Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani kwa Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha mapya! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 13 ya Mwaka B wa Kanisa: Imani kwa Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha mapya! 

Tafakari Jumapili 13 ya Mwaka B: Imani Chimbuko la Maisha Mapya!

Katika Injili ya leo tunasikia Yesu akifanya miujiza miwili. Kwanza tunakutana na mkuu wa Sinagogi, Yairo anayekuja kwa Yesu kumsihi na kumwomba ili amponye binti yake aliyekuwa kufani. Tunakutana na mwanamke mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu kwa miaka kumi na miwili. Binti Yairo na Mwamke huyu aliyeteseka wanaponywa kwa imani kwa Kristo Yesu!

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya leo ni mwendelezo wa Injili tuliyoitafakari Dominika iliyopita baada ya Yesu kuvuka na wanafunzi wake na kufika upande wa pili wa ziwa lile la Galilaya. Yesu leo yupo katika nchi ya wapagani, ndio Wagerasi. Katika Injili ya leo tunasikia Yesu akifanya miujiza miwili. Kwanza tunakutana na mkuu wa Sinagogi, Yairo anayekuja kwa Yesu kumsihi na kumwomba ili amponye binti yake aliyekuwa kufani. Na kabla ya kutimiza ombi la Yairo, tunakutana na mwanamke mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu kwa miaka kumi na miwili. Ni baada ya kumponya mwanamke yule, tutasikia tena Injili ikirejea katika kurejeshewa uhai binti wa Yairo. Mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, Mwinjili Marko hautaji tu ugonjwa au tatizo la yule mwanamke bali zaidi sana anatupa hata na taarifa nyingine nyingi zaidi. Muda wa miaka kumi na miwili, anayekosa tiba kwa matabibu wengi, ametumia gharama kubwa na hata kumaliza akiba yake yote bila mafanikio kwani hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi na zaidi.

Lakini mbaya zaidi kwa kadiri ya dini ya Kiyahudi kutokwa na damu ilimfanya ahesabike kuwa ni najisi na hata kutengwa na shughuli za ibada. Hivyo alipaswa kutengwa sio tu kwenye kushiriki ibada bali hata kwa maisha ya siku kwa siku kwani alihesabika sawa na mkoma. Na hata ikitokea mtu akagusana na mtu mwenye tatizo kama hilo naye alipaswa kufuata taratibu za kiibada ili aweze kujitakasa. (Walawi 15:25-27) Mwanamke yule aliyekuwa na tatizo la kutokwa na damu, kama wengi wengine wenye shida mbali mbali waliosukumwa kwa ndani kwenda na kumlilia Yesu ili wapate uponyaji, naye anasukumwa na imani kubwa kabisa kuwa yatosha sio tu kumshika Yesu mwenyewe bali hata vazi lake, na hapo anaweza kupokea uponyaji wa shida na tatizo lake. Ni imani inayomsukuma yule mama, “nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona”. Lugha yake inaonesha hakika kubwa anayokuwa nayo ndani. Pamoja na kuwa na imani kubwa katika uwezo wake Bwana wetu Yesu Kristo, mwanamke yule alikabiliwa na vizuizi viwili mbele yake, mosi ni katazo la kisheria ya kuwa yeye ni najisi hakupaswa kugusa wengine kwani kwa kufanya hivyo angeweza kuwaambukiza wengine unajisi wake, na pili kikwazo cha kimazingira kwani Mwinjili anatuambia uwepo wa umati mkubwa wa watu waliokuwa wakimfuata na kumsonga-songa Yesu.

