Mashemasi ni Wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa lakini zaidi mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini. Mashemasi ni Wahudumu wa Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa lakini zaidi mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini. 

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Wapata Mashemasi Wapya!

Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, hivi karibuni, ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi wawili kutoka Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Mashemasi ni wahudumu wa Injili ya Upendo.

Na Angela Kibwana, - Morogoro.

Sakramenti ya Daraja Takatifu imegawanyika katika Madaraja makuu matatu: Daraja ya Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Daraja ya Ushemasi “Diakonia” huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa: Shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu Sakramenti za Kanisa na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa; tafakari ya Neno Mungu na nidhamu katika maisha ya utii, useja na ufukara.

Hiki ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu! Utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia katika huduma ya Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza. Huu ni wito na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake. Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe. Mashemasi wawe na huruma na wenye bidii wakienenda katika ukweli wa Bwana Yesu Kristo aliyejifanya mtumishi wa watu! LG 29.

Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, hivi karibuni, ametoa Daraja Takatifu ya Ushemasi kwa Majandokasisi wawili kutoka Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania. Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa kwenye Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Kola, Jimbo Katoliki la Morogoro, Tanzania. Waliopewa Daraja takatifu ya Ushemasi ni John Francis Kisori na Abel William Missanga. Askofu Edward Elias Mapunda katika mahubiri yake, amewataka Mashemasi wapya kujenga na kudumisha tabia ya unyenyekevu, ili kunogesha mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wajitahidi kuepukana na tabia ya majivuno na kiburi kwani ni hatari kwa maisha yao ya kiroho.

Mwenyezi Mungu ndiye muasisi wa miito yote mitakatifu ndani ya Kanisa. Kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, amewekewa kusudi na malengo yake, tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Miito mbalimbali ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake ni kuendeleza kazi ya uumbaji na ukombozi inayopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mashemasi wapya wajitahidi kuishi kikamilifu wito wao kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu na utii kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa mwaliko kwa miito mbalimbali na kuikamilisha kazi hii kwa njia ya neema na baraka kutoka kwake Yeye ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo. Wazazi na walezi wasiwe ni kikwazo kwa watoto wao kuitikia miito mbalimbali kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu anawaita watu mbalimbali kutenda kazi katika shamba lake.

Jambo la msingi kwa wale wote waliotikia wito na zawadi ya Daraja Takatifu kuendelea kukesha kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Upatanisho mambo yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha wongofu wa shughuli za kichungaji. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu ni dalili kwamba, wito na utume wa Daraja takatifu umehifadhiwa katika chombo cha udongo. Mwenyezi Mungu anapenda kuwatakasa na kuwaimarisha katika utume wao, ili waweze kuifanya kazi hii kwa uaminifu na uadilifu mkubwa. Mashemasi na Mapadre wajenge hofu ya Mungu, Ibada na uchaji kamili tayari kumtumikia Mungu. Kamwe wasijenge hofu juu ya maneno ya watu, kwani Mwenyezi Mungu anayeona sirini daima atakuwa pamoja nao, kwani siku zote anaumba na kutuma. Mashemasi na Mapadre walinde na kutunza: heshima na hadhi ya wito, zawadi na maisha ya kipadre.

Watekeleze dhamana na wajibu wao kwa weledi, uadilifu na uaminifu mkubwa kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, daima wakijisadaka katika huduma kwa watu wa Mungu kama walivyofanya Mitume wa Yesu. Watende mema kwa ujasiri, imani na matumaini; huku wakitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima wakijitahidi kufuata nyayo za Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Mashemasi wawe ni wahudumu waaminifu wa Neno la Mungu na Injili ya upendo kwa watu wa Mungu, ili Kristo Yesu aweze kufahamika, kupendwa na kutumikiwa zaidi kwa njia ya huduma ya upendo kwa jirani. Mashemasi watambue kwamba, hii si ajira, bali ni huduma kwa watu wa Mungu! Hivyo wajitahidi kuwa wema, watakatifu na wachamungu.

Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida amewapongeza Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania kwa hatua mbalimbali za majiundo katika maisha yao ya kitawa yanayosimikwa katika nguzo kuu tatu yaani: Utume wa kuendeleza ndoto ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo ya kutangaza na kuhubiri: huruma na upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Damu yake Azizi, daima wakiwa makini kusoma alama za nyakati. Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo Yesu, wanaitwa na kutumwa kwenda kusikiliza na kujibu kilio cha damu kwa njia ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Mhimili wa pili ni maisha ya kijumuiya yanayofumbatwa katika kifungo cha upendo “Vinculum Caritatis”. Hii ni kutokana na sababu kwamba, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ni Shirika la Kazi za Kitume ambalo halina nadhiri hata kama wanaziishi kama Mapadre na Watawa wengine.

Wote kwa pamoja huweka vipaji, rasilimali, amana na utajiri wao kwa ajili ya kutangaza Ufalme na kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mhimili wa tatu ni tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, mto wa rehema, chemchemi ya huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Shemasi John Francis Kisori na Shemasi Abel William Missanga wamemshukuru Mungu kwa zawadi, wito na utume wa Daraja Takatifu ya Ushemasi wa mpito. Wanawaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka zao katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya utakatifu wa maisha na utume wao kwa watu wa Mungu!

Mashemasi CPPS
16 July 2021, 08:21