Tafuta

Askofu mkuu Renatus Nkwande, Mapadre na Makatekista wakutana na kuteta mazito katika mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Mwanza. Askofu mkuu Renatus Nkwande, Mapadre na Makatekista wakutana na kuteta mazito katika mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Mwanza. 

Askofu Mkuu Nkwande, Mapadre na Makatekista Wateta Jambo Zito!

Askofu mkuu Renatus Nkwande na Mapadre wake, walipata fursa ya kushinda na Makatekista, ili kujadiliana kuhusu: fursa, changamoto, matatizo na jinsi ya kunogesha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa waamini Jimbo kuu la Mwanza. Makatekista wamesema kwamba, kuna uhaba mkubwa wa walimu wa kufundisha dini shuleni! Mahusiano na Mapadre yaboreshwe zaidi.

Na Padre Kelvin Mkama, Jimbo kuu la Mwanza, - Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko kwa Barua yake Binafsi "Motu Proprio", "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” ameanzisha Utume wa Katekista ambao kimsingi ni huduma kale. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwamba, kuna mafundisho ambayo Mitume waliwarithisha baadhi ya waamini na kuwasihi kuyahifadhi Mapokeo waliyopokea, wapiganie imani, ili Kanisa liweze kuishi katika utakatifu na kukuza imani. Mama Kanisa anakiri kwa dhati kabisa kwamba, huduma hii imesaidia katika utume wa uinjilishaji na kwamba, Kanisa katika ulimwengu mamboleo linapongeza njia mbalimbali zinazoendelea kujitokeza ili kuliwezesha Kanisa lenyewe liendelee kuwa aminifu kwa Neno la Mungu, ili kwamba, Injili Takatifu iweze kuhubiriwa kwa kila kiumbe. Katika kipindi cha miaka elfu mbili iliyopita mihimili ya uinjilishaji imeonesha ufanisi mkubwa katika utume wake. Wakleri na watawa wameendelea kujisadaka kwa ajili ya kufundisha Katekesi, ili kwamba katekesi iweze kuwa ni chombo madhubuti cha kuimarisha imani kwa watu wote. Kuna baadhi ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ambayo yameendelea kujipambanua kwa ajili ya kufundisha Katekesi.

Mama Kanisa anawakumbuka kwa heshima na taadhima waamini walei waliojisadaka usiku na mchana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa njia ya mafundisho ya Katekesi. Hawa ni watu waliokuwa na imani thabiti na mashuhuda wa utakatifu wa maisha, baadhi yao wakaanzisha Makanisa na wengine kuitupa mkono dunia kwa njia ya ushuhuda wa kifodini. Hata leo hii, kuna Makatekista mashuhuri ambao ni viongozi wa Jumuiya zao na wanasaidia pia kurithisha na ukuzaji wa imani kwa watu wa Mungu. Kuna jeshi kubwa la wenyeheri, watakatifu na mashuhuda ambao ni Makatekista waliolisongesha mbele Kanisa na kwa hakika wanahitaji kutambuliwa, kwa sababu wao ni utajiri mkubwa na amana ya Katekesi pamoja na historia nzima ya tasaufi ya Kikristo. Tangu Baba Mtakatifu Francisko achapishe Barua yake Binafsi "Motu Proprio", "Antiquum ministerium" yaani “Huduma kale” kumekuwepo na mwamko kwa Kanisa kuwasikiliza na kuwaenzi Makatekista katika maisha na utume wao kwa watu wa Mungu. Mwamko huu umepelekea kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania kuendesha semina na hija kwa Makatekista wake.

Ni katika muktadha huu, Jimbo kuu la Mwanza nchini Tanzania, kuanzia tarehe 8 hadi 11 Juni 2021 katika Chuo Cha Makatekista Bukumbi, Jimbo kuu la Mwanza kumefanyika semina iliyoendeshwa na Padre Titus Amigu kutoka Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT). Kati ya mada zilizochambuliwa ni: dhamana na wajibu wa Katekista; Changamoto za utandawazi, Historia ya Kanisa, Jinsi ya kushinda hofu za uchawi na ushirikina. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza na Mapadre wake, walipata fursa ya kushinda na Makatekista, ili kujadiliana kuhusu: fursa, changamoto, matatizo na jinsi ya kunogesha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Mwanza. Makatekista wamesema kwamba, kuna uhaba mkubwa wa walimu wa kufundisha dini shuleni. Kwenye baadhi ya Parokia, hakuna uhusiano mwema na wenye tija kati ya Mapadre na Makatekista wao.

