Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay linaadhimisha Mwaka wa Ekaristi Takatifu ili kuzima kiu ya Ekaristi Takatifu na kukoleza majadiliano, upendo na mshikamano. Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay linaadhimisha Mwaka wa Ekaristi Takatifu ili kuzima kiu ya Ekaristi Takatifu na kukoleza majadiliano, upendo na mshikamano. 

Mwaka wa Ekaristi Takatifu Nchini Paraguay: Mshikamano & Upendo

Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay limetangaza Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu unaolenga kuganga na kuponya njaa na kiu ya Ekaristi Takatifu kwa kujikita katika majadiliano, ushiriki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kauli mbiu ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu ni “Yakafunguliwa macho yao, wakamtambua kwa kumega mkate”. Rej. Lk. 24: 31-32. Upendo zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii Sherehe ya Ekaristi Takatifu kwa mwaka 2021 anasema kwamba, Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya upendo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni shule ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa mwamini anayeshiriki Ekaristi Takatifu, hawezi kuwageuzia kisogo maskini na wale wote wanaopekenywa na baa la njaa duniani. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay, CEP, kuanzia tarehe 3 Juni 2021 limeanza maandali ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa katika ngazi ya Parokia. Mwezi Agosti 2021 itakuwa ni katika ngazi kijimbo. Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya waamini.

Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Hili ni Fumbo kubwa linalopaswa kuadhimishwa vyema; Kuabudiwa na Kutafakariwa kikamilifu. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: “Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje ya Misa. Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay, CEP., limetangaza kwamba, Mwaka 2021 ni Mwaka wa Ekaristi Takatifu unaolenga kuganga na kuponya njaa na kiu ya Ekaristi Takatifu kwa kujikita katika majadiliano, ushiriki na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kauli mbiu ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu ni “Yakafunguliwa macho yao, wakamtambua kwa kumega mkate”. Rej. Lk. 24: 31-32. Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay linapenda kutumia maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu kuwaingiza waamini katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuwapatia Katekesi makini katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekarisri Takatifu, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji.

Hii ni fursa nyingine tena ya kuweza kukutana na Kristo Yesu katika Maumbo ya Mkate na Divai, ili kuwaonjesha uwepo wake angavu. Maaskofu wanasema, watu wa Mungu nchini Paraguay wana njaa na kiu ya Ekaristi Takatifu, itakayowanyanyua na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, kukoleza majadiliano katika ukweli na uwazi pamoja na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Maaskofu Katoliki nchini Paraguay wanapenda kutumia maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi ili kusimama kidete katika kutafuta na kudumisha haki jamii; kuendelea kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuhakikisha kwamba, majadiliano ya kidini, kiekumene, kitamaduni na kisiasa yanapewa uzito wake, kwa kujielekeza zaidi katika maboresho ya elimu, ili iweze kuwaletea watu wa Mungu nchini Paraguay, ukombozi wa kweli, unaoshuhudiwa katika maisha ya Kikristo kwa ajili ya Mungu na jirani!

Maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu nchini Paraguay ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Mwaka wa Neno la Mungu ambao kwa bahati mbaya sana, umekumbwa na dhoruba kali ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kutokana na janga hili, waamini wengi wameshindwa kufaidika na matunda ya Maadhimisho ya Mwaka wa Neno la Mungu. Kutokana na kuzingatia itifaki ya kudhibiti janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.  waamini wengi walishindwa kuhudhuria Ibada mbalimbali zilizokuwa zimeandaliwa. Hili ni janga la kiafya ambalo limegusa na kutikiza hata masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kwa kugawana na kushirikishana karama na mapaji mbalimbali ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa kujitahidi kila mmoja wao, kuwa ni Ekaristi inayomegwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika ulimwengu huu ambao umegeuka na kuwa kama “tambara bovu” wanasema Maaskofu Katoliki wa Paraguay, kuna haja ya kuganga njaa na kuzima kiu ya: haki, ut una heshima ya binadamu; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa sababu uchafuzi mkubwa wa mazingira ni chanzo cha majanga asilia, umaskini, magonjwa pamoja na mahangaiko mbalimbali ya binadamu.

Wananchi wana kiu ya fursa za ajira, haki na amani; huduma bora ya elimu na afya. Watu wana kiu ya kutaka kuona wema na uadilifu wa wafanyakazi wa umma; ukweli, uwazi na uaminifu katika huduma na matumizi ya mali na rasilimali za umma. Wanataka kuona familia ya Mungu nchini Paraguay inasimikwa katika misingi ya uaminifu, udugu, mshikamano tayari kujikita katika mchakato wa majadiliano, upatanisho, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, ili kuendeleza misingi ya haki, amani na umoja wa Kitaifa. Maaskofu wanasema, waamini wana kiu ya kutaka kuona kwamba, Injili ya uhai inapewa kipaumbele cha kwanza dhidi ya utamaduni wa kifo na sera zake. Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu kwa watu wote, kumbe kuna haja ya kuhakikisha kwamba, waamini kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanajizatiti katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu mpya, kwa kuhimiza upendo na mshikamano; kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kuondokana na ulaji wa kupindukia, ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, unaowatumbukiza baadhi ya watu katika mifumo ya utumwa mamboleo. Ili kuweza kufanikisha yote haya, kuna haja kwa waamini kujenga dhamiri nyofu.

Janga Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 limesababisha madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Kumbe, maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu yanapania kuganga na kuponya madonda haya kwa kukazia upendo wenye huruma. Maaskofu Katoliki Paraguay wanasema, Mwaka wa Ekaristi Takatifu, uwasaidie waamini kukutana na Kristo Yesu na hii iwe ni fursa ya kumfahamu, kumpenda, kumtumikia na hatimaye, waweze kufika kwake. Ni wakati wa ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Fumbo la mwili wa Kristo yaani Kanisa. Upendo kwa Yesu wa Ekaristi umwilishwe kwenye uhalisia wa maisha ya kifamilia, kijamii na hatimaye Kitaifa. Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yanakwenda sanjari na huduma makini kwa watu wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Ekaristi Takatifu, na kama sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, linawaelekeza waamini, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuboresha maisha yao, ili kupambana na hatimaye, kuung’oa umaskini. Wajitahidi kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Waamini waendelee kujikita katika mchakato wa utamadunisho; majiundo na katekesi makini na endelevu ili kupambana na changamoto mamboleo mintarafu maisha ya kiimani, kimaadili na kiutu. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani tendaji, mchakato unaopania utakatifu wa maisha. Kwa wale waliobahatika kupata nafasi katika masuala ya kisiasa, wajitahidi kuhakikisha kwamba, wanashiriki vyema zaidi katika mchakato mzima wa kutafuta, kupanga na kutekeleza mipango hiyo. Kumbe, kila Mkristo ajitahidi kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni kikolezo makini cha Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume wa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kongamano hili litawawezesha waamini kutambua umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kukoleza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji.

Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) tayaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay linasema kwamba Mwaka wa Ekaristi Takatifu utafungwa rasmi huko Caacupè tarehe 24 Oktoba 2021.

Mwaka wa Ekaristi Takatifu
03 June 2021, 16:31