Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni mwanzo kwa waamini kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe! Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni ni mwanzo kwa waamini kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe! 

Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Mbinguni: Nendeni Ulimwenguni!

Kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda mbinguni ni fundisho la Kanisa. Ambalo tunasadiki katika Kanuni ya Imani. “Siku ya tatu akafufuka katika wafu akapaa mbinguni, akaketi kuume kwa Mungu Baba". Utume: Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri habari njema Kabla ya kupaa anawapa baraka ili wakawabatize watu. Nasi tumebatizwa na tunatumwa kumhubiri Yesu Kristo.

Na Padre Nikas Kiuko, - Mwanza, Tanzania.

Kanisa, tarehe 13 Mei 2021 linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Yesu Kristo Mbinguni, ingawa kutokana na sababu za kichungaji, Sherehe hii itaadhimishwa rasmi, Jumapili tarehe 16 Mei 2021 sanjari na Siku ya 55 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa Mwaka 2021 inayonogeshwa na kauli mbiu “Njoo uone”, Yn 1:46. Kupaa kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwenda mbinguni ni fundisho la Kanisa. Ambalo tunasadiki katika Kanuni ya Imani. “Siku ya tatu akafufuka katika wafu akapaa mbinguni, akaketi kuume kwa Mungu Baba. Kabla ya kupaa anawapa mitume majukumu mazito. Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri habari njema Kabla ya kupaa anawapa baraka ili wakawabatize watu. Nasi tumebatizwa na tunatumwa kumhubiri Yesu Kristo. Kwa nini kupaa kwakwe sisi kwetu ni sherehe?

TAFAKARI: Maisha ya hapa ulimwenguni ya Bwana wetu Yesu Kristo yalianza kwa fumbo la Umwilisho na kumalizikia kwa fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo, ufufuko na kupaa mbinguni kwa shangwe. Simulizi lilianza kwa kuacha enzi na utukufu wake mbinguni na kuja ulimwenguni na kumalizika kuacha ulimwengu na kurudi mbinguni. Ilianza kwa ahadi na kumalizika katika utimifu. Leo Mitume wapo katika mshangao mkubwa wanapo mwona Yesu akipaa. Tofauti na alivyokuja ambapo wengi tulifurahia ujio wake kwa Sherehe ya Noeli wengi walifanya sherehe kubwa, walipeana kadi, walialikana na kupeana zawadi, muziki ulichezwa na nyuso za furaha kwa wote kwa fumbo hilo la umwilisho. Ni vigumu kwa watu kufanya hivyo katika sherehe ya kupaa Bwana wetu Yesu Kristo Mbinguni.  Tulifurahia kuzaliwa kwa Yesu Kristo hata kama hakufanya chochote, alizaliwa katika mazingila ya duni kabisa. Tunapatwa na mshangao mkubwa kwa Yesu kurudi kwa Baba baada ya utume uliotukuka wa hapa duniani wagonjwa walipona, aliwasaidia vipofu, aliwasaidia wajane, aliwasaidia yatima sasa kurudi kwake baada ya utume ingekuwa sherehe kubwa ya kumshukuru kwa upendo wake mkuu. Ipi sahii kusherekea ujio wake au kuondoka kwake?

Yesu Kristo baada ya ufufuko aliwaandaa Mitume kwa muda wa siku 40, akiwafunulia Maandiko Matakatifu. Kisha akaziangazia akili zao iliwapate kuelewa Maandiko Matakatifu (Luka 24:45). akiwa na wafuasi kuelekea Emau.  Akiwafundisha Maandiko Matakatifu kuanzia Musa hadi manabii. Aliwafafanulia Maandiko na sheria. Mpango wa Mungu wa kuwakomboa watu wote.  Mateso, kifo na ufufuko wake, hivyo aliwaandaa mpaka wakajua maandiko. Lakini bado Mitume walifadhaika walipo ambiwa na Yesu kama bado kitambo kidogo hamtaniona (Yohane 16:16-20).Yawezekana walikuwa wanajiohoji itakuwaje? Kwa mwendo gani? Atachukuliwa na upepo wa kisulisuli kama Eliya? Hawakuwa na majibu ya maswali mengi. Hapo ndipo hofu iliwajaa. Wapendwa Kupaa kwa bwana wetu Yesu Kristo ni fumbo linalozidi ufahamu wetu, akili zetu za kisayansi na uwezo wetu wa kuelewa. Ni fundisho la Kanisa kwamba Akapaa mbinguni ameketi kuume kwa Mungu Baba mbinguni.

Alipo kuwa akiwabariki akachukuliwa mbinguni. Baraka ya namna gani hiyo? Baraka iliyojaa Amani, neema, huruma, wokovu, faraja na upendo. Baraka iliyowaondolea maswali mengi, hofu, Yesu aliwaandaa mitume wake kuondoka.  Ni mwaliko kwetu tupende Baraka, tubariki familia zetu, makazi yetu, nyumba zetu, watoto wetu na sehemu zetu za biashara tukaribishe Baraka ya Mwenyezi Mungu. Mitume wakapata ujasiri wa kumshuudia Bwana wetu Yesu Kristo akipaa, (Matendo 1:9. Wakawakumbuka Elia (2Wafalme 2), na Enok katika kitabu cha (Mwanzo 5:4). Mitume walipata ujasiri wa kufanya alicho waagiza baada ya Baraka na kupaa, maana hata alipokuwa akifunualia maandiko wakielekea Emau walimtambua katika kuumega make na akatoweka mbele yao. (Luka 24:13-35) Hivyo haikuwa shida wakiona anapaa. Baada ya hapo walimwabudu, huu ndio wajibu wao mkubwa waliofanya.  Kuabudu kwa moyo. Kuthamini ukuu wa Mungu, (Ufunuo 5:12) Walirudi Yerusalemu kwa furaha kubwa. Hi ni sababu kwa nini kupaa kwake sisi ni sherehe. Furaha ya nini wakati hawata isikia sauti yake, mafundisho na miujiza yake?

 Furaha waliyo kuwanayo ni furaha ya kujua maandiko matakatifu, maana tumeambiwa aliwafundisha maandika matakatifu kwa muda wa siku 40 baada ya ufufuko wake. Na sasa yupo mbinguni, kama neno la Mungu limetimia Zaburi 2.  Nimwaliko kwetu.Tujitahidi kusoma maandiko matakatifu, maana yeye mwenyewe anasema yupo katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa na kati ya maskini na wanyonge ndani ya jamii. Wamefahamu kwamba, Yesu Kristo ni mfalme Zaburi 72:8.) Mitume wakajawa na furaha, walijua kuwa Mungu amemkweza juu kabisa, akampa jina lilokuu kuliko majina yote (Wafilip 2:9-11). Walirudi kwa furaha na wala hawakuwa na maumivu, huzuni kwa kuondokewa na Yesu, hawakuomboleza wala kuwa na mahangaiko yote yalifunikwa kwa kuyafahamu maandika matakatifu. Hivyo matokeo ya Kupaa Yesu mitume walibaki wakisali, Nasi tunaalikwa kudumu katika kusali, kuziombea familia zetu, maeneo yetu ya kazi wakuu wetu wa kazi Mungu awaongoze na waweze kutenda haki.  

13 May 2021, 08:57