Na ni kutokana na sababu hizo mbili tunaona mwanamke yule anaamua kugusa vazi la Yesu kwa siri, ndio kusema kuogopa kubanwa na sheria iliyomkataza kugusa au kugusana na wengine ili kuepuka kuwanajisi wengine. Mwanamke yule katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; naye akapata kupona msiba ule. Yafaa sasa tujaribu kuingia ndani ili tuweze kupata ujumbe kusudiwa katika muujiza huu wa uponyaji wa yule mwanamke. Mbele yetu tunasikia juu ya mwanamke ambaye hatajwi kwa majina, aliyekuwa na msiba wa kutokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Mwinjili tunaona leo anakazia juu ya hiyo namba kumi na mbili, kwani hata anapomzungumzia binti wa Yairo, mkuu wa sinagogi hatajwi jina lake bali umri wake wa miaka kumi na miwili. Ni hapo mara moja tunatambua kumi na mbili ni namba inayotumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu kulitambulisha Taifa teule la Israeli. Unajisi wa yule mwanamke asiyetajwa majina aliyekuwa na msiba wa kutokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, na pia umauti wa yule binti wa Yairo mkuu wa sinagogi aliyekuwa na umri wa miaka kumi na miwili, hali zote mbili zinaonesha hali duni ya ya kuhuzunisha ya taifa la Israeli. Ni hali ambayo hata wakuu wake wa dini badala ya kuliponya na kulisaidia taifa lile ndio walizidi kuwa kikwazo cha kulifanya taifa lile kushindwa kumuona aliye mkombozi wa kweli, anayeweza kuwajalia uhai wa kweli. Maradhi na magonjwa katika Maandiko Matakatifu ni ishara ya kifo.

Kwa Wayahudi si tu ugonjwa kama ule wa kutokwa na damu ulimfanya najisi aliyekuwa nao bali hata na wale aliogusana na kukaribiana nao. Hivyo wote waliendelea kuishi kwa hofu na mashaka makubwa. Hatari hii kama ilivyo kwa wakati huu wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Leo Yesu tunaona anatualika kubadili vichwa vyetu, ndio namna zetu za kufikiri na kutenda. Yesu badala ya kuwakimbia na kuwa mbali na wale wanaoonekana kuwa najisi na kutengwa na jamii na hasa jumuiya ya kiimani, ni yeye anaruhusu wamkaribie na hata kumgusa na hata hatumuoni akienda kujitakasa baada ya kuguswa na hawa walio najisi kama ilivyotakikana na sheria ya Walawi. Ni Yesu anajifunua na kuonesha uwezo wake wa kuleta uzima wa kweli badala ya kifo na mauti. Ni hapa Yesu anamuita na kumweka mbele ya wote, sio kwa nia ya kumfedhehesha au kumdhalilisha bali awe kielelezo cha imani. Ni wazi mwanamke yule akaingiwa na hofu na kutetemeka, ni kama anarudi tena katika hali yake ya umauti, hali yake duni ya kutokwa na damu. Badala yake anazidi kupokea hakika ya uponyaji wake, binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani. Ni Yesu anamfungua kutoka katika kila kifungo iwe cha kiroho na hata vya kijamii na kiimani. Hakuna hata mmoja wetu awe na maradhi iwe ya kiroho au ya kimwili yanayopaswa kutufanya kuwa mbali na Mungu kwani ni kwake tunaalikwa kukimbilia na kupokea uponyaji wa kweli iwe ule wa kimwili na zaidi sana wa kiroho.

Ni sisi sote kila mmoja ana uhitaji wa kumsogelea Bwana wetu Yesu Kristo ili kwake tuweze kupokea uponyaji wa miili na hata wa roho zetu, ili kwake tuweze kutakaswa na kuwa na uhai na uzima wa kweli. Mwanamke yule ambaye anawakilisha pia hali duni ya taifa lile la Israeli ni kielelezo kwetu leo, kuwa muhimu ni imani kwa Mungu, imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa njia ya hapo sisi tunakuwa huru kutoka hali duni na ya msiba. Imani ni mahusiano na Mungu, ni kuunganisha maisha yetu na Mungu mwenyewe, na hivyo hapo tunakuwa na hakika ya kuwa salama. Kila mara tunapojitenga na kuwa na Mungu hakika tunabaki katika hali ya msiba n aduni, kwani tunakosa uzima wa kweli ndani mwetu. Yesu pia anatufundisha nasi badala ya kuwatenga na kujiweka mbali na wale wanaonekana kuwa ni najisi na wadhambi, na badala yake kuwasaidia ili nao waweze kumfikia Yesu na kugusa vazi lake ili waweze kupokea uponyaji. Ni kuwasaidia katika safari ya imani ili waweze kumgusa Yesu kwa imani. Hakika umati ule mkubwa wengi walimgusa kama anavyosema Mwinjili walimsonga-songa, basi sisi tuwe sio tunaomsonga-songa Yesu bali tunaomgusa Yesu. Kumgusa Yesu ndio kuingia katika mahusiano naye na kinyume chake ni kubaki kuwa kama bendera fuata upepo, ndio kumsonga-songa.

