Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Chombo ni Kanisa na Kristo Yesu ni Nahodha wake! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Chombo ni Kanisa na Kristo Yesu ni Nahodha wake! 

Tafakari Jumapili 12 ya Mwaka B wa Kanisa: Nahodha ni Yesu!

Mababa wa Kanisa tangu mwanzo katika sehemu hii ya Injili wanaliona Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Katika maisha na historia yake, Kanisa limekumbana na dhoruba mbalimbali, lakini limeweza kuvuka yote haya na kusonga mbele kwa sababu Kristo Yesu ndiye nahodha wa chombo hiki na kamwe hajawahi kulala na kukiacha chombo kizame!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Hakika baadhi ya miujiza inayosimuliwa katika Maandiko Matakatifu inatuacha na mshangao mkubwa: Mtini uliolaaniwa kwa kukosa kutoa matunda wakati si majira yake (Marko 11:13), maji yanageuzwa kuwa divai (Yohane 2:1-11), Yesu akitembea juu ya maji na Petro akimwomba naye atembee juu ya maji (Mathayo 14:22-33), Petro analipa zaka ya hekalu kwa kupata pesa kutoka kinywa cha samaki (Mathayo 17:24-27). Ili kupata ujumbe kutoka miujiza hii hatuna budi kuingia ndani kabisa bila kuishia katika miujiza tu. Muujiza wa leo pia ambapo Yesu anatuliza dhoruba ya upepo mkubwa baharini ni moja ya miujiza inayotutaka kutafakari zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Hata baada ya kulisoma somo la Injili ya leo mara moja tunaweza kuwa na maswali kadhaa. Mwinjili anatuambia kuwa ilikuwa jioni, na kama ni jioni iliwapasa kurejea nyumbani Kafernaumu na sio kuvuka na kwenda upande mwingine, maana bado swali kwa nini muda ule walivuka kwenda upande mwingine? Na zaidi sana kwa nini walienda upande wa Wagerasi, watu waliokuwa wapagani na waliochangamana na Wayahudi?

Na hata tukisoma zaidi Injili ya Marko tunaona kuwa Yesu hakupokelewa wala kufahamika vema katika nchi ile ya Wagerasi. (Marko 5:17). Na hata wafuasi wake wanaomwamsha ili awaokoe katika hatari ile ya dhoruba kubwa, na wanafanya hilo kwani waliamini katika uwezo wa Yesu, lakini Yesu anawakemea kwa kuwa hawana imani. Pia hata baada ya Yesu kuituliza dhoruba ile kubwa, tunashangaa kuona wanafunzi wake badala ya kufurahi wamejawa na uoga na hofu kuu. Ni kwa msaada wa maswali haya tunaweza sasa kuona somo la Injili la leo linatualika kwenda ndani zaidi ili kuweza kupata ujumbe kusudiwa. Si nia wala lengo la Mwinjili Marko kutupa simulizi tu la muujiza alioufanya Yesu wa kuituliza dhoruba, bali tangu mwanzo tunaona ni nia ya Mwinjili Marko kutusaidia hatua kwa hatua katika kumtambua Yesu ni nani, utambulisho wa Kimasiha unaojifunua hatua kwa hatua. Hivyo masimulizi na nia kuu ya Mwinjili Marko ni kumtambulisha Yesu kwetu, kwa kila mmoja anayetaka kukutana na kumjua Masiha basi Injili ya Marko ni msaada mkubwa kwetu. Ni Injili ambayo tangu mwanzoni inajaribu kujibu swali lile la; Yesu ni nani?

Leo tunakutana na chombo kikiwa baharini pamoja na vyombo vingine, zaidi sana pia chombo hiki kikielekea katika nchi ya wapagani, yaani Wagerasi, mawimbi makali na makubwa, giza la usiku maana ilikuwa jioni, Yesu amelala katika shetri na juu ya mto, upepo mkali, hofu na uoga uliowajaa wafuasi wa Yesu, ni moja kati ya lugha ya picha tunazokutana nazo mara nyingi katika Maandiko Matakatifu. Injili yetu ya leo inaanza na kutuambia muda wa muujiza ndio jioni na uelekeo wa chombo kile alimokuwemo Yesu na wanafunzi wake.  Ni jioni. Ndio kusema ni baada ya Yesu kumaliza utume wake ya kuusimika na kuutangaza Ufalme wa Mungu, wanafunzi wake wanaingia chomboni pamoja na Yesu na kuelekea upande mwingine, lakini wanakwenda wapi haswa ? Ni baada ya kusoma zaidi Injili ya Marko 5 :1, kuwa walikuwa wanaelekea katika nchi ile ya Wagerasi, waliokuwa wapagani. Na ndio tunaona mara moja kuwa katika nchi ile kulikuwepo na nguruwe malishoni mlimani, ambapo Yesu baada ya kumponya mtu aliyekuwa na pepo wachafu, pepo wale wakamwomba Yesu kutoka na kuwaingia nguruwe na hata nguruwe wale wakaishia wote baharini.

