Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu ni sherehe ya sadaka na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu ni sherehe ya sadaka na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Sadaka: Fumbo la Upendo wa Yesu

Sadaka ya Misa ni Sala ya Yesu Kristo mwenyewe anayejitoa sadaka kwa ajili ya wengi. Sisi tunaalikwa kushiriki pia katika fumbo la upendo wa Mungu usiokuwa na kipimo. Ekaristia ni mwaliko wa kushiriki fumbo la Yesu Kristo anayejitoa sadaka katika kila adhimisho la Misa Takatifu. Ekaristia ni sala ya Yesu Kristo mwenyewe ambamo nasi tunaalikwa kuingia na kushiriki katika fumbo hilo.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama! Jumuiya za waamini wa kwanza walikuwa wanakusanyika pamoja katika nyumba au makazi binafsi kila Dominika ili kuadhimisha fumbo la Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Ekaristia. Neno ευκαριστια (Eukaristia) ni neno la kigiriki likimaanisha shukrani. Hivyo Ekaristia ni sala ya Yesu Kristo mwenyewe tunayoalikwa nasi kushiriki katika fumbo la upendo wake Mungu kwa watu wake. Ni Mungu anayejitoa sadaka au zawadi kwa wokovu wa mwanadamu. Ni Mungu anayebaki nasi katika maumbo yale ya mkate na divai. Ni sala ya shukrani kwani ni Mungu anajitoa zawadi katika maumbo yale duni kabisa ya mkate na divai, ni Mungu anayekuja na kuwa chakula chetu cha kiroho. Wapendwa ni vema kukumbuka kuwa Sadaka ya Misa ni Sala ya Yesu Kristo mwenyewe anayejitoa sadaka kwa ajili yako na yangu. Sisi tunaalikwa kushiriki pia katika fumbo hilo la upendo usio na kipimo wa Mungu kwa kila kiumbe. Na ndio maana nasi hatuna budi kukumbuka kuwa Ekaristia ni mwaliko wa kushiriki fumbo la Yesu Kristo anayejitoa sadaka katika kila adhimisho la Misa Takatifu. Ekaristia ni sala ya Yesu Kristo mwenyewe ambamo nasi tunaalikwa kuingia na kushiriki katika fumbo hilo.

Ekaristia ni τεοφανια (Teofania), ni Mungu anayejidhihirisha na kujifunia katika maumbo yale duni ya mkate na divai. Ni Yesu Kristo mwenyewe anayebaki na Kanisa lake siku zote katika safari yetu ya wokovu kuelekea Yerusalemu mpya ya Mbinguni. Ni Yesu Kristo Mfufuka anayekuwa karibu na jirani kwa kila mmoja wetu kwani anabaki kuwa chakula chetu cha njiani. Katika Injili ya leo tunaona ni wafuasi wake Yesu Kristo wanaokuwa wa kwanza kutoa wazo la kushiriki Pasaka ile ya kale, hivyo wanamuuliza Bwana na Mwalimu wao ni wapi anataka wakamwandalie Pasaka. Wanafunzi wake wanataka kuadhimisha kumbukumbu ya kukombolewa kwao kutoka utumwa wa Wamisri. Bado hawakuwa wanajua kuwa ni jioni ile nao watashirikishwa Pasaka ya Agano Jipya, yaani kushiriki katika fumbo la Upendo la kumkomboa mwanadamu kwa kuutoa Mwili wake na kumwaga Damu yake pale Msalabani.

Wanaalikwa na Bwana waende mjini na kukutana na mtu fulani atakayewaonesha chumba cha juu kilicho tayari ili wamwandalie Pasaka. Ni chumba kikubwa kumaanisha ni mwaliko usiokuwa na ubaguzi wa aina yeyote. Ni sote tunaalikwa bila kujali tofauti zetu katika kushiriki Pasaka mpya. Pasaka ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima. Ni chumba kilicho tayari, na ndio kushirikishwa uzima na ukamilifu wa Kimungu. Ni kwa kushiriki katika Pasaka ya Upendo nasi tunapata uzima wa kweli, yaani muunganiko na Mungu mwenyewe. Mwinjili Marko pia anatuonesha katika sehemu ya Injili ya leo ile kanuni iliyotumika na jumuiya za waamini wa mwanzo katika Maadhimisho ya kiliturjia ya Kuumega mkate, ndio Ekaristia. Hapa Yesu Kristo anapoumega mkate anasema huu ni Mwili wangu! Na hii ni Damu yangu!  Huu sio tu mkate bali ni mimi mwenyewe, ni mwili wangu, na hii sio tu divai bali ni damu yangu. Ni maneno hayo kila anapotamka kuhani katika maadhimisho ya Ekaristia nasi pia tunashiriki kikamilifu katika fumbo lilelile la siku iliyotangulia kuteswa kwake.

Ni Yesu Kristo mwenyewe anayekuwepo katika kila adhimisho la Ekaristia. Na anatualika kula mwili wake na kunywa damu yake ili nasi tuweze kushiriki katika fumbo lile la upendo wa Mungu kwa kila kiumbe. Yesu Kristo anatoa maisha yake kama zawadi kwa kila mmoja wetu. Anajimega kwa upendo ili kuukomboa ulimwengu mzima. Ni mwaliko kwetu nasi kujitoa kwa sadaka katika maisha yetu ya siku kwa siku kwa ajili ya ndugu zetu. Ekaristia narudia ni zawadi ya upendo wa Mungu kwetu, hivyo nasi tunaoalikwa kushiriki katika fumbo hilo kubaki katika upendo huo. Twaeni mle wote na twaeni mnywe nyote ni mwaliko kwa kila mwanadamu kushiriki katika fumbo hilo la Ekaristia.

Ekaristia ni Agano la Mungu na mwanadamu, kama Agano la Kale lilifanyika pale mlimani Sinai.  Damu ni ishara ya uhai, na Altare ni ishara ya uwepo wa Mungu, na wote wanaoizunguka meza ile wanafanyika kuwa jumuiya moja. Ekaristia ni kifungo cha umoja, kwani sote tunaoshiriki Mwili na Damu yake tunaunganika na kufanyika mwili mmoja, yaani Kanisa. Yesu leo pamoja anatumia kanuni ya sala ambazo zilikuwa zinatumika na Wayahudi wengine katika mlo wa Kipasaka, anatumia maneno yanayotuacha na mshangao mkubwa. Huu ni Mwili wangu, twaeni mle wote, Hii ni Damu yangu twaeni mnywe nyote! Kuutoa Mwili na Damu yake ni kujitoa Yeye mwenyewe, ni Yeye anayekuwa mlo wa kweli wa kila anayeshiriki katika meza ile ya Ekaristia. Ekaristia ndio chimbuko na kilele cha maisha ya Kanisa kama watufundishavyo Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ndio kiini cha imani yetu na kushiriki ila karamu ya milele mbinguni tukiwa tungali bado duniani. 1Wakorintho 15:28. Nawatakia maadhimisho mema ya Dominika ya Mwili na Damu yake Bwana wetu Yesu Kristo!

03 June 2021, 09:50