Daima hatuna budi kutambua imani ni kumgusa Yesu, ni kugusana naye ni kuruhusu nguvu yake ya Kimungu ibubujike na kuingia ndani mwangu, kubadili maisha yangu, kunifanya kuwa kiumbe kipya. Makutano ndio sisi waamini wakristo ambao daima tunakuwa karibu na Yesu Kristo iwe kwa kulisikia Neno lake na pia katika Maadhimisho ya masakramenti yake. Neno la Mungu na ushiriki wetu wa masakramenti hauna budi kuwa ni matendo ya imani, yenye kutusaidia kumgusa Yesu, ili aponye na kutujalia uzima kwa kututoa katika umauti na msiba. Neno la Mungu tunalolisoma na kulisia kila siku halina budi kuliruhusu kuingia ndani mwetu na kutufanya kuwa watu wapya, masakramenti pia na hasa Ekaristi Takatifu hatuna budi kuruhusu kugusa na kugeuza maisha yetu, kujitahidi kila siku kuyafananisha maisha yetu na yake Bwana wetu Yesu Kristo. Mwinjili Marko anatuonesha pia muujiza wa binti Yairo aliyepokea uponyaji. Miujiza yote ya leo msisitizo ni katika IMANI. Na ndio kitu kinachounganisha miujiza hii ya leo kwani hitaji la lazima si kitu kingine chochote bali ni imani. Katika muujiza wa binti Yairo tunaona sio hali inazidi kuwa mbaya kuzidi ya yule mwanamke aliyekuwa najisi na kutengwa kwa kutokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, hapa mbele yetu sio hali mbaya tu bali ni kifo. Katika hali ya kawaida hatutegemei kuona lolote kutoka kwa Yesu kwani kama inavyoelezwa katika Injili kuwa binti yule hakuwa tena hai bali amekufa na hata kumsihi Yairo kukubali matokeo na hivyo kuacha kumsumbua mwalimu.

Lakini maneno ya Yesu kwa Yairo; “Usiogope, amini tu!” Ndio kusema Yesu anazidi kufunua kwetu uwezo wake wa Kimungu ambao unafanya kazi hata katika mazingira yale ambapo kibinadamu hatuna tena matumaini. Kijana hakufa bali amelala tu! Ni maneno ya kuchekesha na hata kukejeliwa kwa mtu yeyote yule mwenye akili timamu, kwani watu wale walikuwa na hakika juu ya kifo cha yule binti wa Yairo. Ni hapo tunaona kinachohitajika katika mahusiano yetu na Mungu ni imani, ni kujikabidhi mikononi mwake na kuwa na hakika na uwezo wake wa Kimungu. Ni kuwa na imani kwake hata katika mazingira ambayo kibinadamu hatuoni tena mbele. Ni Yesu anayejifunua uwezo wake si tu kwa maradhi na magonjwa bali hata juu ya kifo. Kifo hakina kauli ya mwisho mbele ya nguvu za Mungu! Ni wito wa Yesu hata kwetu leo tunapopitia magumu na vikwazo katika maisha na hasa katika safari yetu ya kuyafananisha maisha yetu na yake, hatuna budi kutambua silaha yetu kubwa na ya lazima si nyingine bali ni imani. Ni kwa njia ya imani pekee tutayashinda na kusonga katika safari ya kuwa wanafunzi na wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo. Imani, imani, imani! Imani sio kutokutumia akili, bali ni kuwa na hakika katika uwezo wake Mungu hata katika mazingira magumu na ya kukatisha tamaa, ni kujikabidhi na kumwachia Mungu mwenyewe aongoze maisha yetu, awe kiongozi na mchungaji wetu daima. Nawatakia Dominika na tafakuri njema.

24 June 2021, 15:41