Tafuta

Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales kwa Sherehe ya Pentekoste 2021: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote. Waraka wa Kichungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales kwa Sherehe ya Pentekoste 2021: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote. 

Waraka wa Sherehe ya Pentekoste 2021: Utunzaji Bora wa Mazingira!

Roho Mtakatifu ni “Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa kwa Manabii”. Mungu amejifunua katika Kazi ya Uumbaji, changamoto kwa watu wa Mungu kutumia vyema uhuru na utashi wao kwa ajili ya kuheshimu, kupenda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote! Mazingira! Laudato si!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Kwa maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, Mitume wa Kristo Yesu walitambua kwamba, wanayo dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote bila ubaguzi. Roho Mtakatifu anawataka waamini wote kutangaza imani na kumbukumbu endelevu ya Kristo Yesu kati yao kwa njia ya umoja. Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa uinjilishaji na umoja wa wale wanaotangaza na kushuhudia Injili. Mitume walikuwa na ari na mwamko wa kuwashirikisha watu wa Mungu kile ambacho walikuwa wamepokea! Roho Mtakatifu ni kiini cha siri ya umoja kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowashirikisha wengine, ili kuweza kumfahamu Mungu anayeleta mageuzi katika sakafu ya maisha ya mwamini na kuendelea kutunza mazingira nyumba ya wote! Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales katika Waraka wao wa kichungaji kama sehemu ya Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2021, linapenda kuwakumbusha waamini kwamba, Kazi ya Uuumbaji ambayo pia inajulikana kama Injili ya Uumbaji ni zawadi kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kimsingi Roho Mtakatifu ni “Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa kwa Manabii”. Mwenyezi Mungu amejifunua katika Kazi ya Uumbaji, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kutumia vyema uhuru na utashi wao kwa ajili ya kuheshimu, kupenda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote. Pentekoste inaadhimishwa tarehe 23 Mei 2021 mwishoni mwa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si” litakalofikia kilele chake tarehe 25 Mei 2021 sanjari na kufunga rasmi “Mwaka wa Laudato si.” Huu ni muda muafaka kwa Kanisa kupima mafanikio yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Mwaka wa “Laudato si” katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” kuhusu mazingira inakazia kuhusu mwingiliano wa viumbe vyote. Kumbe, Kanisa linaona kwamba, kuna umuhimu wa pekee kukazia dhamana na wajibu wa Kanisa katika kuendeleza Kazi ya Uumbaji na kama kielelezo cha imani tendaji katika ulinzi wa mazingira nyumba ya wote, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu!

Maaskofu wanasema, kumekuwepo na ulaji wa kupindukia ambao umekuwa ni chanzo cha uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kuwa na teknolojia rafiki itakayoheshimu na kutunza mazingira, ili kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayoendelea kusababisha athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Jumuiya ya Kimataifa itambue wajibu wake wa pamoja kwa ajili ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utambuzi huu ni changamoto ya kujikita katika kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, kwa kuwaangalia maskini wanaoathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Utunzaji bora wa mazingira ni dhamana na wajibu wa kila mtu mintarafu: hali na mzunguko wa maisha, vipaumbele na maamuzi yanayofikiwa na kutekelezwa kila kukicha, bila kusahau matumaini kwa siku za mbeleni. Maamuzi yanayofanywa na watu mbalimbali madhara yake yanagusa mchakato wa maboresho ya mazingira nyumba ya wote. Haya ni maamuzi yanayofanyika mintarafu: chakula, matumizi ya maji na nishati; safari pamoja na utunzaji wa taka zinazozalishwa na zinazoweza kutumiwa tena. Haya ni mambo yanayoweza kutekelezwa na mtu binafsi kama wito wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote!

Maadhimisho ya Pentekoste kwa mwaka 2021 yanakuja kama kipindi cha neema na baraka baada ya itifaki za kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 kuanza kulegezwa. Hii inaonesha kwamba, watu wakijikita katika nidhamu, kanuni maadili na utu wema wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uso wa dunia. Mwezi Juni 2021 Uingereza itakuwa ni mwenyeji wa G7. Mkutano wa 26 wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 utafanyika kuanzia tarehe 1-12 Novemba 2021 huko mjini Glasgow nchini Scotland. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Leo hii, kuna maafa na majanga makubwa yanayotokana na ukame wa kutisha, mafuriko pamoja na majanga ya moto sehemu mbalimbali duniani. Matokeo yake ni watu wengi kuanza kunyemelewa na baa la njaa, utapiamlo wa kutisha, umaskini na magonjwa ya milipuko.

Kumbe, mikutano hii miwili ni muhimu sana katika kupanga sera na mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kujikita zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kimsingi Roho Mtakatifu ni “Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana” anayewahimiza waamini kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu, ili aieneze nyoyo ya waamini wake; awashe moto wa mapendo, vitaumbwa upya na sura ya nchi itageuka.

Maaskofu Uingereza
18 May 2021, 14:50