Makatekista wengi hawajapikwa wala kufundwa barabara kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala, hivyo inakuwa ni vigumu sana kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao nyeti kwa watu wa Mungu. Kuna baadhi ya Makatekista, wamekuwa ni wazembe kutekeleza dhamana na wajibu wao mbele ya Kanisa. Kuna baadhi ya viongozi wa Halmashauri Walei wanaoingilia na kuvuruga utume wa Makatekista Parokiani na Vigangoni na hivyo kukwamisha juhudi za katekesi kwa watu wa Mungu. Makatekista wamewaomba wakleri wa Jimbo kuu la Mwanza kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kuleta ufanisi na tija katika mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Mwanza. Makatekista wameomba kuwezeshwa kupata zana, vitabu na miongozo ya kufundishia: Katekesi, somo la dini, maadili na utu wema shuleni. Wakleri wametakiwa kuwathamini, kuwapenda, kuwajali na kuwategemeza Makatekista, ili nao waweze kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Mapadre nao kwa upande wao, kwanza kabisa waliwapongeza Makatekista kwa kazi kubwa ya uinjilishaji wanayoitekeleza katika hali na mazingira magumu. Mapadre wamesikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya Makatekista hawatimizi vyema wajibu na dhamana yao kutokana na: uzembe, ulevi, tamaa na kukosa uaminifu kwa rasilimali fedha. Mapadre wamewaomba Makatekista kuendeleza dhamana na wajibu wao kwa watu wa Mungu kadiri ya miongozo ya Kanisa. Watekeleze wajibu huu kwa ibada na uchaji wa Mungu; kwa nidhamu na unadhifu, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Ili kuweza kukabiliana na baadhi ya changamoto hizi katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Mwanza, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande anawasihi walimu wakatoliki kujitolea kufundisha somo la dini shuleni, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Askofu mkuu Nkwande amekazia umuhimu wa mihimili ya uinjilishaji kushirikiana, kushikamana na kupendana kama ndugu wamoja ili kunogesha mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mapadre wawajengee mazingira bora zaidi Makatekista wao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili kwa watu wa Mungu.

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande amekazia umuhimu wa elimu kwa watoto wa Makatekista pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata makazi bora ya kuishi. Elimu bora na makini itawasaidia kujikwamua kutoka katika dimbwi la hofu, mila na tamaduni zilizopitwa na wakati, tayari kujielekeza na kutembea katika mwanga wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! (Mbina ja mabasa yaani ngoma za mapacha” au “Kugema mbula). Makatekista wa Jimbo kuu la Mwanza wamempongeza Askofu mkuu Nkwande kwa kujenga daraja ya mahusiano mema miongoni mwa mihimili ya uinjilishaji. Wameanza kuchangia ujenzi wa Kituo cha Mafungo na Semina cha Makatekista Jimbo kuu la Mwanza. Wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha mradi mkubwa unaotarajiwa kuboresha malezi na majiundo makini na endelevu ya Makatekista Jimbo kuu la Mwanza.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makatekista wanaitwa kuwa ni wataalamu na wahudumu wa jumuiya ya waamini katika kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani katika hatua mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu. Waanzie hatua ya kwanza ya kutangaza Injili, “Kerygma”, kufundisha maisha mapya katika Kristo Yesu sanjari na kuwandaa waamini kwa ajili ya kupokea Sakramenti za Kanisa na hatimaye, kuendelea na majiundo endelevu ili kila mwamini aweze kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu anayemuuliza habari za tumaini lililo ndani mwake; lakini kwa upole na kwa hofu. Rej. 1Pet.3:15. Makatekista wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa imani, waalimu, wandani wa imani na walimu wanaofundisha kwa niaba ya Kanisa. Yote haya yanaweza kutekelezwa kwa njia ya sala, masomo na ushiriki wa moja kwa moja katika maisha ya jumuiya yanayoweza kukuza utambulisho na uwajibikaji wake wote.

Makatekista Mwanza
24 June 2021, 16:19