiliza majibu kwa makini hata ikiwa ukweli huu ni sehemu ya machungu kwa mtu binafsi. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano katika ukweli, haki na upendo, ili kuelewana zaidi. Waamini wawe ni watu wa sala, ili kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kupata mang’amuzi katika maisha, wakitambua kwamba, wako kwenye mikono salama ya Mwenyezi Mungu na Kristo Yesu daima anaendelea kuambatana nao katika hija ya maisha hapa duniani. Waamini wanapaswa kufuata vidokezo vya uwepo wa Mungu katika maisha, ili hatimaye kung’amua ni mahali gani ambapo Mwenyezi Mungu anapenda kuwapeleka. Kwa maneno mengine, haya ni mang’amuzi katika maisha yatakayowasaidia kudumu katika haki, amani na maridhiano.

Katika kipindi cha kinzani na mipasuko ya kijamii, watu wengi wanapenda kujifungia katika undani wao wakidhani ni mahali pa salama. Lakini, jambo la msingi hapa ni kutoka katika ubinafsi ili kuunganika na wengine, kiasi hata cha kuthubutu kuhatarisha maisha. Lengo kuu ni kubaki ukiwa umeunganika na wengine katika imani, matumaini na mapendo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jambo la msingi ni kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kama Mzaburi anavyosema kwamba, Mwenyezi Mungu ni kinga kuu ya waadilifu katika shida na mahangaiko yao. BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Rej. Zaburi ya 91. Mtakatifu Paulo VI aliwahi kusema, ukitaka amani, jibidishe kutenda haki!

Waraka wa Kichungaji

 

11 July 2021, 15:28