Uwepo wa nguruwe kati yao ni ishara tosha kuwa watu wale hawakuwa Wayahudi bali wapagani, kwani Wayahudi ni marufuku kufuga au kula nyama ya nguruwe. Chombo ndio ishara ya jumuiya ya Wakristo, ambao baada ya Yesu kukamilisha utume wake, wanaalikwa kutoka na kwenda kuitangaza Habari Njema ya wokovu kwa watu wote. Lakini tunaona chomboni lazima pia awepo na Yesu, kwani uwepo wake ni wa lazima na wa muhimu kwa usalama wa jumuiya ya Kanisa. Tunaona leo chombo kikiwa katikati ya safari kinakuwa katika hatari kubwa kwa upepo mkubwa na dhoruba. Mwinjili Marko anatuambia pia kulikuwa na vyombo vingine, ndio kusema Mwinjili anajaribu kutuonesha kuwa hata baada ya utume wa Yesu Kristo kukamilika hapa duniani, kulikuwa na jumuiya kadhaa za Kikristo katika Kanisa lile la mwanzo. Ilikuwa jioni ndio kusema ilikuwa giza. Giza katika Maandiko ni ishara hasi, ni kukosekana utaratibu kama ilivyokuwa mwanzo kabla ya uuumbaji. (Mwanzo 1 :2) Fujo ni kukosekana uwepo na hasa uweza wake Mwenyezi Mungu. Ni hapo katika uwepo wa giza tunaona yule muovu anatawala na hivyo tunaitaji uwepo wake Mungu ili kututoa na kutuacha salama katika mitego ya yule muovu.

Chombo kinasafiri saa ile ya giza, saa ile ya fujo, saa isiyokuwa ya mwanga wala utulivu. Ni saa ile ambayo chombo kinakuwa katika hatari kubwa na kupigwa na kuyumbishwa na upepo mkali wa dhoruba. Yesu anakuwepo chomboni lakini amelala katika shetri, sehemu ambayo kwa desturi anakaa nahodha, mwongoza meli au vyombo vya majini. Ni Yesu anayepaswa kuwa nahodha na rubani wa chombo kile yaani Kanisa lake, ni Yeye ambaye tunapaswa kumkimbilia na kumlilia. « Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia ? » (Marko 4 :38). Kauli hii ya wanafunzi wa Yesu inatuacha pia na maswali, ni wao wanaoona wanaangamia na mwalimu wao hakuwa katika hatari hiyo pamoja na ukweli kuwa wote walikuwa chomboni. Yesu hakuwa katika hatari ya kuangamia na zaidi sana hakujishughulisha na kuwaokoa wanafunzi wake waliokuwa hatari kwani alibaki amelala katika shetri juu ya mto.

Yesu amelala. Kulala katika Maandiko Matakatifu ni ishara ya kifo au umauti. (Ayubu 14 :12) Na hata Yesu pia alirejelea kifo cha rafiki yake Lazaro kuwa amelala (Yohane 11 :11), hata kwa kifo cha Binti Yairo, « Msichana hajafa, amelala tu » (Marko 5 :39-40. Lakini pia Mwinjili Marko anatuambia alilaza kichwa chake juu ya mto. Mto unaotajwa hapa kwa lugha ya Kigiriki unajulikana kama « proskephalaion », ndio kusema sio mtu wa kawaida tunayoitumia kwa kulala bali ni ule unaotumika kulaza kichwa cha mtu mfu wakati wa maziko. Na ndio tunaweza kuona Mwinjili Marko anapozungumzia juu ya Yesu alilala na pia alilaza kichwa chake juu ya mto, ni nia yake kutuambia juu ya kifo cha Yesu baada ya kumaliza utume na misheni yake ya kuutangaza ufalme wa Mungu hapa duniani. Chombo kikiwa ni Kanisa, linaalikwa kutoka na kwenda kupelekea Habari njema kwa watu wote. Kanisa katika kutumiza wajibu wa utume huo hakika litapatwa na misukosuko na dhoruba na upepo mkali. Yesu yupo chomboni, ndio kusema anasafiri pamoja na Kanisa lake lakini katika namna isiyoonekana kirahisi wka macho. Ndio maana anasema alikuwa kwenye shetri, sehemu ile ya nahodha, sehemu ile ya kiongozi wa chombo.

