Tafuta

Kardinali Polycarp Pengo Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre: Huduma kwa Watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika. Kardinali Polycarp Pengo Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre: Huduma kwa Watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika. 

Kardinali Polycarp Pengo Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre: Huduma!

Kardinali Pengo alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Juni 1971, mikononi mwa Hayati Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga (1958 – 1994), siku ambayo anasema mwenyewe kamwe hataweza kuisahau kwani tangu mwanzo kabisa alimwambia Mama yake kwamba, angetamani kuwa Padre na shuhuda wa imani kama alivyokuwa Mtakatifu Polycarp.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam na Tanzania katika ujumla wake, inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kardinali Pengo alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Juni 1971, mikononi mwa Hayati Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga (1958 – 1994), siku ambayo anasema mwenyewe kamwe hataweza kuisahau kwani tangu mwanzo kabisa alimwambia Mama yake kwamba, angetamani kuwa Padre na shuhuda wa imani kama alivyokuwa Mtakatifu Polycarp. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Kardinali Pengo katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu kuanzia: Nachingwea na Tunduru-Masasi, Kardinali Pengo ameweza kusimama imara bila kuteteleka katika masuala ya imani, maadili na utu wema. Na kwa njia ya msimamo wake, akaweza kuiepusha Tanzania katika dhoruba na mawimbi makali yaliyokuwa yanaisonga nchi.

Kardinali Pengo katika maisha na utume wake, amekuwa ni chombo na shuhuda wa majadiliano ya kiekumene, kidini, kisiasa na kitamaduni; mambo yaliyosaidia kujenga na kuimarisha maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa; daima ni kiongozi aliyesimamia: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na kipaji cha unyenyekevu na usikivu, kiasi kwamba, alikuwa tayari kupokea watu, kuwasikiliza, kung’amua pamoja na kuwapatia ushauri. Kwa wale ambao wametekeleza kikamilifu ushauri wake, wamefanikiwa kupata suluhu ya changamoto zilizokuwa zinawaandama. Kardinali Polycarp Pengo ni kiongozi aliyebahatika kuwa na ushauri chanya katika changamoto za maisha. Katika maisha na utume wake, hasa kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, mafanikio makubwa yameonekana chini ya uongozi wake. Idadi kubwa ya Maaskofu walioko nchini Tanzania, wengi wao wamepitia katika mikono mwake, kama wanafunzi na hata akawaweka wakfu kuwa Maaskofu, ili waweze kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Ni kiongozi ambaye amewathamini sana vijana, akawawekeza amana, utajiri, uzoefu na mang’amuzi yake katika malezi, leo hii, Jimbo kuu la Dar es Salaam linaendelea kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu si tu kwa watawa na watu wa ndoa, bali hata kwa wingi wa Mapadre. Ameimarisha malezi, makuzi na majiundo endelevu na fungamani kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kama kielelezo cha ukomavu wa imani na mwanzo wa mchakato wa kujitegemea kwa rasimali watu, bila kusahau pia rasimali fedha. Jimbo kuu la Dar es Salaam ni kati ya Majimbo ambayo yana mwamko mkubwa katika kulitegemeza Jimbo kwa rasilimali fedha na vitu. Hizi ni juhudi za Kardinali Polycarp Pengo katika utume wake. Askofu Mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anaendelea kufafanua kwamba, Kardinali Pengo ni mtu mwenye msimamo na malengo katika maisha na amejitahidi kuhakikisha kwamba, anatekeleza malengo yake kwa wakati. Kabla ya kung’atuka kutoka madarakani, alijipangia kwamba, Jimbo kuu la Dar es Salaam liwe limefikia Parokia 100, lakini hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2019, Parokia za Jimbo kuu la Dar es Salaam zimeongezeka zaidi ya namba aliyokuwa amekusudia. Nia ilikuwa ni njema, kuhakikisha kwamba, waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wanapata huduma ya kichungaji kwa karibu zaidi.

Askofu Nyaisonga anasema, shukrani hizi kwa Kardinali Polycarp Pengo ni kwa niaba ya familia yote ya Mungu, nchini Tanzania. Kwa sadaka na majitoleo yake, yaliyowawezesha watu wa Mungu nchini Tanzania licha ya mawimbi mazito katika medani mbalimbali za maisha, kuendelea kusimama na kushikamana kama ndugu wamoja. Bado familia ya Mungu nchini Tanzania inahitaji kutumia hekima, busara na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Polycarp Pengo, alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 huko Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Juni 1971 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Na kwa kipindi cha miaka miwili yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1973 aliteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1977 alitumwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa la Lateran, Kitivo cha Taalimungu Maadili cha Alfonsianum, kilichoko mjini Roma. Aliporejea nchini Tanzania baada ya kuhitimu masomo yake, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenda kufundisha taalimungu maadili Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.

Kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1983 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Gambera na muasisi wa Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika, Kanisa la Tanzania linajivunia Seminari ya Segerea, matunda ya jasho na ubunifu wa Kardinali Polycarp Pengo. Tarehe 11 Novemba 1983 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na kuwekwa wakfu wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 1984 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Mtakatifu Yohane Paulo II. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Nachingwea hapo tarehe 19 Februari 1984. Tarehe 17 Oktoba 1986, akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lengo likiwa ni kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini katika kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Akasimikwa rasmi tarehe 12 Februari 1987. Tarehe 22 Januari 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuingia Jimboni tarehe 24 Mei 1990.

Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 12 Februari 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na kumsimika rasmi tarehe 21 Februari 1999. Tanzania ikaweka historia ya kupata Kardinali mpya miezi michache tu baada ya kufariki dunia, Kardinali Laurian Rugambwa. Tarehe 2 Septemba 1990 wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Tanzania, Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu mwandamizi, ndiye aliyetoa hotuba, wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa anazungumza na wakleri pamoja na watawa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alikazia kwa namna ya pekee uaminifu na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ari na mwamko wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Tarehe 12 Aprili 1994, Kardinali Pengo alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika na kukazia umuhimu wa waamini kumwilisha imani yao kila siku ya maisha kama ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu!

Kardinali Pengo alishiriki katika mkutano wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya kumchagua Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Machi 2013. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Kardinali Polycarp Pengo, akang’atuka kutoka shughuli za uongozi Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa ufupi, hii ndiyo historia ya Kardinali Polycarp Pengo ambayo imeandikwa kwa jasho, uvumilivu na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Kardinali Pengo
17 June 2021, 16:13