Askofu Simo Chibuga Masondole kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi ili kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bunda. Askofu Simo Chibuga Masondole kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi ili kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bunda. 

Askofu Simon Chibuga Masondole Awekwa Wakfu na Kusimikwa Rasmi!

Tarehe 4 Julai 2021 Askofu Simon Masondole amesimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Bunda. Changamoto kwa watu wa Mungu ni kujizatiti katika sala zinazobubujika kutoka katika nyoyo zao, ili kumwombea Askofu Masondole, ili apate nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa ari na moyo mkuu, huku akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bunda.

Na Padre Nikas Kiuko, Bunda, Tanzania.

Mama Dorothea Nyamtondo Masondole, Mama mzazi wa Askofu Simon Chibuga Masondole ni kati ya waamini waliovuta hisia za watu wengi, aliposimama kutoa neno la shukrani, akisema kwamba, katika maisha yake alibahatika kupata watoto kumi na mmoja. Kati yao kuna watoto wakike saba na wakiume ni wanne na kati yao kuna Padre na sasa katika familia wamepata pia Askofu. Anasema, watoto wake walipomshikirisha wazo la kwenda Seminarini kwa malezi ya Kipadre alipokea mawazo haya kwa moyo wa ukarimu na kumshirikisha Mungu ambaye ni asili ya maisha na zawadi zote. Amewakumbusha wazazi wenzake kwamba, wito unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wazazi wawe wepesi kuwaruhusu watoto wao wanaoonesha nia ya kuwa Mapadre na Watawa. Wawasaidie kutimiza ndoto zao na kuendelea kuwasindikiza kila siku katika sala, kwa hali na mali! Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Maaskofu ni waandamizi wa Mitume wamekabidhiwa mamlaka na utume wa kuyafundisha Mataifa yote, kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, ili watu wote wapate wokovu kwa njia ya imani, ubatizo pamoja na kuzishika Amri za Mungu.

Maaskofu wanatenda na kutekeleza wajibu huu kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Huu ni utumishi wa kweli unaosimikwa katika huduma kwa watu wa Mungu. Maaskofu wamepewa jukumu la kufundisha imani, maadili na utu wema, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa njia hii, Maaskofu ni mashuhuda wa kweli za Kiinjili. Maaskofu wamepewa dhamana ya kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo na Sakramenti za Kanisa. Hivyo kwa njia ya sala na utume wao kwa ajili ya watu wa Mungu wanamimina ukamilifu wa utakatifu wa Kristo kwa namna mbalimbali na kwa wingi. Lakini zaidi ni kwa njia ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa pamoja na maisha adili, yenye mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu. Maaskofu wamepewa jukumu la kuwaongoza watu wa Mungu kwa njia ya mashauri, maonyo, mamlaka na uwezo mtakatifu; mambo yanayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma makini. Maaskofu wajenge na kudumisha sanaa ya kusikiliza kwa makini na awe tayari kutangaza na kuishuhudia Injili kwa watu wote wa Mataifa. Rej. 24-27.

Haya ndiyo majukumu aliyokabidhiwa Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda katika Ibada ya kumweka wakfu na hatimaye, kumsimika kuwa ni Askofu wa Pili wa Jimbo Katoliki la Bunda lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Tarehe 20 Febuari 2011 Jimbo la Bunda likazinduliwa rasmi na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, akasimikwa na kuwa ni Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Bunda. Tarehe 4 Julai 2021 Askofu Simon Masondole amesimikwa na kuwa ni Askofu wa pili wa Jimbo Katoliki la Bunda. Changamoto kwa watu wa Mungu ni kujizatiti katika sala zinazobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kumwombea Askofu Masondole, ili apate nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa ari na moyo mkuu, huku akifundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bunda.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande katika mahubiri yake amemtaka Askofu Masondole awe na ujasiri wa kukemea dhambi jamii zinazokwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Askofu Masondole awe na ujasiri wa kukemea rushwa, ufisadi na tabia ya watu kutaka kukwepa kulipa kodi, wakati ni wajibu wao kwa ajili ya kunogesha maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu Masondole kwa kumtumikia Mungu, Kanisa na watu, anabeba dhamana nzito sana katika maisha yake, kumbe, ni wajibu wake kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa tunza na ulinzi wake, huku akiendelea kujikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, kufunga na matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, amemshauri Askofu Simon Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda kuzingatia ushauri kutoka Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, na kutekeleza kwa amani na utulivu kwenye majukumu yake. Kanuni ya Imani aliyokiri mbele ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bunda pamoja na viapo vya utii na uaminifu kwa Baba Mtakatifu, daima akijiaminisha katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu sanjari na kuendelea kufuata mifano bora ya Mitume wa Yesu. Auanze utume wake kwa furaha, amani na utulivu. Askofu Masondole, atambue umuhimu wa sala katika maisha na utume wake. Katika salam zake za shukrani, Askofu Simon Chibuga Masondole, amewashukuru watu wote wa Mungu nchini Tanzania na ameahidi kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea katika sala zake na amewakaribisha Jimbo Katoliki la Bunda, ili kwa pamoja waendelee kumshukuru na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani.

Naye Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amekazia umuhimu wa kujikita katika utakatifu unaofumbatwa katika upendo wa dhati. “Ut essemus sancti in caritate” yaani “Tuwe watakatifu katika upendo”. Kumbe, kipaumbele chake cha kwanza ni kuwasaidia watu wengi zaidi wawe watakatifu katika upendo, kwa kutimiza mapenzi ya Mungu na hatimaye, waweze kufika mbinguni. Katika Ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Simon Chibuga Masondole kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewakilishwa na Waziri mkuu Kassim Majaliwa. Amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bunda, ili kumwezesha kutekeleza vyema majukumu yake, kwani Serikali inatambua mchango wa mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini. Maisha ya sala yatamwezesha Askofu Masondole kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zitakazoibuka katika maisha na utume wake.

Kanisa Katoliki nchini Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu. Kati ya shule za msingi 18, 546, Kanisa Katoliki linamiliki na kuendesha shule 204. Kuna shule za Sekondari 5, 289 kati ya hizo, Kanisa Katoliki lina miliki shule 266. Kuna vyuo vikuu 47 na kati yake Kanisa Katoliki linamiliki vyuo 12. Ni matumaini ya Serikali ya Tanzania kwamba, Kanisa Katoliki litaendelea kujizatiti katika kuboresha elimu, ili watanzania waweze kupata elimu bora. Kanisa liendelee pia kuwekeza katika sekta ya afya, kwani Serikali ina thamini huduma na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kujikita katika kanuni ya dhahabu! Waziri mkuu, amewasihi watanzania kuwa ni watu wa sala, upendo, mshikamano na msamaha, ili kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kicha ya tofauti msingi zinazoweza kuwepo miongoni mwa watanzania.

Askofu Masondole

 

 

05 July 2021, 15:51