Pamoja hatumwoni kwa macho ya nyama kama walivyomwona wanafunzi wake miaka 2000 iliyopita, lakini bado ndiye kiongozi na rubani na nahodha wa chombo. Kama wanafunzi wale wa mwanzo hata nasi leo, kuna nyakati tunapitia na kuingiwa na kishawishi kuona kuwa Yesu hayupo pamoja nasi, ametuacha na hata hajali kuona sisi tunaangamia kwenye dhoruba na upepo mkali. Ni hamu na tamaa yetu kuona Yesu akisafiri na kuwa macho ili kuweza kuzuia na kukemea upepo wa dhoruba tukiwa safarini. Lakini Yesu leo anatufunulia Mungu anayelala, anayelaza kichwa chake juu ya mto. Ni Mungu anayekuja na kutuokoa kila mara tunapomlilia na kumuomba kwa dhati kwani hayupo mbali nasi, ni msafiri pamoja nasi. Lazima kufungua macho ya mioyo yetu na kumkimbilia hakika anatuokoa na kutulinda na kila aina ya hatari. Ni bahati mbaya sana kwani kama wale wanafunzi wa kwanza, hata nasi huwa tunatambua uwepo na kumkimbilia pale tunapokuwa hatarini na katika giza kubwa. Wanafunzi hawakujali uwepo na uwezo wake, na ndio maana tunaona wakajaribu kila njia kujiokoa wao wenyewe, ni mwishoni wanatambua uwepo wa Mwalimu wao na kumlilia na ndio maana Yesu anawakemea kwa kukosa imani.

Ni kishawishi walichokuwa nacho kukosa macho ya imani ili kuweza kuuona uwepo wa Bwana na Mwalimu wao kati yao, ni kosa langu na lako hata leo kwani kuna nyakati tunashawishika kuona ni kwa nguvu, akili na uwezo wetu wa kibinadamu tunaweza kumshinda yule muovu, tunaweza kusafiri wenyewe chomboni na kushinda kila aina ya dhoruba na upepo mkali na mawimbi ya baharini. Yesu anatuhakikishia kuwa yu pamoja nasi siku zote hata ukamilifu wa dahari. (Mathayo 28 :20). « Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii ? » Ni swali la haki kabisa kujiuliza kwani walijua hakika mwenye uwezo pekee wa kuamuru upepo na bahari ni Mungu pekee. Ndio kusema kama Yesu anaweza kuamuru na kuzitiisha upepo na bahari basi hakika Yeye ni Bwana, yaani, ni Mungu. Na ndio maana wamejawa hofu kuu, kama vile Musa baada ya kukutana na Mungu alijawa na hofu kuu, basi hata nao katika tukio la muujiza wa leo wanajawa na hofu kuu, ni hofu kuu inayotokana na ukweli kuwa wamekutana na Mungu. Ni hofu chanya, ni matunda na matokeo ya uwepo wa Mungu, hivyo ni kubaki na mshangao mkuu, ni mshangao unaochanyanyika pia na furaha.

Ndio tunaweza kuona muujiza huu anaotupatia Mwinjili Marko ni ufunuo wa Yesu kama Mungu, ni « Teofania », ni Mungu anayejifunua mwenyewe, uwezo na nguvu zake za Kimungu na hasa uwepo wake kati yetu katika hali isiyoonekana kwa macho ya nyama. Tuimbe na kusali pamoja na Mzaburi; « Unisalimishe, ee Mungu, maji yamenifikia mpaka shingoni. Nimezama katika matope mengi, hakuna mahali pa kuweka miguu. Nimeingia katika kilindi cha maji ; na mawimbi yananichukua » (Zaburi 69 :2-3) Tunaalikwa kusali sio tu nyakati tunapokuwa shidani bali kila wakati, na sala ya kweli ni matunda au matokeo ya upendo na imani yetu kwa Mungu. Kusali ni kuonesha upendo na imani yetu kwa Mungu, ya uwepo na uwezo wake wa daima ! Nawatakia Dominika na tafakuri njema.

18 June 2021, 09:26